Papa Francisko Aanzisha Tume ya Mashahidi Wapya, Mashuhuda wa Imani: Uekumene wa Damu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Jubilei hii ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Kumbe, kama sehemu ya maandalizi ya Jubilei ya Mwaka 2025, waamini wanahamasishwa kujikita katika sala, chemchemi ya baraka na neema zote. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo, Baba Mtakatifu Francisko tarehe 5 Julai 2023 ameanzisha Tume ya Mashahidi Wapya, Mashuhuda wa Imani kwenye Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu. Lengo ni kuandaa orodha ya majina ya waamini walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Ikumbukwe kwamba, Wafiadini ndani ya Kanisa ni Mashuhuda wa matumaini yanayobubujika kutoka katika Injili ya Kristo Yesu na kukita mizizi yake katika upendo wa kweli. Tumaini huweka hai imani ya kina kwamba, wema una nguvu kuliko uovu, kwa sababu Mwenyezi Mungu katika Kristo Yesu ameshinda dhambi na kifo. Tume hii itaendeleza tafiti ambazo zimeanza tangu wakati wa Maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, kuwatambua Mashuhuda wa imani katika robo hii ya kwanza ya Karne ya Ishirini na moja na kisha kuendelea katika siku zijazo.
Tangu awali hadi leo hii, Wakristo wanaitwa kutoa ushuhuda mkubwa mbele ya watu wote, hasa mbele ya madhulumu. Kwa hiyo kifodini (Martyrium) ambacho kwa njia yake mwanafunzi anafananishwa na mwalimu wake aliyekubali kwa hiari kufa kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu, na kulinganishwa naye katika kuimwaga damu, kinathaminiwa na Mama Kanisa kwa kuwa ni karama bora na uhakikisho mkuu wa upendo. Ingawa ni wachache wanaokirimiwa neema hii ya kifodini, lakini waamini wote wanapaswa kuwa tayari kumkiri Kristo Yesu mbele ya watu wote, na kumfuata katika Njia ya Msalaba kati ya madhulumu ambayo hayakosekani kamwe katika Kanisa. Rej. LG 42. Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, kwa hakika wafia imani wameandamana na maisha ya Kanisa katika kila zama na wanastawi wakiwa ni “matunda yaliyoiva na bora ya shamba la Mzabibu la Bwana”. Wafia imani ni wengi zaidi katika zama hizi kuliko katika karne ya kwanza. Hawa ni maaskofu, mapadre watawa na waamini walei na familia zao ambao katika nchi mbalimbali za ulimwengu wana tuzo ya maisha yao na kwamba, wamethibitisha upendo mkuu. Kama vile Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alivyoandika tayari katika Waraka wake wa Kitume “Tertio millennio adveniente” Yaani “Mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo” alikaza kusema, “Kila kitu lazime kifanyike ili kuhakikisha kwamba, wingu kubwa la askati wasiojulikana wa kazi ya Mungu haupotei. Tayari tarehe 7 Mei 2000 walikumbukwa katika maadhimisho ya kiekumene, ambayo yalishuhudia wawakilishi wa Makanisa na jumuiya za kikanisa kutoka sehemu zote za dunia wakikusanyika katika Magofu ya Coloseo yaliyoko mjini Roma ili kuamsha, pamoja na Khalifa wa Matakatifu Petro utajiri wa yale ambayo yatafafanuliwa baadaye na Baba Mtakatifu Francisko. Huu ndio uekumene wa damu. Pia katika Jubilei ya Miaka 2025 Waamini wengi watajikuta wameungana ili kulisherehekea tukio hili kubwa katika maisha na utume wa Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, hakuna vigezo vipya kuhusu wafia imani, bali ni mwendelezo wa kile kilichoanzishwa hadi sasa kwa sababu hawa wanauwawa kwa vile tu ni Wakristo. Huu ni mwendelezo wa kihistoria utakaoliwezesha Kanisa kukusanya shuhuda za wakristo walioyamimina maisha yao, ili kumbukumbu yao iendelee kung’ara kama amana na utajiri unaohifadhiwa na Jumuiya ya Kikristo. Tafiti hizi zitajumuisha Makanisa yote ya Kikristo, kwani Wakristo kwa njia ya Ubatizo wao, wanaendelea kuhatarisha maisha yao kwa njia ya ushuhuda pamoja na kushiriki Ibada ya Misa Takatifu kila Dominika. Kuna baadhi ya mashuhuda wa imani wanayamimina maisha yao wakati wakiwa wanatoa huduma ya upendo; kwa kuwalinda na kuwatunza maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; na wengine wanauwawa wakati wakitangaza na kushuhudia Injili ya amani sanjari na nguvu ya msamaha. Kuna baadhi ya waamini kama mtu mmoja mmoja au kama kundi la waamini wanaendelea kuchangia katika historia mamboleo. Wote hawa, Mama Kanisa analo deni kubwa sana kwao na kamwe hawawezi kusahaulika. Tume ya Mashahidi Wapya, Mashuhuda wa Imani kwenye Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini Kuwa Wenyeheri na Watakatifu itaendeleza orodha ya wafia imani wanaotambulika rasmi na Mama Kanisa na shuhuda zao zilizohifadhiwa ili kwa pamoja waweze kutambulikana kuwa ni “Mashuhuda Wakristo” “Martyria”. Tume hii inatarajia kupata ushirikiano wa dhati kutoka kwenye Makanisa mahalia, Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume pamoja na ukweli unaobubujika kutoka kwa Makanisa yote ya Kikristo. Katika ulimwengu mamboleo, uovu unaonekana kutawala zaidi! Kumbe Orodha ya Mashuhuda wapya wa imani katika Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, itakuwa ni msaada mkubwa katika mwanga wa Pasaka ya Bwana, wakichota kutoka huko uaminifu mwingi wa ukarimu kwa Kristo Yesu kwa sababu za maisha na wema.