Vatican na Vietnam Wawekeana Saini Mkataba wa Ushirikiano wa Kidiplomasia
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi jioni tarehe 27 Julai 2023 amekutana na kuzungumza na Rais Vo Van Thuong wa Vietnam ambaye baadaye alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Vatican na Vietnam baada ya mazungumzo yaliyofanyika tarehe 31 Machi 2023 kati ya Kikosi kazi cha majadiliano kati ya Vitenam na Vatican na hivyo kufikia hatima ili kuanzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia kwa Vietnam kuwa na Mwakilishi wa kudumu mjini Vatican na kwa upande wake, Vatican kuwa ni mwakilishi mwenye makazi yake nchini Vietnam. Viongozi hawa wawili wamepongeza maendeleo makubwa ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Vietnam sanjari na mchango wa Kanisa Katoliki nchini Vietnam katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Viongozi hawa wawili waomeonesha imani na matumaini yao kwamba, Mkataba huu utawasaidia wawakilishi wa nchi hizi mbili kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao na kwamba, Mkataba utakuwa ni nyenzo msingi kwa waamini wa Kanisa Katoliki kutekeleza dhamana na wajibu wao, huku wakiheshimu sheria za nchi, daima wakijitahidi kufuata Mamlaka Fundishi ya Kanisa yaani “Magisterium” katika kuwasindikiza watu wa Mungu nchini Vietnam ili waendelee kuwa Wakatoliki na raia wema, huku wakiendelea kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mwakilishi wa Vatican nchini Vietnam atakuwa ni faraja na kiungo cha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Vietnam.
Kardinali Pietro Parolin, katika mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican amesema, huu ni mchakato unaopania kuziwezesha nchi hizi mbili kufahamiana kwa karibu zaidi, mchakato ulioanzishwa kunako mwaka 1989 kwa wakati huo na Kardinali Roger Etchegaray, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Haki na Amani alipotembelea kwa mara ya kwanza nchini Vietnam, ili kuanzisha mchakato wa majadiliano, haki na amani; mafundisho jamii sanjari na ushuhuda wa Wakristo mawazo makuu ya Mtakatifu Yohane Paulo II. Tangu wakati huo, kukaanzishwa utamaduni wa wawakilishi wa Serikali kutembelea mjini Vatican. Mwaka 1996 Vatican ikaanzisha Mkataba kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahalia.
Mwaka 2009 Rais Nguyen Minh Triet akakutana na Baba Mtakatifu Benedikto XVI mjini Vatican, mwanzo wa majadiliano ya kuwa na Mwakilishi wa Vatican nchini Vietnam, Askofu mkuu Leopoldo Girelli, tarehe 13 Januari 2011 akiwa anaishi nchini Singapore. Kikosi kazi cha majadiliano kati ya Vatican na Vietnam kilisimika majadiliano yake katika ukweli na uwazi; uhuru wa kidini, sheria za nchi ya Vietnam; mazingira yatakayomwezesha Balozi wa Vatican kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa watu wa Mungu nchini Vietnam, huku Wakristo wakijitahidi kuishi vyema Ukristo wao na hivyo kuendelea kuwa ni raia wema mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Majadiliano ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa Kanisa Katoliki kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu na kwamba, uteuzi wa Maaskofu mahalia umetekelezeka bila shida wala mgogoro wowote.
Kardinali Parolin anakaza kusema, Balozi wa Vatican ni kiungo cha mahusiano na Kanisa mahalia katika kushereheka maisha na utume wake. Balozi mkazi atakuwa na dhamana ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na Serikali ya Vietnam mintarafu sheria, kanuni na taratibu za nchi ya Vietnam na kwamba, Balozi wa Vatican atakuwa ni kiungo na daraja kati ya Vatican na Vietnam. Watu wa Mungu nchini Vietnam kwa hakika ni wachapa kazi, wanyenyekevu na wenye kuheshimu watu wengine. Kumbe, Mkataba huu ni mwaliko kwa pande zote mbili kutembea kwa pamoja, ili kuboresha zaidi mahusiano haya mapya kwa kuheshimiana na kuaminiana.