Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia barua wakleri wa Jimbo kuu la Roma wakati huu wanapotekeleza dhamana na wajibu wao kwa Mungu na Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia barua wakleri wa Jimbo kuu la Roma wakati huu wanapotekeleza dhamana na wajibu wao kwa Mungu na Kanisa.  (Vatican Media)

Barua ya Baba Mtakatifu Francisko Kwa Mapadre wa Jimbo kuu la Roma: Ushuhuda!

Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia barua wakleri wa Jimbo kuu la Roma wakati huu wanapotekeleza dhamana na wajibu wao kwa Mungu na Kanisa, huku wakiwa wamesheheni furaha, matumaini na hata wakati mwingine hali ya kukata tamaa, mwaliko wa kujifunza kutoka kwa Kristo Yesu aliyewaonea huruma Mitume wake, kiasi hata cha kuwaalika akisema, “njooni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo” Mk 6:31. Ushuhuda!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia barua wakleri wa Jimbo kuu la Roma wakati huu wanapotekeleza dhamana na wajibu wao kwa Mungu na Kanisa, huku wakiwa wamesheheni furaha, matumaini na hata wakati mwingine hali ya kukata tamaa, mwaliko wa kujifunza kutoka kwa Kristo Yesu aliyewaonea huruma Mitume wake, kiasi hata cha kuwaalika akisema, “njooni ninyi peke yenu kwa faragha, mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo” Mk 6:31. Baba Mtakatifu katika barua hii anawashukuru na kuwapongeza wakleri wa Jimbo kuu la Roma kwa ushuhuda, mwaliko ni kubaki wakiwa wameungana na Kristo Yesu ili waweze kuzaa matunda. Anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa karibu wakati wa furaha, mateso na mahangaiko pamoja na faraja za kichungaji. Wajifunge kibwebwe kupambana na malimwengu ya maisha ya kiroho yanayojikita kwa mwonekano wa nje pamoja na kutaka kujikweza, hali inayowafanya kujitafuta wenyewe. Badala yake, wakleri wamtazame Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Washirikiane kwa karibu na waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa, katika kipindi hiki cha ukanimungu, kamwe wasikate tamaa, wajikite katika maisha ya sala ili kweli waweze kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa Habari Njema ya Wokovu. Mwishoni, anawashukuru wakleri wa Roma kwa kuupokea ujumbe wake, waendelee kushikamana katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ili kweli waweze kuwa ni wachungaji wapendwa wa Kristo Yesu, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya upendo wake usiokuwa na kifani.

Papa Francisko anawashukuru na kuwapongeza wakleri wa Jimbo kuu la Roma
Papa Francisko anawashukuru na kuwapongeza wakleri wa Jimbo kuu la Roma

Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake kwa wakleri wa Jimbo kuu la Roma anasema, anawakumbuka wakati huu wa likizo ya kipindi cha kiangazi na anapenda kuwashukuru na kuwapongeza kwa ushuhuda, huduma na yale yote wanaotekeleza hata katika kificho, anawashukuru kwa msamaha na faraja wanayotoa kwa ajili ya watu wa Mungu hata wakati mwingine bila ya kutambuliwa. Lakini watambue kwamba, ufanisi wa shughuli za kichungaji hautegemei mafanikio ya shughuli za kichungaji, jambo la msingi ni kuendelea kushikamana na kuambatana na Kristo Yesu ili kuweza kuzaa matunda kwani Kristo Yesu ni chemchemi ya huruma na kwa neema yake anawawezesha Mapadre wake kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika shughuli za kichungaji, kwa kukubali na kupokea mafanikio na hali ya kushindwa; kufurahi na kuendelea kuwa wanyenyekevu na wavumilivu, daima wakiwa tayari kuanza upya sanjari na kuwanyooshea mkono jirani zao, ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu; huku wakiwa na uhuru wa ndani unaowawezesha kukabiliana fika na changamoto za shughuli za kichungaji. Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia wakleri wa Roma uwepo wake wakaribu wakati wa furaha na majonzi, katika mahangaiko na hali ya kukata tamaa. Anapenda kuwafariji ili kwa pamoja Jimbo kuu la Roma liweze kustawi katika ushirika na upendo na hivyo kuendelea kuwa ni mfano wa huruma na mapendo, wachungaji wake wakiwa tayari kujivika huruma ya Mungu, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa walimwengu. Mwenyezi Mungu anawataka kujikita zaidi katika mapambano dhidi ya malimwengu ya maisha ya kiroho ambayo ni hatari sana kwa maisha na utume wa Kanisa kimaadili na kiutu.

Papa Francisko anawataka Mapadre kumwangalia Kristo Mfufuka
Papa Francisko anawataka Mapadre kumwangalia Kristo Mfufuka

Hii ni hali ya maisha inayojikita katika mwonekano wa nje, watu wanaofikiri na kutenda kama walimwengu, kwa kumezwa na uchu wa mali na madaraka, tabia ya ubinafsi na kutaka kujikweza; kwa ugumu wa moyo na ukali katika kutekeleza sheria. Baba Mtakatifu anakaza kusema, malimwengu ya kiroho, yanajificha nyuma ya mwonekano wa moyo wa ibada na pengine hata nyuma ya kulipenda Kanisa, yanahusu kutafuta si utukufu wa Mwenyezi Mungu, bali utukufu mwanadamu na ustawi wa mtu binafsi. Rej. Evangelii gaudium, 93. Hiki ni kielelezo cha unafiki katika maisha na utume wa Kanisa. Kuna haja ya kuwa makini katika maisha ya kiroho kwa kuruhusu nguvu ya Roho Mtakatifu iweze kuwatakasa kutoka katika undani wa maisha yao ili waweze kuwa wakweli kutoka moyoni. Kwa kumezwa na malimwengu ya maisha ya kiroho, baadhi ya wakleri hujikweza kupita kiasi na kuona kana kwamba, wana upendeleo wa pekee kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kinyume kabisa cha mshikamano wa upendo wa udugu wa kibinadamu na hivyo kusahahu dhamana waliojivika wakati walipokea Sakramenti ya Ubatizo ambayo inawafanya kuwa ni: Makuhani, Manabii na Wafalme. Kumbe, wakleri wanapaswa kukuza moyo wa unyenyekevu, kwani ole wao wachungaji wanaojilisha wenyewe na kushindwa kuwatia nguvu na kuwaponya wagonjwa; kuwafunga waliovunjika; kuwarudisha waliofukuzwa na kuwatafuta walio potea.

Mapadre pambaneni ya malimwengu ya maisha ya kiroho
Mapadre pambaneni ya malimwengu ya maisha ya kiroho

Kumbe jambo la msingi ni kujitahidi kumwilisha Neno la Mungu linalowaangazia katika mapito ya maisha yao bila ya kujitaabisha kutafuta: umaarufu, mali na utajiri mambo yanayochafua ari, huduma na moyo wa kipadre; kiasi hata cha kuvuruga mipango ya shughuli za kichungaji na hivyo kuonekana kana kwamba si mali kitu. Hii ni kwa sababu ya uchoyo na ubinafsi, mchungaji hujitafuta mwenyewe; anakosa ile neema, sadaka na majitoleo; mambo yanayo mpendeza Mungu ikiwa kama yanamwilishwa katika huduma kama anavyokaza kusema, Kristo Yesu “Mmepata bure, toeni bure” Mt 10: 8. Baba Mtakatifu anasema, ili kuepuka kumezwa na malimwengu ya maisha ya kiroho, wanapaswa kumwangalia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Kristo Yesu ni kielelezo cha umoja na unyenyekevu “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya Msalaba.” Flp 2:7-8. Kwa kuyaangalia Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu, wakleri wajifunze kujisadaka bila ya kujibakiza kwa kuwa ni mkate unaotolewa kwa wenye njaa na hivyo kushirikiana safari na wale wote wanaoteseka na kunyanyasika; yaani kuwa kweli ni watumishi wa watu wa Mungu, tayari kuwaosha miguu watu wa Mungu badala ya kuwakanyaga na kuwakandamiza. Mtakatifu Paulo Mtume na Mwalimu wa Mataifa ni mfano bora wa fadhila ya unyenyekevu.

UNyenyekevu, umoja na mshikamano ni muhimu kwa uchungaji
UNyenyekevu, umoja na mshikamano ni muhimu kwa uchungaji

Baba Mtakatifu anatoa angalisho pia kwa waamini walei wanapotekeleza dhamana na wajibu wao kwa kujijengea kuta na hivyo kujifungia katika undani wao na hivyo kumezwa na kiburi. Dalili za mambo haya ni pale waamini wanapokosa furaha na kuanza kulalama kwa kila jambo, wakali na watu wanaojipambanua kwa kukosoa, kiasi hata cha kusahau unyenyekevu wa Kiinjili, heshima na msaada wa udugu wa kibinadamu. Baba Mtakatifu anawakumbusha wakleri wa Jimbo kuu la Roma kwamba, licha ya udhaifu na mapungufu ya kibinadamu, lakini Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu, changamoto na mwaliko wa kujikita katika sala ili kukuza na kujenga ushirika katika utekelezaji wa sera na mipango ya shughuli za kichungaji. Kuna haja ya kujikita katika toba na wongofu binafsi na ule wa kichungaji kwa kurejea kwenye chemchemi za Kiinjili, ili kuvunjilia mbali tabia ya kutenda kwa mazoea. Baba Mtakatifu anawashukuru wakleri wa Jimbo kuu la Roma kwa kupokea ujumbe huu wanaopaswa kuutafakari mbele ya Kristo Yesu katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Huu ni mwaliko wa kusonga mbele kwa ari na ujasiri mkuu; kwa kujenga umoja na ushirika na waamini walei kama sehemu ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ili faraja ya Kristo Yesu iweze kuwafikia na kuwaambata watu wote wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, akiwa mbele ya Sanamu ya Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” amesali na kuwaombea wapate ulinzi na tunza ya Bikira Maria; awapanguse machozi na kuwaamshia ndani mwao furaha ya utume wa Kipadre na hatimaye, kuwawezesha kila siku kuwa ni wachungaji wapendwa wa Kristo Yesu, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya upendo wake. Mwishoni Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wakleri wa Jimbo kuu la Roma kwa yale wanayotenda na kwa jinsi walivyo!

Barua kwa Mapadre wa Roma

 

08 August 2023, 15:07