Kardinali Nzapalainga Anaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya Daraja Takatifu ya Upadre
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kardinali Dieudonné Nzapalainga, C.S.Sp. Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati alizaliwa tarehe 14 Machi 1967 Jimboni Bangassou. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kitawa na Kipadre tarehe 6 Septemba 1997 akaweka nadhiri zake za daima kwenye Shirika la Roho Mtakatifu “Congregatio Sancti Spiritus sub tutela Immaculati Cordis Beatissimae Virginis Mariae”: Spiritans” na hatimaye, tarehe 9 Agosti 1998 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 14 Mei 2012 Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu na kuwekwa wakfu tarehe 22 Julai 2012 na tarehe 29 Novemba 2012 akasimikwa rasmi kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati.
Tarehe 19 Novemba 2016 Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Kardinali na kusimikwa rasmi tarehe 18 Desemba 2016. Kwa ufupi kabisa, Kardinali Dieudonné Nzapalainga, C.S.Sp. Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bangui amekwisha litumikia Kanisa kama Padre kwa miaka 25, kama Askofu akiwa na dhamana ya kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu kwa muda wa miaka 11 na kama Kardinali kwa muda wa miaka 6. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre, Baba Mtakatifu Francisko katika katekesi yake, Jumatano tarehe 9 Agosti 2023 ametumia fursa hii kumshukuru na kumpongeza kwa zawadi ya maisha na wito wa Kipadre. Amewatakia heri na baraka mahujaji na wageni wote waliofika kutoka Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati kuhudhuria Jubilei hii ya Miaka 25 tangu Kardinali Dieudonné Nzapalainga, C.S.Sp. Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre.