Kwa wote
ANDREA TORNIELLI
“Kanisa ni mahali pa kila mtu... Kila mtu, kila mtu, kila mtu!”. Papa Francisko alirudia mara kadhaa kwa vijana nusu milioni waliomkaribisha jana jioni tarehe 3 Agosti 2023 katika Bustani ya Edoardo VII mjini Lisbon. Papa alionekana kuhuishwa na kutiwa nguvu tena na shauku ya wasichana na wavulana ambao, pamoja na wachungaji wao na waelimishaji wao, walifika Ureno kutoka ulimwenguniko kote. “Kwa kila mtu, turudie”, Francisko alipaza sauti. Ni ujumbe ambao unaweza takriban kuwakilisha muunganisho wa miaka kumi ya kwanza ya Upapa. Upapa uliofunguliwa kwa ishara ya huruma. Je hii inamaanisha nini kuthibitisha tena kwamba kuna nafasi kwa kila mtu katika Kanisa? Papa Francisko alisema: “Hakuna mtu asiyefaa, hakuna aliye bora, kuna nafasi kwa kila mtu. Kama sisi sote tulivyo ... “Padre, lakini nina bahati mbaya, nina bahati mbaya: ipo nafasi yangu?”: kuna nafasi kwa kila mtu”. Kwa sababu “Mungu anatupenda, Mungu anatupenda jinsi tulivyo, si vile tungependa kuwa au jinsi jamii inavyotaka tuwe: jinsi tulivyo. Anatupenda kwa kasoro tulizo nazo, kwa mapungufu tuliyo nayo na kwa nia tuliyo nayo ya kusonga mbele kimaisha. Hivi ndivyo Mungu anatuita: tumaini kwa sababu Mungu ni Baba, na yeye ni Baba atupendaye, Baba anayetupenda.”
Wakati ambapo kila mtu anatoa maoni na hakuna anayesikiliza, wakati ambapo wengi wanajaribu kuonekana jinsi wasivyo, hakuna ujumbe wa kuvutia na wa kimapinduzi kama huu: Mtu anatupenda jinsi tulivyo, hutusamehe kila wakati, anakaa pale kutusubiri kwa mikono iliyo wazi, huenda mbele yetu akiwa tayari kutupatia huruma. Ni mantiki ambayo si ya kibinadamu hata kidogo na ya kimungu kabisa tunayojifunza kutokana na tukio la kiinjili kuhusu Zakayo, mtoza ushuru mwenye dhambi asiyependwa na kila mtu katika jiji la Yeriko ambaye, akihisi kutaka kujua kuhusu nabii wa Nazareti, alipanda mti wa mkuyu na kusubiri, akiwa nusu anaoneka katikati ya matawi ya mti.
Yesu alimtazama kwanza, akampenda kwanza, akajikaribisha nyumbani kwake bila kujali maoni ya kashfa ya waliopo. Hakuna masharti ya awali ya kukutana na kumbatio la huruma ya Yesu. Hakuna “maelekezo” ya kujikita katika vitendo, hakuna kozi za maandalizi ya kuhudhuria au mbinu za kujifunza. Inatosha kuwa pale anapopita, kujisalimisha kwa macho yake yaliyojaa upendo na huruma. Acha tu vizuizi vianguke na kumruhusu atukumbatie, tukimtambua katika nyuso za mashahidi ambao anawaweka kwenye njia yetu kila siku. Kuna nafasi kwa kila mtu katika Kanisa, kama vile ilivyokuwa nafasi kwa Zakayo mtoza ushuru ambaye alipata fursa ya kumpokea Mnazareti nyumbani kwake, kwenye meza yake mwenyewe. Mshangao usio na kifani, zawadi ya bure, ambayo ilitokea kwa neema safi.
Mtazamo huo, mwito huo ulivuruga maisha ya mtoza ushuru wa Yeriko: kwa sababu alipendwa sana kuliko wakati mwingine wowote maishani mwake, aliweza kuelewa ni kiasi gani cha dhambi na ni kiasi gani cha upotovu kilihusisha kuwepo kwake. Lakini uongofu kwa Zakayo haukuwa sharti la lazima ili kupendwa na kusamehewa. Nguvu ni tofauti: hasa kwa sababu alihisi kukaribishwa, kupendwa na kusamehewa kwa mara ya kwanza, aliweza kutambua dhambi yake na ufisadi wake. Kupitia hurumaa ya kimungu kulimfanya atambue kwamba yeye ni mtenda dhambi maskini.
Mwaliko ambao Papa alirudia kati ya vijana, alioambukizwa na shauku yao, ni ufunguo wa uinjilishaji leo hii. Kwa hakika, ni nini kingine tunachohitaji ikiwa si Mtu anayetukumbatia jinsi tulivyo, na kutufanya tujisikie kuwa tunatarajiwa, tunatafutwa, tunapendwa na kusamehewa? Ni nini kingine tunachohitaji ikiwa hatutaambiwa: kuna nafasi kwako pia, kwa hali yoyote uliyo nayo?