Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko imehitimisha maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa “Parque Tejo.” Baba Mtakatifu Francisko imehitimisha maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa “Parque Tejo.”   (ANSA)

Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni: Ibada ya Misa Takatifu Kufunga Siku ya Vijana

Papa imehitimisha maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa “Parque Tejo." Amegusia: Tukio la kung’ara Bwana na jinsi ambavyo vijana wameshiriki mang’amuzi yao na Kristo Yesu, changamoto kubwa ni kung’arisha upendo wa Mungu kwa jirani zao; Mmsikieni Yeye anapozungumza katika Maandiko Matakatifu, Sala, kwa kusikilizana wao kwa wao, ili kujenga utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi. Inukeni

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tarehe 6 Agosti 2023, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kung’ara Bwana Yesu Kristo, yaani akiwa Mlimani Tabor aligeuka sura mbele ya Mitume wake Petro, Yakobo, na Yohane nduguye. Uso wake ukang’aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. Rej. Mt 17:2. Hili ni tukio ambalo Kristo Yesu alipenda kuwafunulia Mitume wake na kwa njia hii, watu wote utukufu wake. Akawaonesha kwamba, hatima ya maisha ya mwanadamu ni kuelekea mbinguni kwa Baba wa milele. Hii ni changamoto ya kuendelea kujizatiti kikamilifu katika kuuponya Ulimwengu kutokana na uharibifu na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote na kuendelea kuujenga Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anawakumbusha watoto wake kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Benedikto XVI, akifanya tafakari kuhusu Sikukuu hii anasema kwamba, huu ni muhtasari wa Mafumbo ya Imani ya Kanisa, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, ili aweze kuwaimarisha wafuasi wake katika hija ya mwanga wa imani. Ni kielelezo cha mshikamano wa dhati kati ya Kristo Yesu na kazi ya uumbaji ambayo ameikomboa kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Mama Kanisa katika maadhimisho haya, anaungama kwa dhati kabisa kuhusu: Ubinadamu na Umungu wa Kristo; Kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu na Mkombozi wa dunia sanjari na kuzaliwa kwa Kanisa Sakramenti ya wokovu kwa binadamu! Sikukuu hii inagusa kwa namna ya pekee, umuhimu wa Kanisa kusimama kidete kulinda na kutunza kazi ya uumbaji kama anavyokaza kusema Mtakatifu Damascene. Katika maadhimisho ya Sikukuu ya Kung’ara Bwana, Kanisa kwa mwaka huu, 2023, linafanya kumbukizi ya miaka 44 tangu Mtakatifu Paulo VI alipofariki dunia, “Dies natalis” akiwa kwenye Ikulu ndogo ya Castel Gandolf, nje kidogo ya mji wa Roma na kuzikwa tarehe 12 Agosti 1978 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia habari Njema ya Wokovu
Kanisa linatumwa kutangaza na kushuhudia habari Njema ya Wokovu

Tarehe 6 Agosti 2023 ni kilele cha Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno inayonogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Hii ni hija ya 42 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa na ni mwendelezo wa tema kuhusu dhamana na utume wa Bikira Maria katika maisha ya Kanisa. Baba Mtakatifu imehitimisha maadhimisho haya kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa “Parque Tejo.” Katika mahubiri yake, amegusia kuhusu: Tukio la kung’ara Bwana na jinsi ambavyo vijana wameshiriki mang’amuzi yao na Kristo Yesu, changamoto kubwa ni kung’arisha upendo wa Mungu kwa jirani zao; Mmsikieni Yeye anapozungumza katika Maandiko Matakatifu, Sala, kwa kusikilizana wao kwa wao, ili kujenga utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi. Inukeni wala msiogope kwani Kristo Yesu ndiye dira na mwongozo wao wa maisha na kwamba, anawafahamu fika kutoka katika undani wa maisha yao. Uwanja wa “Parque Tejo” ulikuwa umefunikwa na bahari ya vijana waliofika kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuadhimisha Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, wengi wao wamekesha uwanjani hapo ili kushiriki Ibada ya Misa Takatifu. Tukio la Kristo Yesu kung’ara Uso mbele ya Mitume wake Petro, Yakobo na Yohane lilipania kuwaandaa ili kukabiliana kikamilifu na Kashfa ya Fumbo la Msalaba, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu, tayari kuambatana na kukumbatia mpango wa upendo wa Mungu kwa binadamu. Kung’ara huku kulipania kuwaimarisha wafuasi wake nyakati za giza wakati wa mateso yake mjini Yerusalemu na Njia ya Msalaba kuelekea Mlimani Kalvari. Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, hata wao katika safari ya maisha yao kuna nyakati za giza, lakini Kristo Yesu ndiye mwanga angavu unaoendelea kung’ara hata kati kati ya giza nene!

Watu zaidi ya milioni moja na nusu wamehudhuria
Watu zaidi ya milioni moja na nusu wamehudhuria

Katika mwanga wa Kristo Yesu, hata vijana nao wanapaswa kung’ara katika ujana wao, kwa kutangaza na kushuhudia mwanga wa Injili sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, wanaitwa na kutumwa kuwa ni nguzo za matumaini katika nyakati za giza nene! Baba Mtakatifu anawaambia vijana kwamba, wataweza kung’ara katika maisha, ikiwa kama watamkaribisha Kristo Yesu katika sakafu ya nyoyo zao na kujifunza kupenda kwa dhati kama yeye mwenyewe anavyopenda, kiasi hata cha kutuhubutu kuhatarisha maisha kwa ajili ya upendo, kwa kutuhubutu kupenda hata kile ambacho kimsingi hakipendwi. Kwa maneno mengine anasema Baba Mtakatifu ni kuwapenda jirani jinsi walivyo na kwamba, jambo hili linawezekana kwa msaada wa mwanga angavu wa Kristo Yesu, kwa kuvunjilia mbali maamuzi mbele na hivyo kuwakirimia watu mwanga wa upendo wa Kristo Yesu unaookoa, huku wakiendelea kung’ara kwa sababu Kristo Yesu “ni nuru ya ulimwengu.” Yn 8:12. Mwinjili Mathayo anasema, “Msikieni yeye” Mt. 17:5. Huu ni mwaliko kwa wafuasi wa Kristo Yesu kuhakikisha kwamba, wanajenga utamaduni wa kumsikiliza Kristo Yesu kwa njia ya Neno lake na kulimwilisha katika uhalisia wa maisha, na kuendelea kufuata nyayo zake kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Baba wa milele na kwamba, kwa njia ya Roho Mtakatifu waamini nao wamekuwa watoto wapendwa wa Mungu. Vijana katika maisha wasitafute umaarufu, mafanikio makubwa katika maisha au fedha na mali. Bali wanapaswa kumsikiliza Kristo Yesu ili watambue kwamba, wanapendwa na kuthaminiwa na Kristo Yesu na kamwe hawezi kuwaangusha.

Umati mkubwa wa vijana umehudhuria
Umati mkubwa wa vijana umehudhuria

Huu ni mwaliko wa kujenga utamaduni wa hata wao wenyewe kusikilizana, kwa kuwa makini na tamaduni za watu mahalia; kwa kutoa kipaumbele cha pakee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama aliyejeruhiwa kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Inapendeza ikiwa kama vijana watajenga utamaduni wa kumsikiliza Kristo Yesu, kusikilizana wao kwa wao, ili hatimaye, kujenga utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi katika ulimwengu huu ambao umegubikwa na ubinafsi na uchoyo wa kutupwa! Baba Mtakatifu anawataka vijana kung’ara, kusikiliza na hatimaye kutoogopa. “Inukeni, wala msiogope.” Mt17:7 Ni maneno ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake, baada ya kushuhudia utukufu wake na kusikililiza sauti ya Baba yake wa milele, sasa anawataka kushuka kutoka mlimani, ili kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku. Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa hata kwa vijana wa kizazi kipya, ikiwa kama watang’arisha mwanga na maneno ya Kristo Yesu katika maisha yao, nyoyo zao zitakuwa huru dhidi ya woga na hofu za maisha kiasi hata cha kudhani kwamba, ndoto zao zitaendelea kubaki kuwa ndoto na wala hazitatekelezwa; kwa kuogopa changamoto za maisha au kukatishwa tamaa ya maisha kutokana na maumivu. Vijana wanahamasishwa kuleta mabadiliko ulimwenguni kwa kujikita katika mchakato wa haki na amani na kwamba, Kanisa linawategemea vijana kama ardhi inavyotegemea mvua. Vijana watambue kwamba wao ni matumaini ya ulimwengu kumbe, hawana sababu ya kuogopa!

Watu milioni 1.5, Maaskofu 700 na Mapadre 10, 000
Watu milioni 1.5, Maaskofu 700 na Mapadre 10, 000

Kama vile Mtakatifu Yohane Paulo II alivyowahi kuwaambia vijana wa kizazi kipya kwamba, Kristo Yesu ndiye kilele cha ndoto na furaha yao na kwamba, yupo daima anawasubiri kwani Kristo Yesu ni uzuri wanaoutamani na kuutafuta, ili kuwaweka huru sanjari na kutekeleza matamanio yaliyomo ndani ya nyoyo zao bila kukatishwa tamaa na wengine. Kristo Yesu ndiye anayewawezesha vijana kutenda mambo makuu katika maisha, changamoto na mwaliko kwa vijana ni kuhakikisha kwamba, wanajiaminisha kwa Kristo Yesu! Jambo la msingi ni kutoogopa kwa sababu Kristo Yesu anawaona, anawafahamu na anawapenda upeo! Mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya imani inayoleta vuguvugu katika nyoyo za wat una upendo wa dhati katika yale mambo wanayofanya. Vijana wawe ni mng’ao wa mwanga wa Kristo Yesu, wasikivu ili hata vijana nao, waweze kuwa ni mwanga wa Mataifa; Kamwe wasiogope kwa sababu Kristo Yesu anawapenda upeo na anatembea kandoni mwao. Kwa kuambatana na Kristo Yesu, maisha yanapyaishwa!

Maadhimisho ya Siku ya Vijana 2027 ni Korea ya Kusini
Maadhimisho ya Siku ya Vijana 2027 ni Korea ya Kusini

Wakati huo huo, Kardinali Manuel José Macário do Nascimento Clemente, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lisbon, Ureno, katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kuongoza Ibada ya Misa Takatifu ili kufunga rasmi Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa uwepo na ushiriki wake mkamilifu katika Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni na kwamba, Kanisa linaendelea kumwombea maisha marefu na afya njema katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Matakatifu Petro. Baba Mtakatifu ameshuhudia umati wa vijana wa kizazi kipya kutoka sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Ni wakati wa vijana kujenga: umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Maadhimisho ya 37 ya Vijana Ulimwenguni ni kazi kubwa ya Baba Mtakatifu Francisko, kwa kutoa mwaliko kwa vijana kuhudhuria kwa wingi, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kwa kusimikwa katika udugu wa kibinadamu. Amewashukuru wote walioshiriki kwa hali na mali katika kufanikisha Maadhimisho haya na mwishoni, amemshukuru Mungu kwa Ibada hii ya Misa Takatifu!

Vijana wawe ni nguzo ya imani,matumaini na mapendo
Vijana wawe ni nguzo ya imani,matumaini na mapendo

Naye Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha mara baada ya Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, kilelel cha Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwawezesha vijana kuadhimisha imani sanjari na kutangaza na kushuhudia upendo wa Kristo unavyowaka ndani mwa nyoyo zao. Mama Kanisa hakukata tamaa, mwaka 2020 Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni yaliyohairishwa kutokana na maambukizi makubwa ya janga la Virusi vya Ugonjwa wa Korona, UVIKO-19. Kwa maombezi ya Bikira Maria wa Fatima, ndoto hii imejamilika. Kuna umati mkubwa wa vijana ambao haukuweza kuhudhuria, lakini umeshiriki kwa njia ya mitandao katika sala, ujenzi wa udugu wa kibinadamu na utume wa vijana. Naye Kardinali Kevin Joseph Farrell, anamshukuru Baba Mtakatifu kwa kutangaza na kushuhudia upendo wa Mungu kwa waja wake bila ubaguzi; amekoleza matumaini miongoni mwa vijana; haki, amani na maridhiano na kwamba, amemwonesha Bikira Maria kuwa ni mwandani wa hija ya imani. Amewaombea vijana baraka ili waendelee kuwa ni Mitume wamisionari, Wakiongozwa na haraka ya Bikira Maria, vijana wawe ni vyombo na mashuhuda wa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu kwa watu wote, Roho Mtakatifu apende kuwaimarisha kama mahujaji wa matumaini.

Papa Vijana 2023
06 August 2023, 15:26