Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni 2023: Muhtasari Wake

Baba Mtakatifu amegusia kuhusu mkutano wake na viongozi, vyama vya kiraia na wanadiplomasia; safari yake kwenye Madhabahu ya B.Maria wa Fatima kwa ajili ya kuombea amani duniani pamoja na Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana kwa kumwangalia Bikira Maria kama kielelezo cha huduma, imani na matumaini. Siku za vijana ulimwenguni ni chemchemi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kwamba, Kristo Yesu amepandikiza mbegu ya matumaini miongoni mwao

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 6 Agosti 2023 Sikukuu ya Kung’ara Bwana amehitimisha Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni Jimbo kuu la Lisbon, Ureno yaliyonogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Hii ilikuwa ni hija yake ya 42 ya Kitume Kimataifa na mwendelezo wa tema kuhusu dhamana na utume wa Bikira Maria katika maisha ya Kanisa. Itakumbukwa kwamba, maadhimisho haya yalizinduliwa rasmi tarehe 1 Agosti 2023 kwa Ibada ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa kwa mafuriko ya vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia. “Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa.” Lk 1:39-42. Hii ni sehemu ya Maandiko Matakatifu yaliyonogesha Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 9 Agosti 2023 kwa kujikita katika hija yake ya 42 ya Kitume nchini Ureno kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni. Katika Katekesi yake, Baba Mtakatifu amegusia kuhusu mkutano wake na viongozi wa serikali, vyama vya kiraia na wanadiplomasia; safari yake kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima kwa ajili ya kuombea amani duniani pamoja na Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana kwa kumwangalia Bikira Maria kama kielelezo cha huduma, imani na matumaini. Siku za vijana ulimwenguni ni chemchemi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa na kwamba, Kristo Yesu amepandikiza mbegu ya matumaini miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, tayari kupyaisha maisha na ulimwengu katika ujumla wake na kwamba, kuna uwezekano wa ujenzi wa mshikamano wa udugu wa kibinadamu, bila chuki, hofu wala uwepo wa silaha. Huu umekuwa ni ujumbe mkubwa kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa.

Bikira Maria ni kielelezo cha imani na fadhila
Bikira Maria ni kielelezo cha imani na fadhila

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni imekuwa ni fursa ya kukutana na viongozi wa Serikali sanjari na Kanisa mahalia pamoja na kutembelea Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima. Maadhimisho haya yameonekana kuwa ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu baada ya athari kubwa za maambukizi ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19. Fumbo la Utatu Mtakatifu limewezesha tena kuzielekeza nyoyo za vijana wengi katika njia ya Injili, chemchemi ya matumaini kwa familia kubwa ya Mungu. Maambukizi makubwa ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 yamesababisha madhara makubwa katika medani mbalimbali za kijamii, lakini zaidi ni utengano wa kijamii ambao vijana wameonja athari zake zaidi. Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni yamekuwa ni mwanzo mpya wa hija ya matumaini miongoni mwa vijana wa kizazi kipya kwa jina la Kristo Yesu. Maadhimisho haya yamefanyika Jimbo kuu la Lisbon nchini Ureno, nchi yenye wavumbuzi wengi, kielelezo cha matamanio ya binadamu ya kwenda mbali zaidi ili kuvumbua nchi mpya, vinginevyo vijana watajikatia tamaa na kujifungia katika ubinafsi wao. Baba Mtakatifu anasema, Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni kwa mwaka 2023 yamenogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Bikira Maria katika ujana wake alikirimiwa zawadi ya ujasiri hata katika udogo na unyenyekevu wake; akaondoka kwa haraka kwenda kutoa huduma pamoja na kushiriki mpango wa ukombozi. Hata katika Millenia ya tatu ya Ukristo, Bikira Maria bado anaendelea kuwaongoza vijana katika hija ya maisha ya kumfuasa Kristo Yesu. Tarehe 13 Mei 1917 Bikira Maria aliwatokea watoto watatu wa Fatima Francis, Yacinta Marto na Lucia dos Santos na kujitambulisha kuwa ni Bikira Maria wa Rozari Takatifu, kwa kuwakabidhi watoto hawa ujumbe wa matumaini kwa binadamu wote, akiwataka wajizatiti katika kupambana na ubaya, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Maadhimisho haya yamewawezesha vijana kukutana na Kristo Yesu
Maadhimisho haya yamewawezesha vijana kukutana na Kristo Yesu

Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unaweza kufupishwa kwa maneno makuu matatu: Sala, Toba na Wongofu wa ndani! Sala ni majadiliano ya kina kati ya mwamini na Muumba wake; majadiliano yanayomwongoza mwamini kuelekea katika maisha ya uzima wa milele. Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kuwa na mwelekeo mpya katika maisha yao. Bikira Maria wa Fatima anawaalika waamini kuchuchumilia utakatifu na kuendelea kusali kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani; kwa kujiweka wakfu kwa Moyo wake usiokuwa na doa, mkazo wa ujumbe huu zaidi ni imani na matumaini kwa Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, akiwa ameungana na vijana amemwomba Mwenyezi Mungu apende kuganga na kuponya madonda makuu yanayousonga moyo wa binadamu katika ulimwengu mamboleo: kiburi, uongo, uadui pamoja na vita. Baba Mtakatifu amerudia tena kuliweka wakfu Bara la Ulaya na Ulimwengu katika ujumla wake chini ya Moyo Safi wa Bikira Maria. Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni imekuwa ni fursa kwa vijana kufanya mang’amuzi ya ujenzi wa urafiki na udugu wa kibinadamu katika parokia na kwenye familia sehemu mbalimbali za Ureno na hatimaye, wakashiriki katika sherehe za ufunguzi wa Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, Mkesha na hatimaye, Ibada ya Misa Takatifu. Huu ni mkutano kati ya vijana wa kizazi kipya na Kristo Yesu kwa njia ya Kanisa, tukio ambalo linawawezesha vijana kukua na kukomaa katika imani na furaha kwa kila mmoja kugundua wito wake, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu na kwamba, Mwenyezi Mungu ni Baba anawapenda sana watoto wake.

Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, moto wa kuotea mbali
Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, moto wa kuotea mbali

Hija hii imemwezesha baba Mtakatifu Francisko kukutana na kuzungumza na bahari ya vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Baba Mtakatifu anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kufanikisha tukio hili na ametoa shukrani zake za dhati kwa wadau mbalimbali waliohusika katika maandalizi na hatimaye, maaadhimisho yenyewe, tayari kutupa nyavu nyingine kwa ari na moyo wa kitume. Mbegu ya Habari Njema imepandwa nyoyoni mwa vijana wa kizazi kipya nchini Ureno, chachu ya mabadiliko yanayosimikwa katika matumaini yanayobubujika kutoka kwa vijana wanaokita maisha yao katika Injili, vijana waliokutana na Kristo Yesu na wanamfuta, kwa sababu Kristo Yesu ndiye peke yake anayeweza kuupyaisha ulimwengu, kwa kupyaisha moyo wa mwanadamu. Wakati ambapo vita inaendelea kupiganwa sehemu mbalimbali za dunia, Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni yameonesha kwamba, kuna uwezekano wa kujenga ulimwengu unaosimikwa katika umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kuishi bega kwa bega, bila chukio na uhasama; hofu na woga, bila ya kuzama katika tabia ya kujifungia katika uchoyo na ubinafsi wala bila mtutu wa bunduki kurindima mitaani. Lakini, jambo la kujiuliza Je, ujumbe huu wa vijana utasikika na kupokelewa katika mwelekeo chanya na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa? Mwishoni mwa Katekesi yake, Baba Mtakatifu amewashukuru watu wa Mungu nchini Ureno kwa kufanikisha Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni. Amewaweka wote hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria.

Muhtasari siku ya Vijana 2023
09 August 2023, 15:26

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >