Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kurejea mjini Vatican Dominika tarehe 6 Agosti 2023 alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kurejea mjini Vatican Dominika tarehe 6 Agosti 2023 alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni: Mahojiano na Waandishi wa Habari

Papa Francisko alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake aliweza kujibu maswali matano kwa ufasaha kuhusu: Sala kwa ajili ya kuombea amani katika hali ya ukimya! Kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo nchini Ureno, kuhusu afya yake na kwamba, kipaumbele cha hija zake za kitume ni kutembelea nchi ndogo ndogo kwanza na kwamba, ndani ya Kanisa kuna nafasi kwa kila mwamini na Siku ya Vijana Duniani

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 6 Agosti 2023 Sikukuu ya Kung’ara Bwana amehitimisha Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni Jimbo kuu la Lisbon, Ureno yaliyonogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Hii ilikuwa ni hija yake ya 42 ya Kitume Kimataifa na mwendelezo wa tema kuhusu dhamana na utume wa Bikira Maria katika maisha ya Kanisa. Baada ya kuhitimisha hija yake ya kitume Kimataifa, Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kurejea mjini Vatican alipata nafasi ya “kuchonga” na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake aliweza kujibu maswali matano kwa ufasaha kuhusu: Sala kwa ajili ya kuombea amani katika hali ya ukimya! Kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo nchini Ureno, kuhusu afya yake inaendelea kuimarika na kwamba, kipaumbele cha hija zake za kitume ni kutembelea nchi ndogo ndogo kwanza na kwamba, ndani ya Kanisa kuna nafasi kwa kila mwamini; maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni na hatimaye ni kuhusu upweke hasi unaowatumbukiza watu wengi kwenye ugonjwa wa sonona au msongo wa mawazo. Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 5 Agosti 2023 alikwenda kutembelea na kusali kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, nchini Ureno pamoja na kuongoza Ibada ya Rozari Takatifu kwa vijana wagonjwa. Baba Mtakatifu anasema, alisali kuombea amani katika hali ya ukimya, huu ni mwaliko wa kuendelea kusali bila ya kuchoka kwa ajili ya kuombea amani duniani. Anakaza kusema kwamba, amesali na kuombea amani katika hali ya ukimya bila kutaka makuu. Kuhusu nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa.

Papa akiwa Fatima ameombea amani katika ukiimya
Papa akiwa Fatima ameombea amani katika ukiimya

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni janga kubwa la kijamii na kwamba, takwimu zinaonesha kwamba, asilimia 40 ya kesi za nyanyaso za kijinsia zinafanyika katika mazingira ya kifamilia. Taarifa kutoka kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbalimbali za dunia inaonesha kwamba, hii ni kashfa kubwa na kwamba, viongozi wa Kanisa hawana budi kuwajibika barabara na kwamba, nyanyaso za kijinsia kwa sasa ndani ya Kanisa Katoliki hazivumiliki. Kesi za nyanyaso za kijiniia zinaendelea kushughulikiwa vyema na Kanisa Katoliki nchini Ureno kwa ufanisi mkubwa. Huu ni mwaliko kwa waandishi wa habari kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia katika jamii. Baba Mtakatifu ametoa angalisho kwa baadhi ya watu kupenda na kuwatumia watoto wadogo kwa mafao binafsi.

Kashfa ya nyanyaso za kijinsia haivumiliki tena
Kashfa ya nyanyaso za kijinsia haivumiliki tena

Baba Mtakatifu anasema, anapopata nafasi anapenda kuzungumza na wahanga wa nyanyaso za kijinsia ili kufahamu ukubwa wa tatizo. Nyanyaso mbalimbali zinaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu, kuna watoto wanaonyanyaswa kwa kufanyishwa kazi ngumu, kuna wanawake na wasichana wanaonyanyaswa kwa kutumbukizwa katika mifumo ya utumwa mamboleo. Kumbe, kuna mifumo mbalimbali ya nyanyaso dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu, inayopaswa kupatiwa ufumbuzi wa kutosha kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Baba Mtakatifu amezungumzia afya yake kwamba, inaendelea kuimarika kila kukicha na kwamba, wakati mwingine anapunguza au kuongeza mahubiri yake kwa kusoma alama za nyakati, ili kufafanua pamoja na kuhakikisha kwamba, ujumbe uliokusudiwa unawafikia walengwa. Baba Mtakatifu anasema kwenye Waraka wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani: “Furaha ya Injili” amegusia kipengele cha mahubiri ambacho ni kipimo cha kutambua ni kwa kiasi gani mchungaji yupo karibu na watu wake na ni kwa kiwango gani anaweza kuwasiliana nao; mahubiri katika muktadha wa liturujia, maongezi ya Mama; maneno yanayoiwasha miyo ya waamini; Jinsi ya kuandaa mahubiri kwa kuheshimu ukweli sanjari na kunafsisha maneno. Rej. Evangelii gaudium namba 135-149. Kimsingi mahubiri yasizidi dakika nane. Hapa kuna haja ya Kanisa kufanya toba na wongofu wa ndani kwa wachungaji kuhakikisha kwamba, wanaandaa mahubiri mafupi, yanayoeleweka na kupenya katika akili na nyoyo za watu. 

Mahubiri yawe ni mafupi yanayogusia mambo msingi
Mahubiri yawe ni mafupi yanayogusia mambo msingi

Baba Mtakatifu tarehe 22 hadi 23 Septemba 2023 atafanya Hija ya Kitume ya 44 Kimataifa huko Jimbo kuu la Marseilles, Ufaransa ili kufunga mkutano wa Maaskofu na vijana utakaofunguliwa rasmi tarehe 17 hadi 24 Septemba 2023. Kipaumbele cha kwanza ni wakimbizi na wahamiaji. Bahari ya Mediterrania imegeuka kuwa ni kaburi la maisha na matumaini ya watu wanaokimbia vita, ghasia, umaskini, dhuluma, nyanyaso pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Hawa ni watu wanaokufa maji wakiwa njiani kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Pengine anasema Baba Mtakatifu, hii ni kazi ya wafanyabiashara ya binadamu na viungo vyake. Wakimbizi na wahamiaji wanatekwa, wananyanyaswa na kudhulumiwa haki zao msingi. Baba Mtakatifu anawaalika waandishi wa habari kujisomea kitabu kijulikanacho kama “Hermanito, Fratellino au Ndugu Mdogo.” Hiki ni kitabu kinachosimulia mchakato wa wakimbizi na wahamiaji kabla ya kupanda mashua kutafuta hifadhi na maisha bora Barani Ulaya. Maaskofu wanataka kufanya upembuzi yakinifu kuhusu tatizo la wakimbizi na wahamiaji Kaskazini mwa Afrika. Rais Emmanuel Jean-Michel Frédéric Macron wa Ufaransa ameonesha nia ya kushiriki katika mkutano huu. Kumbe, Baba Mtakatifu anasema, kipaumbele chake kwa sasa ni kutembelea nchini ndogo, kama alivyoanza Albania!

Kipaumbele chake katika maisha ni wakimbizi na wahamiaji
Kipaumbele chake katika maisha ni wakimbizi na wahamiaji

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna nafasi kwa waamini wote ndani ya Kanisa. Maisha na utume huu unaratibiwa kwa Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo. Kanisa liko wazi hata kwa wale ambao wana vizuizi vya kupokea Sakramenti za Kanisa. Kanisani ni mahali ambapo waamini wanafika kusali na kumwomba Mwenyezi Mungu. Kila mtu anajitahidi kuhakikisha kwamba, maisha yanasonga mbele hata kwa watu wenye maelekeo ya mapenzi ya jinsia moja. Kanisa linaonesha uvumilivu katika kuadhimisha mafumbo yake. Kanisa ni Mama na Mwalimu anayewapokea watoto wake wote bila ubaguzi. Kila mtu atekeleze dhamana na wajibu wake bila kutaka kujimwambafai. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni kuanzia kule Rio de Janeiro, Cracovia, Panama na sasa Lisbon imevunja rekodi kwa kuwa na washiriki wengi zaidi ya milioni moja na nusu. Maandalizi yamefanyika kwa umakini mkubwa na kwamba, “kwa hakika ujana ni maji ya kuotea mbali.”  Jambo la msingi na changamoto kubwa katika maisha na utume wa vijana ni kutambua jinsi ya kuwasindikiza, ili wasijikute wanang’oka kutoka katika mizizi yao. Vijana wajengewe utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili waweze kuelekezwa kuwa ni wachaji na wachamungu. Vijana waruhusiwe kuanguka na hapo watajifunza kusimama na kutembea tena, huu ndio mtindo wa maisha. Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, daima yuko tayari kuwapokea wale wanaotubu na kumwongokea. Kwa hakika, Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni Jimbo kuu la Lisbon, Ureno yametia fola!

Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni yamefana sana
Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni yamefana sana

Upweke hasi ni hatari sana katika maisha ya mwanadamu kwani unaweza kumtumbukiza mtu katika ugonjwa wa sonona au msongo wa mawazo kama unavyofahamika na wengi. Sonona ni ugonjwa wa kawaida wa akili unaohusisha hali endelevu ya huzuni au kukosa shauku au raha inayoambatana na dalili zifuatazo: hali ya kukosa usingizi na hata hamu ya chakula, hisia za mtu kujiona kuwa hafai, uchovu wa kupindukia, umakini hafifu na ugumu katika kufanya maamuzi. Dalili nyingine ni ukosefu wa utulivu wa mwili, mtu kuongea sana pamoja na kukosa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Sababu zinazoweza kuchangia sonona ni kama hizi zifuatazo: Nyanyaso za kijinsia na utumiaji haramu wa dawa za kulevya. Migogoro ya kifamilia, kijamii na kimahusiano husababisha kwa baadhi ya watu kutumbukia katika ugonjwa wa sonona, ambapo mtu hujiona hana thamani tena baada ya kutengwa na jamii kwa muda mrefu. Kifo au hasara za kikazi, wakati mwingine mtu hujikuta amepata tatizo hili baada ya kupoteza mtu muhimu kwake na jamii kwa ujumla au endapo mtu akapata hasara kubwa kiasi cha kufilisika mali yake, basi mtu huyu hunyong'onyea na kudhohofika afya yake taratibu, asijue wapi pa kuanzia na hatima yake huona jamii yote kwake kuwa ni mbaya na imemtenga kiasi cha kujiona si mali kitu! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, leo hii tatizo la vijana kujiua ni kubwa na mara nyingi hizi si taarifa zinazopenyezwa kwenye vyombo vya mawasiliano ya jamii. Kuna vijana wengi wanaojaribu kutaka kujinyonga kwa sababu ya sonona. Sababu kubwa ni changamoto za masomo vyuoni, mahusiano pamoja na ukosefu wa fursa za ajira kiasi cha kujisikia kuwa si mali kitu katika jamii. Hili ni tatizo kubwa linalopaswa kuvaliwa njuga. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kwa kazi nzuri wanayo ifanya katika tasnia ya mawasiliano ya jamii. Baba Mtakatifu Jumatatu asubuhi, tarehe 7 Agosti 2023 amekwenda moja kwa moja hadi kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu Jimbo kuuu la Roma, kutoa heshima zake kwa Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani” baada ya kuhitimisha maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni, Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno.

Papa Waandishi wa Habari
07 August 2023, 16:23