Maadhimisho ya Siku ya Vijana Ulimwenguni: Hotuba Kwa Vijana wa Kujitolea
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 6 Agosti 2023 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kilele cha Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno, iliyonogeshwa na kauli mbiu “Maria aliondoka akaenda kwa haraka.” Lk. 1:39. Hii ni hija ya 42 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Kimataifa na ni mwendelezo wa tema kuhusu dhamana na utume wa Bikira Maria katika maisha ya Kanisa. Baba Mtakatifu jioni amepata fursa ya kukutana na kuzungumza na watu wa kujitolea 25, 000 kutoka katika Mataifa 150, wenye umri kati ya miaka 28. Hawa ndio waliosadaka maisha yao ili kuhakikisha kwamba, Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni yanakwenda kama yalivyopangwa. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amewapongeza watu wa kujitolea katika huduma inayojenga urafiki wa kijamii kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Baba Mtakatifu ametoa shukrani zake za dhati kwa Kristo Yesu anayetembea bega kwa bega na vijana wa kizazi kipya kwa njia ya huduma. Vijana washikamane na kutegemezana ili kuvuka mawimbi ya maisha. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru viongozi wa Kanisa, Serikali pamoja na vijana wa kujitolea, waliosadaka maisha yao kiasi cha kuwawezesha vijana wote kuimba wimbo wa sifa na shukrani kwa Kristo Yesu anayetembea na kuambatana pamoja nao!
Hawa ni vijana waliojisadaka kwa ajili ya huduma, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria aliyeondoka akaenda kwa haraka, ili kumshirikisha binamu yake, ile furaha ya huduma. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Zakayo Mtoza ushuru aliyeshuka haraka mtini ili kumhudumia Kristo Yesu aliyekuwa ameamua kushinda nyumbani kwake. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa wale wanawake wanaosimuliwa katika Injili, Siku ile ya kwanza ya Juma, walipoondoka kwenda kaburini, lakini wakamkuta Kristo Yesu amefufuka, wakarejea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Ufufuko. Baba Mtakatifu anakaza kusema, kwa mtu anayependa, yuko tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma; daima yuko tayari kutoka kwa haraka. Hiki ni kipindi ambacho wameguswa na kutikiswa na uchovu pamoja na wingi wa kazi, lakini daima wameendelea kubaki wakiwa na macho angavu na kuhakikisha kwamba, wanafanikisha Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni. Wamejisadaka kwa ajili ya huduma kwa Kristo Yesu kupitia vijana walioshiriki katika maadhimisho haya. Amewashukuru vijana waliotoa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kwa kukutana na Kristo Yesu katika sala, Ibada ya Misa Mitakatifu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Vijana wa kujitolea waliweza kushinda uchovu wao kwa njia ya huduma kwa vijana wenzao. Vijana hawa wametembea, wakatoa huduma na kusali. Kwa njia hii vijana wa kujitolea wamejifunza kutengeneza vyumba vyao vya kulala. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza vijana wa kujitolea kwa sababu wamepata nafasi ya kukutana na Kristo Yesu anayetembea pamoja nao, akiwahimiza kuwa ni wachamungu na watu wenye moyo wa Ibada. Hii imekuwa ni fursa ya kukutana na Kristo Yesu pamoja na vijana wenzao. Kukutana na Kristo Yesu ni tendo la faragha linalonogeshwa na huduma kwa vijana wengine, huduma inayowawezesha tena kukutana na Kristo Yesu.
Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu amewapongeza vijana wa kujitolea kwa kupambana na mawimbi ya vijana waliokuwa wanashiriki katika Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni. Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na kwa moyo wa upendo na ukarimu, wameweza kukabiliana na mawimbi ya vijana wenzao, changamoto na mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kuendeleza mwaliko huu wa kupambana na mawimbi ya Bahari kwa njia ya upendo. Hii ndiyo dhamana ambayo angependa kuwaachia vijana wa kujitolea kwamba, huduma hii iwe ni kati ya mema mengi ambayo wanapaswa kutenda, daima wakijitahidi kumsogelea Mungu. Kwa upande wake, Kardinali Manuel José Macário do Nascimento Clemente, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lisbon, Ureno katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko azungumze na vijana wa kujitolea, amesikika akisema kwamba, kwa hakika maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Ulimwenguni ni tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wa Mungu. Vijana wamepambana na kukabiliana na changamoto za maisha kwa ajili ya ustawi na majitoleo kwa watu wa Mungu. Kwa hakika Kanisa linawategemea vijana wa kizazi kipya ili kulipyaisha na kwamba, tangu kuasisiwa kwake, Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa, Baba Mtakatifu amekuwa ni kiini chake na kwa hakika Maadhimisho haya ni ya Papa Francisko. Upendo na ukarimu wa watu wa kujitolea umewezesha Maadhimisho ya Siku ya 37 ya Vijana Kimataifa kupata ufanisi mkubwa.