Maombi ya Papa kwa ajili ya Cameroon na salamu kwa vijana wa WYD
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Akiwa katika dirisha la Jumba la Kitume, mara baada ya sala ya Malaika Dominika tarehe 13 Agosti 2023, Baba Mtakatifu ameomba sala kwa ajili ya amani nchini Cameroon ambapo tarehe 14 Agosti ni mkesha wa sikukuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni, watafanya hija katika jimbo la Bafoussam ili kuombea amani nchini humo ambayo bado inakumbwa na ghasia na vita. Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu amesema: “Kesho, katika mkesha wa sikukuu ya Mama Yetu Mpalizwa Mbinguni, ifafanyika hija ya kuomba amani nchini, ambayo bado inakumbwa na ghasia na vita, huko Bafoussam, Cameroon. Tuungane katika sala ya pamoja na ndugu zetu wa Cameroon ili kwa maombezi ya Bikira, Mungu aweze kudumisha tumaini la watu ambao wamekuwa wakiteseka kwa miaka mingi, na kufungua njia za mazungumzo ili kufikia maelewano na amani.”
Vita vya wenyewe kwa wenyewe 2017
Nchini Cameroon, vita vya wenyewe kwa wenyewe vimekuwa vikiendelea tangu 2017, ambavyo vilianza kutokana na migogoro ya kijamii na kiutamaduni. Pia inajulikana kama mgogoro au mzozo huo ulitokana na uasi uliofanywa na watu wanaozungumza Kiingereza wanaotaka kujitenga dhidi ya vikosi vya kawaida vya jeshi. Katika kukabiliana na hali hiyo, serikali ilituma jeshi katika mikoa inayozungumza Kiingereza ili kukabiliana na wapinzani. Katika miezi sita ya kwanza , ya mwaka 2023, vurugu na ukandamizaji vimeongezeka. Huku nyuma, misukosuko ya kisiasa iliyohusishwa na mrithi wa Rais Paul Biya mwenye umri wa miaka 90, ambaye ameongoza tangu 1982.
Kuombea Ukraine
Katika muktadha wa mgogoro huo wazo la Baba Mtakatifu Francisko kama kawaidia yake limegeukia kwa mara nyingine tena “kwa nchi ya Ukraine inayoteswa sana na vita”.
Bendera za vijana wa WYD
Papa Francisko akitazama katika uwanja uliojaa bendera nyingi kutoka sehemu mbali mbali za mataifa, amesema: “Sasa ninatoa salamu zangu kwenu nyote, Warumi na mahujaji kutoka nchi mbalimbali. Ninasalimia hasa baadhi ya vikundi vilivyoshiriki katika Siku ya Vijana huko Lisbon… Ni wengi! Ninaona bendera… Poland, Mexico, Argentina, Italia, Salvador, nyingi! Mapadre na vijana wa El Salvador ambao wana nguvu sana; wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Ibero-Amerika cha Puebla, Mexico; na vijana wa Taiwan. Tembeeni vizuri! Na ninawatakia Dominika njema. Tafadhali msisahau kuniombea. Mlo mwema, mchana mwema na kwaheri ya kuonana!