Tafuta

Mkutano unanogeshwa na kauli mbiu “Kwa Kutembea Pamoja na Kristo Tunaishi Udugu wa Amazonia.” Mkutano unanogeshwa na kauli mbiu “Kwa Kutembea Pamoja na Kristo Tunaishi Udugu wa Amazonia.”  

Mkutano wa Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia: Utunzaji Bora wa Mazingira Amazonia

Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia, kuanzia tarehe 8 hadi 11 Agosti 2023 linaadhimisha mkutano ambao pamoja na mambo mengine, ulipania kuweka mbinu mkakati wa kuhifadhi msitu wa Amazonia ifikapo mwaka 2030. Mkutano unanogeshwa na kauli mbiu “Kwa Kutembea Pamoja na Kristo Tunaishi Udugu wa Amazonia.” Huu ni mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unaojikita katika kujadiliana, kusikilizana na kufanya mang'amuzi na utekelezaji kwa pamoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6 - 27 Oktoba, 2019 yaliongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ikolojia fungamani.” Mababa wa Sinodi walipitia, wakajadili na hatimaye wakapigia kura vipengele vyote na kupitisha Hati ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa Mwaka 2019. Hati hii ikaongozwa na kauli mbiu “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ikolojia fungamani.” Baada ya kusali, kutafakari na kusikiliza kwa makini, sasa ni wakati wa kujikita katika wongofu wa kiikolojia, shughuli za kichungaji na kitamaduni. Kanisa liliangalia pia njia mpya za wongofu Ukanda wa Amazonia pamoja na kutoa hitimisho la Hati ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume “Querida Amazonia”, yaani “Wapendwa watu wa Ukanda wa Amazonia” uliochapishwa tarehe 12 Februari 2020 anagusia kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa ndoto ya jamii, ndoto ya kitamaduni, ndoto ya kiikolojia, ndoto ya Kikanisa na hatimaye, anamwonesha Bikira Maria kuwa ni Mama wa Ukanda wa Amazonia. Itakumbukwa kwamba, Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, walipendekeza kuundwa kwa Baraza litakalosaidia kumwilisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa Ukanda wa Amazonia, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia, mkutano kuhusu Amazonia 2023
Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia, mkutano kuhusu Amazonia 2023

Ni katika muktadha huu, kuanzia tarehe 26 hadi 29 Juni 2020, wajumbe kutoka kwenye “Mtandao wa Kanisa Amerika ya Kusini”, (Pan-Amazon Ecclesial Network of the Latin American Church, REPAM” wameunda Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia, “Conferência Eclesial da Amazônia” yaani: CEAMA wakati Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani. Lengo ni kukazia dhana ya unabii na utume wa kimisionari ambao Mama Kanisa hana budi kuuendeleza hadi miisho ya dunia. Hili ni tukio la matumaini ya Mababa wa Sinodi wakiwa wameunganika na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amekuwa nao bega kwa bega katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia, “Conferência Eclesial da Amazônia” yaani: CEAMA” kuanzia tarehe 8 hadi 11 Agosti 2023 linaadhimisha mkutano ambao pamoja na mambo mengine, ulipania kuweka mbinu mkakati wa kuhifadhi msitu wa Amazonia ifikapo mwaka 2030. Mkutano unanogeshwa na kauli mbiu “Kwa Kutembea Pamoja na Kristo Tunaishi Udugu wa Amazonia.” Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 9 Agosti 2023 aliwatumia salam wajumbe wa mkutano huo unaofanyika huko Belèm do Parà nchini Brazil. Amewahakikishia uwepo wake kwa njia ya sala na kwamba, anatumaini kwamba, watapyaisha sera na mikakati ya ulinzi na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rais Luiz Inácio Lula da Silva wa Brazil amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono sera na mikakati ya utunzaji bora wa Misitu ya Amazonia.

Tamko la Belèm la mwaka 2023
Tamko la Belèm la mwaka 2023

Wajumbe, katika “Tamko la Belèm la Mwaka 2023” wanataka watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira. Kusitisha uvunaji na unyonyaji wa mali asili kwa sababu nchi zinazoendelea zimeshindwa kugharimia miradi ya maendeleo kiuchumi iliyokuwa inagharimu kiasi cha dola bilioni 100. Wajumbe wanasema, umaskini ni kikwazo kikubwa cha ustawi na maendeleo ya wengi. Uchimbaji wa madini na uvunaji wa rasilimali za Ukanda wa Amazonia unafanywa kwa kasi ya kutisha. Wajumbe wamekubaliana kukutana tena kunako mwaka 2025 nchini Colombia ili kujitahidi kuweka mbinu mkakati wa utunzaji wa msitu wa Ukanda wa Amazonia mintarafu Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” na ule wa Waraka wa "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” sehemu muhimu sana ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, kama sehemu ya mchango wake katika mkutano huu, amekazia umuhimu wa Kanisa kupandikiza mbegu ya matumaini inayofumbatwa katika mchakato wa kusikiliza kwa makini pamoja na kuwaongoza watu wa Mungu ili waweze kuwajibika barabara, tayari kukabiliana na changamoto mamboleo; kwa kutambua Uso wa Mungu miongoni mwa watu mahalia wa Amazonia.

Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote
Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote

Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia, “Conferência Eclesial da Amazônia” yaani: CEAMA” ni matunda ya mchakato wa maadhimisho ya Sinodi Ukanda wa Amazonia, changamoto kwa Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, anatangaza na kushuhudia Ujumbe wa Matumaini kwa watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia, kwa kuinua utu, heshima na haki zao msingi; tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili sanjari na ushiriki mkamilifu wa waamini walei. Baraza la Makanisa Ukanda wa Amazonia, CEAMA linao wajibu wa kuragibisha umuhimu wa Ukanda wa Amazonia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu katika ujumla wao. Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji haina budi kutoa kipaumbele cha kwanza katika mapambano dhidi ya umaskini kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kanisa Ukanda wa Amazonia halina budi kuendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kujikita katika malezi na majiundo ya Mapadre wake na kwamba, CEAMA inapaswa kuwa ni chombo cha maendeleo  ya watu wa Mungu, daima kwa kusoma alama za nyakati.

Papa Amazonia
11 August 2023, 16:30