Papa Francisko:Ukiwa na Yesu nguvu za ubaya zinabadilishwa mara moja!

Katika tafakari ya Papa kabla ya sala ya Malaika wa Bwana amejikita juu ya Injili ya Yesu anayetembea Bahari ya Galilaya huku akikutana na wanafunzi wake ambao walishikwa hofu.Papa ametoa ombi la kumkaribishwa Kristo wakati wa hofu na kuzama katika maovu,kwa sababu ni Yeye anayekanyaga mauti,dhambi na shetani kwa ajili yetu.

Na Angella Rwezaula,- Vatican.

Leo Injili inasimulia kwa namna ya pekee miujiza ya Yesu: Yeye  katika usiku alitembea juu ya maji katika ziwa la Galilaya na kukutana na mitume ambao walikuwa wanasafiri kwa  mtumbwi (Mt 14,22-33).  Swali: Kwa nini Yestu alifanya  hivyo? Kama Tamasha? Hapana” Lakini kwa nini?  Labda kwa sababu ya ulazima wa dharura na usiotarajiwa, ili kuwasaidia mitume ambao walikuwa wanahangaika na kuzuiwa na upepo mkali? Hapana, na kwa sababu gani wakati Yeye alikuwa amepanga yote na kuwalazimisha waondoke jioni hiyo kama isemavyo Injili kwamba ‘aliwalazimisha’ (Mt 14, 22). Labda ilikuwa ni kuwaonesha wao ukuu na nguvu? Lakini hii siyo rahisi hivyo.  Kwa hiyo ni kwa nini alifanya hivyo? Kwa nini alitaka kutembea juu ya maji? Ndivyo Baba Mtakatifu Francisko alianza tafakari yake, Dominika tarehe 13 Agosti 2023 akiwageukia waamini na mahujaji wote waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu akiendelea amesema kuwa “Nyuma ya kutembea juu ya maji kuna ujumbe,  ambao siyo wa moja kwa moja kuupokea sisi na kuutambua. Na wakati huo huo kiukweli maji yenye kina kirefu hasa  ya mbali  katika enzi zile yalikuwa yanafahamika kama makao ya nguvu mbaya ambazo zisingeweza kutawaliwa na mtu, nguvu mbaya: hasa kama maji yalikuwa yamechafuka kwa dhoruba na kuzimu ilikuwa ni shara ya machafuko hasa na kubainisha giza kuu la kuzimu. Kwa hiyo sasa mitume walijikuta katikati ya ziwa na ndani mwao kuna woga wa kuzama, wa kumezwa na mabaya. Na hapa ndipo anafika Yesu ambaye alikuwa akitembea juu ya maji, yaani juu ya nguvu zile za ubaya na kuwambia: “Jipeni moyo; ni mimi; msiogope…” (Mt 14,27).

Baba Mtakatifu ameongeza: "Ndiyo hayo yote ambayo ujumbe wa Yesu unatupatia na tazama maana ya ishara: “Nguvu za ubaya ambazo zinatuogopesha na tunashindwa kuzitawala, lakini  pamoja na Yesu zinabadilishwa ukubwa mara moja. Yeye, akitembea juu ya maji, anataka kutuambia: Usiogope, nitaweka adui zako chini ya miguu yako”, Huu ni ujumbe mzuri, wa nitaweka adui zako chini ya miguu yako: sio watu!, sio maadui! , lakini kifo, dhambi, shetani na  hawa ni maadui wa watu, adui zetu. Na Yesu anawakanyaga maadui hawa kwa ajili yetu.

Leo hii Kristo anarudia kwa kila mmoja wetu akisema “Jipeni moyo ni mimi, msiogope! Jipeni moyo kwa sababu ni mimi, na kwa sababu wewe hauko peke yako katika maji yaliyochafuka ya maisha. Lakini  je ni kufanya nini wakati tunajikuta katika bahari iliyowazi na wakati inayumbishwa na pepo tofauti? Je ni nini la kufanya katika hofu, ambayo ni bahari wazi, wakati linaonekanagiza tu na tunahisi kupotea?  Baba Mtakatifu amesema ni lazima kufanya mambo mawili ambayo katika Injili Yesu anatufanya tuone na ambayo walifanya mitume.  Je wanafunzi wanafanya nini? Wanamwomba na kumkaribisha Yesu. Katika nyakati mbaya zaidi, na dhoruba ya giza zaidi, ni lazima kumwomba Yesu na kumkaribishe Yesu.

Akidadavua juu ya kuomba, Baba Mtakatifu amebainisha kwamba Wanafunzi waliomba Yesu. Petro alitembea kidogo juu ya maji kuelekea Yesu, lakini baada akaogopa na kuzama na ndipo akapiga yowe akisema ‘Bwana niokoe’, (Mat 14,30).  Walimwomba Yesu na kumwita Yesu. Sala hiyo ni nzuri, ambayo inaelezea uhakika kwamba Bwana anaweza kutuokoa, na ambaye Yeye anashida mabaya yetu na hofu zetu. Baba Mtakatifu aliwaalika waamini na wanahujaji kurudia pamoja “Bwana uniokoe” mara tatu. Na akiendelea amesema kuwa baadaye wanafunzi walimkaribisha lakini  awali ya yote walimwomba na baadaye wakamkaribisha  Yesu katika chombo chao. Maandishi yanaeleza kuwa: "Nao walipopanda chomboni, upepo ulikoma". Kwa hiyo Bwana anajua kuwa mtumbwi wa maisha, kama ulivyo mtumbwi wa Kanisa, umehatarishwa na pepo tofauti na kwamba bahari ambayo tunaogelea mara nyingi imechafuka. Ndiyo Bwana anajua", Papa amesisitiza.

Yeye hatuokoi na ugumu wa kusafiri na chombo  kinyume chake Injili inasisitiza kuwa aliwalazimisha wanafunzi wake kuondoka; na hivyo anatualika kukabiliana na matatizo, kwa sababu katika hayo yanageuka kuwa eneo la wokovu, fursa ya kukutana na Yeye. Yeye kiukweli, katika wakati wetu wa giza, anakuja kukutana nasi, anaomba kukaribishwa na kusikilizwa, kama siku ile  ya wakati wa usiku ule wa ziwa. Baba Mtakatifu kwa kuhitimisha ameomba tujiuliza maswali: je katika woga , katika matatizo ninakuwaje? Ninakwenda mbele peke yangu na nguvu zangu au ninamwomba Bwana kwa imani? Je imani yangu ikoje? Ninaamini kuwa Kristo ni mwenye nguvu dhidi ya mawimbi na pepo tofauti? Na zaidi je ninaogelea na Yeye? Ninamkaribisha, ninaweka nafasi katika mtumbwi wa maisha yangu na kamwe siko peke yangu, daima na Yesu;  ninaelekeza dira kwa Yeye ? Maria Mama wa Yesu, Nyota ya Bahari, atusaidie kutafuta njia katika vivuko vya giza ile nuru ya Yesu.

Tafakari ya Papa kwa Malaika wa Bwana 13 Agosti 2023
13 August 2023, 13:13