Rambirambi za Papa kwa kifo cha Kard.Majella Agnelo na shukrani zake
Vatican News.
Ni kwa masikitiko makubwa, ya Baba Mtakatifu Francisko kupokea taarifa za kifo cha Kardinali Gerardo Majella Agnelo wa Brazil, kilichotokea tarehe 26 Agosti 2023, akiwa na umri wa miaka 89, huko Londrina katika jimbo la Paranà nchini Brazil. Ndivyo inasomeka katika telegramu iliyoelekezwa kwa Kardinali Sergio Da Rocha, Askofu mkuu wa mji mkuu wa Mtakatifu Salvador de Bahia, nchini huo ambamo Papa anatoa rambirambi zake na ambamo anawahakikishia washiriki wote wanaoomboleza kifo chake maombi kwa Bwana “kwa ajili ya mapumziko ya milele ya kuhani anayeheshimika.”
Asante Bwana kwa miaka mingi ya huduma ya Kanisa
Katika telegramu hiyo Baba Mtakatifu anabainisha kwamba “Maombi yangu pia ni ya shukrani kwa Mungu kwa miaka mingi ya huduma yake ya kujitolea kwa Kanisa mama Takatifu, akiongozwa daima na bidii ya kitume, katika utume mbalimbali aliokabidhiwa kama Askofu wa Toledo, Askofu Mkuu wa Londrina, na Katibu wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti, na hatimaye, Askofu mkuu wa Brazil na rais wa Baraza la Maaskofu nchini humo”.
Baraka za Baba Mtakatifu Francisko
Baba Mtakatifu Francisko kwa njia hiyo anatumia Askofu Mkuu Da Rocha na wale wote wanaoungana katika sala kwa ajili ya pumziko la milele la marehemu Kardinali, baraka zake za kitume kama ahadi ya faraja na matumaini katika uzima wa milele.” Alizaliwa tarehe 19 Oktoba 1933 huko Juiz de Fora, katika Jimbo la Minas Gerais, Kardinali Majella Agnelo, alianza masomo yake ya falsafa katika seminari mnamo mwaka 1951, mwaka 1954 alijiunga na Kitivo cha Taalimungu cha Nossa Senhora da Assunção huko Mtakatifu Paulo, na kuhitimu miaka mitatu baadaye. Alipewa daraja la Upadre mnamo tarehe 19 Juni 1957 katika Kanisa kuu la Mtakatifu Paulo na kama msimamizi alishikilia nyadhifa nyingi. Mnamo Oktoba 1967 alianza masomo yake ya liturujia katika taasisi ya kiliturujia ya Kipapa ya Mtakatifu Anselmo, Roma, akipata udaktari tarehe 3 Desemba 1969. Wakati wa kukaa kwake katika mji mkuu, katika Chuo cha Kipapa cha Pio cha Brasil, alishiriki kila Juma katika kipindi cha Radio Vatican kwenye Idhaa ya Brazili kiitwacho “Liturujia na Maisha” na alikuwa mshiriki wa kichungaji katika parokia ya Mtakatifu Clemente Papa katika wilaya ya Montesacro.
Nyadhifa nyingine za utume wake
Mnamo 1970 alirudi katika nchi yake na kufundisha huko Mtakatifu Paulo. Mnamo tarehe 5 Mei 1978, Mtakatifu Paul VI alimteua kuwa askofu wa Toledo, katika jimbo la Paraná, na akapokea daraja la uaskofu tarehe 6 Agosti 1978. Tarehe 4 Oktoba 1982, Mtakatifu Yohane Paulo II alimteua kuwa Askofu mkuu wa jiji kuu la Londrina. Alihusika katika liturujia huko Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Amerika Kusini (CELAM), ambapo alikuwa makamu rais kuanzia Mei 1999 hadi Mei 2003. Mnamo mwaka 1983 alianzisha uchungaji wa watoto huko Florestópolis, ambapo baadaye ilienea katika majimbo yote ya Brazil na katika baadhi ya majimbo ya nchi za Amerika Kusini. Tarehe 16 Septemba 1991 Papa Yohane Paulo II alimteua kuwa katibu wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa na kunako mwaka 1995 Baba Mtakatifu alimwita kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Jubilei ya Mwaka 2000.
Tarehe 13 Januari 1999 aliteuliwa kuwa Askofu mkuu wa Mtakatifu Salvador ya Bahia. Aliundwa kuwa Kardinali na Mtakatifu Yohane Paulo II mnamo tarehe 21 Februari 2001. Kuanzia Mei 2003 hadi Mei 2007 alikuwa rais wa Baraza la Maaskofu Brazili, na mwisho wa mamlaka yake pia alikuwa rais wa Mkutano Mkuu wa V wa Amerika ya Kusini na Maaskofu wa Caribbean. Katika barua iliyothibitishwa mnamo Machi 2020, inaarifu tovuti ya Jimbo kuu la Londrina kuwa Kardinali alikuwa ameelezea hamu ya kuzikwa katika jiji la Londrina. Kwa hivyo, Jimbo kuu ya Londrina na Askofu wake mkuu, Geremias Steinmetz, wanakubali matakwa ya Kardinali, ambaye atazikwa kwenye kaburi la Kanisa kuu la jiji kuu la Londrina. Kufuatia kifo cha Kardinali Majella Agnelo, Baraza la Makardinali kwa sasa linaundwa na makadinali 221, kati yao 120 ni wapiga kura na 101 sio wapiga kura.