Ujumbe wa Papa kwa wafanyakazi wa kikristo:kazi ni msingi wa hadhi ya binadamu
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Katika fursa ya Mkutano Mkuu 14 wa Harakati ya Hoac ya Wafanyakazi wa Chama cha Matendo ya Kikristo nchini Hispania uliozinduliwa, katika mji wa Segovia tarehe 12 Agosti na utahitimishwa tarehe 15 Agosti 2023, Baba Mtakatifu Francisko ametuma Ujumbe wake. Katika ujumbe huo, Baba Mtakatifu anaonesha furaha kubwa anapozungumza nao wote katika muktadha wa Mkutano Mkuu wao ambao unaongozwa na mada: “Kujenga madaraja, kubomoa kuta. Kanisa katika ulimwengu wa kazi hufuma vifungo vya udugu”. Kwa njia hiyo anatoa shukrani zake za kina kwa ajili ya kujitolea na kujitoa kwao kusalia kuwa Kanisa linalotembea katika ulimwengu wa kazi. Baba Mtakatifu akitazama Waraka wake wa kitumea anasema kwamba, “Katika Evangelii Gaudium nilisisitiza umuhimu wa kazi kama sehemu muhimu ya maisha na utu wa binadamu. Sio tu shughuli yenye tija, bali ni njia ambayo kwayo tunashirikiana na Mungu katika kazi ya uumbaji na kujitimiza sisi wenyewe kama wanadamu, kwa sababu katika kazi huria, ubunifu, ushirikishwaji na usaidizi, wanadamu hueleza na kuongeza utu wa hadhi ya maisha yao mwenyewe” (Rej. EG 192).
Matendo yaendane na vitendo
Baba Mtakatifu anakazia kusema kwamba kazi, na aina zake zote, huturuhusu kuwa waundaji-wenza na kushiriki katika ujenzi wa ulimwengu wa haki zaidi na wa kidugu. Kwa njia hiyo “Tumeitwa kuwa watu- chungu” ili kuwapatia wengine kitu cha kunywa. Wakati mwingine chungu kinabadilishwa kuwa msalaba mzito, lakini ni juu ya Msalaba ambapo, Bwana alitundikwa na akajitoa kwetu kama chanzo cha maji ya uzima. Tusiibiwe matumaini yetu!” (Rej. EG 86). Baba Mtakatifu aidha amependa kusisitizia juu ya haja ya kuwa na Kanisa linalisindikiza na ulimwengu wa kazi kutoka pembezoni. “Kujitolea kwetu hakuwezi kuwa kwa hotuba au vitendo vya pekee tu, lakini badala yake lazima iwe ushuhuda wa mara kwa mara wa mshikamano na msaada kwa wale wanaojikuta katika hali ya kazi na mazingira magumu ya kijamii.”
Kanisa lisindikize kuanzi pembezoni
Kuwa Kanisa linalosindikiza kuanzia pembezoni Papa amesisitiza tena kwamba, kunamaanisha kuwa karibu na wale wanaoteseka kutokana na hatari ya kazi na ukosefu wa fursa. Ni lazima tuwe uwepo ulio hai, tukitembea nao, tukiwasikiliza na kushirikiana katika kutafuta suluhisho za haki na za kudumu. Kazi yetu kama Wakristo haikomei kwenye kuta za makanisa yetu tu, bali inatusukuma kwenda kukutana na wale wanaohitaji upendo na udugu wetu zaidi. Ni muhimu kusimama na watu wanaofanya kazi ambao wanakabiliwa na kukata tamaa na kutengwa kwa sababu ya ukosefu wa kazi. Katika ulimwengu ambapo ukosefu wa ajira unaendelea kuathiri familia nyingi, kazi yetu kama Kanisa ni kuwapatia msaada wetu na tumaini letu, tukiwatia moyo ili wasipoteze imani na kutafuta fursa za kurudi katika ulimwengu wa kazi.
Endelezeni vifungu vya udugu
Papa Francisko amewatia moyo harakati hiyo ya Kihispania, kuendelea kusuka vifungo vya udugu, kwa kuleta mwanga wa Injili na kujenga jamii yenye uadilifu zaidi. Kama alivyosema katika utangulizi wa kitabu chenye kichwa: “Sasa zaidi kuliko hapo awali. Kujitolea kwa Kikristo katika ulimwengu wa kazi”, katika hafla ya kuadhimisha miaka 75 tangu kuanzishwa kwa harakati yao ya Matendo Kikatoliki, amewasihi waendelee kuwa watu wa Mungu “katikati ya maisha ya kazi, na kuendelea kusuka historia za upendo na kukumbatia. Hii ni kwa sababu Kanisa linawahitaji wao. Na kwa kuhitimisha, Ujumbe wake kwa Harakati hii ya Hoac amesema: Roho Mtakatifu awaongoze katika kazi yao na awaimarishe katika kujitolea kwao kila siku. Amewashukuru tena kwa kujitolea na kubariki mkutano huo, huku akinukuu tena kifungu cha waraka wake wa Evangelli Gaudium kuwa: “Twende mbele, tutoe yetu yote, lakini tufanye juhudi zetu kuwa na matunda kama apendavyo” (EG 279).