Umoja wa Mataifa: Siku ya Vijana Duniani Kwa Mwaka 2023: Stadi na Mazingira
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 12 Agosti inaadhimisha Siku ya Vijana Duniani iliyoanzishwa Mwezi Desemba mwaka 2009 na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia azimio namba 64/134. Maadhimisho ya Mwaka 2023 yananogeshwa na kauli mbiu: “Stadi kwa vijana zisizoharibu mazingira katika kuelekea dunia endelevu.” Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii anawataka vijana kamwe wasipoteze ujasiri wa kuota ndoto na kuishi kikubwa. Vijana wajitahidi kumwilisha utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira na hivyo kuwa ni sehemu ya vinasaba vya maisha yao na wajitahidi kuueneza. Vijana wajitahidi kuwa ni mabingwa wa udugu wa kibinadamu; wasimame kidete kukabiliana na changamoto; vijana wakabili changamoto za maisha kwa kujiruhusu kuongozwa na Mwenyezi Mungu, huku wakiwatafuta washauri wazuri.
Wakati huo huo, Bwana António Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaka kila mtu kokote pale aliko asaidie na ashikamane na vijana katika harakati zao za kujenga dunia inayosimikwa kwenye usawa, haki na endelevu kwa ajili ya binadamu na sayari. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema hayo katika ujumbe wake wa Siku ya Vijana Duniani inayoadhimishwa tarehe 12 mwezi Agosti kila mwaka kwa kusherehekea azma, mawazo na uongozi wa vijana katika mchakato wa kutafuta uwezekano wa ujenzi wa dunia bora zaidi. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, ushiriki wa vijana uwe katika kila jambo na kila wakati. Amefafanua kuwa katika changamoto zote zinazojitokeza katika ulimwengu mamboleo vijana wanataka kuchukuliwa kwa hatua za kijasiri, wakishikamana na wale walio hatarini zaidi, na kubuni majawabu ya kuhakikisha kuna haki za kiuchumi, kijamii na tabianchi, amani, ustawi na maendeleo kwa watu wote.
Bwana Guterres amesema ili kupanua wigo wa ushiriki wa vijana, hivi karibuni alizindua waraka wa kisera unaotoa wito kwa serikali kufanya ushiriki wa vijana kuwa kanuni ya lazima na si jambo la kuchagua wakati maalum pekee. “Ushiriki wao ufanyike katika maamuzi yote na sera zote duniani.” Vijana wawe na stadi za kumudu hali ya sasa. Amekumbusha kuwa kauli mbiu ya mwaka 2023 inakumbusha umuhimu wa kuhakikisha kwamba, vijana wanapata na kutumia stadi za kuwawezesha kumudu katika shughuli za kiuchumi zisizoharibu mazingira nyumba ya wote. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ametaja stadi hizo kuwa ni kuanzia teknolojia bunifu endelevu na nishati rejelezi hadi mapinduzi kwenye mifumo ya usafiri na shughuli za viwandani akisema, “vijana wanapaswa kupatiwa stadi hizo na ufahamu huo ili kuumba mustakabali safi, wa kijani zaidi, na unaojenga mnepo kwenye tabianchi siku za usoni.”