WYD Papa na Njia ya Msalaba na vijana:Msalaba ni ishara ya uzuri wa Upendo!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Ni nani angeweza kufikiria juu ya usanii uliojengwa wa jukwaa kubwa namna hiyo kwamba lilikuwa na maana gani, tangu kuanza kwa tukio kubwa la kiulimwengu hadi Ijumaa jioni ya tarehe 4 Agosti 2023, tulipowaona Vijana katika maadhimisho ya Siku ya 37(WYD), wakipanda na kushuka kutoka kwenye kiunzi ambacho kinaunda Kalvari ya ubunifu kwenye jukwaa kubwa lililowekwa kwenye Kilima cha Bustani ya Edoardo VII, jijini Lisbon. Haikuwa njia ya Msalaba ya kiutamaduni tuliyozoea, bali ni ya kibunifu kweli katika kiunzi hicho, na ndicho kilionesha kutoka kituo kimoja hadi kituo kingine, vijana wakiwa wanabeba msalaba wa Kristo.
Kwa hiyo hawa walionesha kuanguka na kuinuka tena, kama ilivyo katika ujenzi wa maisha, lakini hawakuwa peke yao: Yesu anatembea pamoja nao. Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na vijana alikumbusha hilo, ambaye katika hotuba yake bila kusoma aliwahimiza vijana wapatao 800,000 waliokuwapo kwamba: “Yesu anatembea kwa ajili yangu, kwa sababu hakuna aliye na upendo zaidi ya Yeye anayetoa maisha yake, kwa ajili ya marafiki zake na kwa wengine.” Yesu alitembea katika maisha yake yote, akiwahudumia wagonjwa, akiwasaidia maskini, akifundisha na kuhubiri, lakini ni njia ya kwenda Kalvari ambayo imesalia kuchorwa kwa undani katika moyo wa kila mtu. Safari yake ni Mungu atokaye ndani yake ili kutembea kati yetu, Papa Francisko alisisitiza kuwa na anafanya hivyo kwa upendo.
Msalaba uleule unaosindikiza kila tukio la Siku ya Vijana Ulimwenguni (WYD), ni picha ya safari hii yaani maana kuu ya upendo mkuu ule ambao Yesu alitaka kukumbatia maisha yetu. Msalaba ni jambo chungu, lakini ambalo tunaona uzuri wa upendo, alisisitiza Papa akikumbuka alivyoambiwa na mwamini mmoja kuwa “Bwana, kwa sababu ya uchungu wako usioelezeka ninaweza kuamini katika upendo”. Yesu pia anatembea na Kaleb, mwenye umri wa miaka 29 kutoka Marekani, ambaye alishuhudia mapambano yake dhidi ya mfadhaiko, kujidhuru na dawa za kulevya hadi kukutana Naye kulimruhusu kudhibiti maisha yake bila kurejea katika mazoea ya zamani na kuacha akakutana na mkewe.
Anatembea na Esther, mwanamke wa Kihispania mwenye umri wa miaka 34 kwenye kiti cha magurudumu baada ya ajali ya barabarani ambaye aliamua na mumewe wa sasa Nacho kukatiza ujauzito wake na ambaye sasa, baada ya Bwana kuja kumtafuta kwa upendo wake mkuu na usioelezeka ni mama wa mtoto mdogo Elisabeth. Na anatembea na João, wa Ureno mwenye umri wa miaka 23 mwathirika wa kunyanyapaliwa na matatizo ya afya ya akili baada ya karantini na janga la uviko, ambaye shukrani kwa imani alisaidiwa na kila anguko.
Katika kila kituo, vijana 50 kutoka nchi 21 duniani, wakisindikizwa na kwaya ya vipengele 62 na wapiga ala 30, walikumbusha kifo cha Kristo, na kuinama pamoja na woga na udhaifu wanaoupata vijana katika ulimwengu wa sasa. “Wanahisi mustakabali wao unachukuliwa kutoka kwao, wanaambiwa kuwa maisha yamejaa fursa, lakini ni ngumu kuona fursa ziko wapi hizo wakati pesa haitoshi, wakati mtu hawezi kupata kazi na wakati wa kupata elimu mara nyingi haiwezekani.” Wanalalamika juu yao wenyewe katika tafakari iliyoandikwa na Padre Nuno Tovar de Lemos, Mjesuit, ambaye alifafanua majibu ya uchunguzi kati ya vijana 20 kutoka mabara matano kuhusu ni wasi wasi gani mkubwa walio nao.
Vita, mashambulizi, ufyatulianaji risasi wa watu wengi, mateso ya kidini dhidi ya walio wachache huikumba dunia ambayo rasilimali zake zinanyonywa bila kudhibitiwa na ambapo watu wanakufa kwa njaa, huku wengine wakiugua kwa kula sana au kukimbia kutokana na hali zisizo za kibinadamu. Vurugu katika ndoa na mahusiano, unyanyasaji wa watoto, uonevu, matumizi mabaya ya mamlaka, ukatili, wasiwasi, huzuni mara nyingi hufuatana na maisha ya watoto, katika familia mahali ambapo maneno mazito kama mawe hutupiwa na kutofikiriwa kwa wazee.”
Kama hiyo haitoshi “bado kuna ugumu wa kupenda na kutokuwa na uwezo wa kutenda ili kufikia mfano uliowekwa na wa kibinafsi wa furaha, ambayo furaha inatimizwa kwa kungojea tabasamu tu kamilifu la selfie na umakini wa bandia “like” kama wengine, pamoja na hofu ya kuangukia katika dawa za kulevya, picha mbaya na pombe. “Hatuwezi kufanya maamuzi, wala hatuoni mwelekeo ambao historia inaweza kuendelea, na tunaona tu njia iliyofungwa na vikwazo vikubwa mbele yetu, " walishuhudia.
Hata hivyo, katika mwaliko wa Baba Mtakatifu aliokuwa ametangulia kuwaeleza ilikuwa ni kutoogopa, kwa sababu Yesu anatembea kuelekea msalabani na kufa msalabani ili roho zetu zitabasamu. Kila mtu maishani, tumelia na bado tunalia,” alisema muda mfupi kabla, huku akiwauliza vijana ni nini kiliwafanya walie maishani. Ni ile ambayo Yesu yuko pamoja nasi, na anatusindikiza katika giza linalotuletea machozi.” Anatembea na kusubiri kwa upendo wake, kwa huruma yake, kutufariji, kuyakausha machozi yetu yaliyofichika kwa huruma yake. Anasubiri hadi aone madirisha wazi ya roho zetu: Ni kwa jinsi gani ilivyo mbaya roho zilizofungwa ambazo hupanda ndani na kutabasamu ndani. Kristo anataka kujaza hofu zetu na faraja yake. Anafanya na anasubiri kutusukuma kukumbatia hatari ya kupenda". Hatari ambayo, Papa Francisko ametoa uhakikisho kuwa inafaa kuchukuliwa kila wakati.
Ifuatayo ni tafakari fupi ya Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kuanza Njia ya Msalaba katika Bustan ya Eduardo VII, jijini Lisbon katika siku ya vijana duniani. Papa ameanza kwa kusema: Leo mtatembea na Yesu. Yesu ndiye Njia na tutatembea naye, maana anatembea. Alipokuwa kati yetu, Yesu alitembea, alitembea akiponya wagonjwa, akiwasaidia maskini, akitenda haki... alitembea akihubiri, akitufundisha. Yesu anatembea, lakini njia iliyochorwa zaidi mioyoni mwetu ni njia ya Kalvari, njia ya Msalaba. Na leo ninyi, sisi, mimi pia, tutaifanya kwa upya njia ya Msalaba kwa maombi. Na tutamtazama Yesu apitapo na tutatembea pamoja naye. Njia ya Yesu ni Mungu atokaye ndani yake, na kutembea kati yetu. Tunayasikia mara nyingi sana katika Misa: Naye Neno alifanyika mwili, akatembea kati yetu. Je mnakumbuka ‘Naye Neno akawa mtu, akatembea kati yetu’? Na hii inafanywa kwa upendo. Anafanya kwa upendo. Na Msalaba unaosindikiza kila Siku ya Vijana Duniani ni picha na kielelezo cha safari hii.
Msalaba ndiyo maana kuu ya upendo mkuu zaidi, upendo ambao Yesu anataka kukumbatia maisha yetu. Yetu? … Ndiyo, yako, ya kila mmoja wetu. Yesu anatembea kwa ajili yangu. Sisi sote tunapaswa kusema. Yesu anachukua safari hii kwa ajili yangu, kutoa maisha yake kwa ajili yangu. Wala hakuna aliye na upendo mwingi kuliko yeye atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake, kuliko yeye atoaye uhai wake kwa ajili ya wengine. Msisahau hili: hakuna aliye na upendo mwingi kuliko yeye atoaye uhai wake, na Yesu alifundisha hili. Kwa sababu hii, tunapoangalia Msalaba, ambao ni mchungu sana, jambo gumu sana, tunaona uzuri wa upendo ambao hutoa maisha yake kwa kila mmoja wetu.”
Mwamini mmoja alisema sentensi ambayo ilinigusa sana. Alisema hivi: “Bwana, kupitia uchungu wako usioelezeka ninaweza kuamini katika upendo.” Na Yesu anatembea, lakini subiri kitu, subiri kampuni yetu, subiri tuangalie ... sijui, ngoja hadi ufungue madirisha ya roho yangu, ya roho yako, ya roho ya kila mmoja wetu. Jinsi gani roho zilizofungwa ni mbaya, ambazo hupanda ndani na kutabasamu ndani! Hazina maana. Yesu anatembea na kungoja na upendo wake, anangoja kwa huruma yake, kutupatia faraja, kukausha machozi yetu. Sasa ninawauliza swali, lakini msijibu kwa sauti: kila mtu ajibu ndani yake mwenyewe. Je, mimi hulia wakati mwingine? Je, kuna mambo maishani ambayo yananifanya nilie? Sote tumelia maishani, na bado tunalia. Na yupo Yesu pamoja nasi, analia pamoja nasi, kwa sababu anatusindikiza katika giza linalotupeleka machozi. Hebu tunyamaze kidogo, na kila mmoja amwambie Yesu kile anacholilia maishani; kila mmoja wetu ajisemee mwenyewe, sasa, kwa ukimya.
(Kipindi cha ukimya)
Yesu, kwa upole wake, anafuta machozi yetu yaliyofichika. Yesu anataka kujaza upweke wetu na ukaribu wake. Ni nyakati za kusikitisha kama nini za upweke! Naye yuko pale, anataka kuujaza upweke huu. Yesu anataka kujaza hofu yetu, hofu yako, hofu yangu, hofu hizo za giza anataka kuzijaza na faraja yake; na kusubiri kutusukuma kukumbatia hatari ya upendo. Kwa sababu, unaijua vema kuliko mimi: kupenda ni hatari. Lazima tuchukue hatari ya kupenda. Ni hatari, lakini inafaa kuchukua, na Yeye hufuatana nawe katika hili. Yeye daima anaongozana nasi, daima anatembea, daima, wakati wa maisha, yuko karibu nasi. Sitaki kusema mambo mengi sana. Leo tutatembea naye, njia ya mateso yake, njia ya mahangaiko yetu, njia ya upweke wetu. Sasa na hebu tunyamaze kwa sekunde na kila mmoja wetu afikirie juu ya mateso yake mwenyewe, afikiria juu ya wasiwasi wetu wenyewe, kufikiria juu ya taabu zetu wenyewe. Msiogope, mfikirie juu yake, na pia mfikirie juu ya shauku ya roho kutabasamu tena.”
(kipindi cha ukimya)
Na Yesu anatembea na Msalaba, anakufa Msalabani, ili roho zetu zitabasamu. Amina.