Ziara ya Kitume ya Papa Francisko huko Mongolia
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Katika matayarisho ya Ziara ya 43 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko kuelekea Nchini Mongolia, barani Asia mnamo tarehe 31 Agosti hadi tarehe 4 septemba 2023, Baba Mtakatifu Francisko, mara baada ya Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana, kwa waamini na mahujaji waliokusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 27 Agosti 2023 amewatangazia kuhusu tukio la ziara yake hiyo.
Baba Mtakatifu amesema: “Siku ya Alhamisi ijayo nitaondoka katika safari ya siku chache katikati ya moyo wa Asia, nchini Mongolia. Ni ziara iliyotarajiwa sana, ambayo itakuwa ni fursa ya kulikumbatia Kanisa ambalo ni dogo kwa idadi lakini lililo hai katika imani na kubwa katika mapendo; na pia kukutana kwa ukaribu na watu mashuhuri, wenye busara na mapokeo makubwa ya kidini ambayo nitapata heshima ya kujua, hasa katika muktadha wa tukio la kidini.” Baba Mtakatifu aidha ametaka kuwaelekea wao kuwa: “Na sasa ningependa kuwalekea, ninyi kaka na dada wa Mongolia, nikiwaambia kwamba nina furaha kusafiri ili kuwa kati yenu kama ndugu wa wote. Ninashukuru Mamlaka yenu kwa mwaliko mzuri na wale wote wanaoandaa ujio wangu kwa dhamira kubwa. Ninaomba kila mtu asindikize ziara hii kwa maombi.”
Sala kwa ajili ya wathirika wa moto
Akiendelea na Salamu, Baba Mtakatifu amesema “Pia ninawahakikishia ukumbusho wangu katika maombi yangu kwa waathiriwa wa moto ambao umezuka siku za hivi karibuni huko kaskazini-mashariki mwa Ugiriki, na ninaonesha mshikamano wangu na watu wa Ugiriki. Na sisi pia daima tubaki karibu na watu wa Kiukraine, wanaosumbuliwa na vita, na wanateseka sana: tusisahau Ukraine.”
Salamu kwa mahujaji
“Ninawasalimu ninyi nyote, Warumi na mahujaji kutoka Italia na kutoka nchi nyingi.nHasa, ninasalimia kikundi cha parokia ambao wametoka Madrid; mapadre wa Jimbo la Molfetta-Ruvo-Giovinazzo-Terlizzi, pamoja na Askofu wao; waamini wa Mtakatifu Cajetan wa Thiene huko Melìa; familia za wilaya ya Pizzo Carano ya Mtakatifu Cataldo na waendesha baiskeli wa Ciociaria. Nawasalimu watumishi wa madhabahu ya kitengo cha kichungaji cha Codevigo, jimboni Padova, wakiwa katika hija yao jijini Roma pamoja na paroko wao.” Na hatimaye Baba Mtakatifu amesema “Na ninawatakia Dominika njema nyote. Tafadhali msisahau kuniombea. Mlo mwema, mchana mwema na kwaheri kuonana!
Kauli mbiu ya Ziara yake: “Kutumainia Pamoja”
“Kutumainia Pamoja” ndiyo kauli mbiu ya ziara yake ya kitume ambayo ilielezwa na Ofisi ya vyombo vya Habari ya Vatican, kwamba “tulitaka kutia nuru ya maana mbili za safari ya kitume ya Baba Mtakatifu huko Mongolia: kwanza ikiwa ni ziara ya kichungaji na ziara ya kiserikali. “Kwa hivyo, chaguo lilikuwa la maadili ya Kikristo (ambayo ni matumaini), lakini yaliyoshirikishwa sana katika mizunguko usiyo ya Kikristo, ikihusishwa na kielezo pamoja, ili kusisitiza umuhimu wa ushirikiano wa nchi mbili kati ya Vatican na Mongolia.”
Kwa hiyo, matumaini ya pamoja yanawakilisha, hali ya kawaida na pia kipengele muhimu kinachoweza kubainisha safari yaani “uwepo wa Baba Mtakatifu unawakilisha kwa sehemu hii ndogo ya watu wa Mungu ishara ya matumaini na faraja kubwa na kwa upande mwingine kwa Kanisa lililoko Mongolia, pamoja na udogo na upendeleo wake, linaweza kutoa ishara ya matumaini kwa Kanisa la kiulimwengu.”
Nembo ya ziara ya Kipapa nchini Mongolia
Kwa mujibu wa Ofisi ya Vyombo vya Habari Vatica walikuwa wameeleza kuwa “Nembo inaonesha ramani ya Mongolia, iliyo na rangi nyekundu na bluu ambayo ni bendera ya taifa. Ndani yake, kuna nyumba ya jadi ya Kimongolia) ambayo moshi wa njano wenye rangi ya benedera ya Vatican unatoka juu. Upande wa kulia wa nyumba hiyo umesimama msalaba. Kushoto mwa Nyumba na kulia mwa msalaba kuna maandishi mawili yaliyosimamishwa wima, katika lugha ya Kimongolia, yenye kauli mbiu: “Kutumaini Pamoja.”