2021.12.05 :Papa alipotembelea Cyprus na Ugiriki katika kituo cha wahamiaji cha Mytilene 2021.12.05 :Papa alipotembelea Cyprus na Ugiriki katika kituo cha wahamiaji cha Mytilene  (Vatican Media)

Katika siku ya 109 ya Wahamiaji Papa amehitimza uhuru wa kuhama au kubaki

Katika salamu kwa waamini katika Uwanja wa Mtakatifu Petro,Papa amekumbusha siku ya Wahamiaji na wakimbizi na kusisitiza umuhimu wa kuwa na uhuru wa kukaa au kuondoka katika nchi pamoja na ule wa kukaribishwa popote mtu anapokwenda.Papa ametoa mwaliko wa mkesha wa kiekumeni Septemba 30.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Dominika tarehe 24 Septemba 2023 ni maadhimisho ya Siku ya 109 ya wahamiaji na wakimbizi ambapo mara baada ya Tafakari na Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu akiwageukia waamini na mahujaji kutoka pande zote za dunia waliounganika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro amesema: “Leo ni Siku ya Wahamiaji na Wakimbizi Duniani, yenye kaulimbiu: “Huru kuchagua kuhama au kubaki”, ili kukumbusha kwamba kuhama kunapaswa kuwa chaguo huru, na kamwe si jambo pekee lisilowezekana. Hakika, haki ya kuhama sasa imekuwa wajibu kwa wengi, na hasa mahali ambapo panapaswa kuwepo haki ya kutohama, kubaki katika nchi ya mtu mwenyewe. Ni lazima kwa kila mwanamume na mwanamke kuhakikishiwa haki ya kuishi maisha yenye heshima katika jamii anamojikuta. Kwa bahati mbaya, umaskini, vita na mgogoro wa tabianchi huwalazimisha watu wengi kukimbia. Kwa hivyo, sote tunatakiwa kuunda jumuiya ambazo ziko tayari na wazi kukaribisha, kukuza, kusindikiza na kuunganisha wale wanaobisha hodi kwenye milango yetu.”

Siku ya wahamiaji na wakimbizi
Siku ya wahamiaji na wakimbizi

Baba Mtakatifu akikumbuka ziara iliyompeleka Kusini mwa Ufaransa ameongeza kusema: “Changamoto hii ilikuwa katikati ya Rencontres Méditerranéennes, yaani Mikutano ya Mediteranea ambayo ilifanyika katika siku za hivi karibuni huko Marsiglia na katika kikao chake cha kuhitimisha nilishiriki jana, nikisafiri hadi jiji, njia panda ya watu na tamaduni.” Baba Mtakatifu akiendelea amesema: “Ninatoa shukrani za pekee kwa maaskofu wa Baraza la Maaskofu wa Italia ambao wanafanya kila wawezalo kuwasaidia kaka na dada zetu wahamiaji. Tumemsikia hivi punde Askofu Mkuu Baturi kwenye televisheni, katika kipindi cha “A Sua Immagine” akifafanua hili.”

Papa alikutana na wahamiaji na wakimbizi
Papa alikutana na wahamiaji na wakimbizi

Papa amesalimia wote kuanzia na  Warumi na mahujaji kutoka Italia na nchi nyingi, hasa Seminari ya Kimataifa ya Jimbo la Redemptoris Mater ya Cologne, nchini Ujerumani. Kadhalika amesalimia kundi la watu walioathiriwa na ugonjwa adimu unaojulikana kama ataxia, wakiwa na wanafamilia zao. Papa amesema “Ninarudia mwaliko wangu wa kushiriki katika mkesha wa maombi ya kiekumeni, yenye jina la “Pamoja”, utakaofanyika Jumamosi hii ijayo tarehe 30 Septemba katika Viwanja vya Mtakatifu Petro, kwa ajili ya maandalizi ya Kusanyiko la Sinodi litakaloanza tarehe 4 Oktoba.” Baadaye Papa amesema: “Hebu tukumbuke Ukraine inayaokabiliwa na tuwaombee watu hawa wanaoteseka sana." Kwa kuhitimisha akiwaaga amesema: "Ninawatakia Dominika njema. Tafadhali msisahau kuniombea. Mlo mwema na mchana mwema. Kwaheri ya kuonana.”

Waamini na mahujaji 24 Septmba katika uwanja wa Mtakatifu Petro
Waamini na mahujaji 24 Septmba katika uwanja wa Mtakatifu Petro

Siku ya 109 ya wahamiaji na wakimbizi duniani kwa mwaka 2023 inaongozwa na kaaauli mbiu “Uhuru wa Kuchagua Kuhama au Kubaki ambayo inasisitiza kuhamaisha ufahamu mpya kuhusu haki ya kuhama au kubaki nyumbani na katika nchi yako mwenyewe ulikozaliwa. Katika ujumbe wa Papa Francisko katika fursa hiyo alifafanua juu ya sababu  zinazowalazimisha watu kuzikimbia au kuzihama nchi zao kama vile Vita, Majanga asilia , utawala mbaya na mengine ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Haki ya kubaki nchini mwake ina mizizi yake katika maisha ya mwanadamu, kwani hii ni haki kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Uwanja wa Michezo Velodrome, Marsiglia wakati wa misa 23 Septemba na Papa
Uwanja wa Michezo Velodrome, Marsiglia wakati wa misa 23 Septemba na Papa

Chimbuko la Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani ni kutokana ni mahangaiko pamoja na mateso ya watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia kutokana na madhara makubwa ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia. Papa Pio X, mnamo mwaka 1914 akawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wakimbizi na wahamiaji duniani. Papa Benedikto XV akaanzisha siku hii rasmi na kunako mwaka 1952 ikaanza kusherehekewa na Kanisa la Kiulimwengu. Lakini ilikuwa mnamo  1985, ambapo Mtakatifu Yohane Paulo II akawa kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki kuanza kutoa ujumbe kwa ajili ya Maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani, kama sehemu ya sera na mbinu mkakati wa Kanisa katika shughuli za kichungaji ili kusikiliza na kujibu kwa dhati kilio cha wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Mkumbatio wa mmoja wa wahamiaji na wakimbizi katika moja ya ziara zake za kitume
Mkumbatio wa mmoja wa wahamiaji na wakimbizi katika moja ya ziara zake za kitume

Kwa njia hiyo katika ujumbe wa Papa Francisko wa siku hii anabainisha kuwa sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha. Si kwa bahati mbaya, haya yote ameyarudia katika hotuba zake wakati wa Ziara ya Kitume ya 44 huko Marsiglia katika kuhitimisha mikutano ya Mediterania inayohusu hali hii ngumu. Na hata akizungumza na waandishi wa habari walioandamana nao.

Siku ya Wahamiaji na wakimbizi duniani
24 September 2023, 14:12