Kwa dakika moja kuonesha siku mbili za kwanza za Papa huko Mongolia!
Na Angella Rwezaula, Vatican.
Kabla ya kukutana na Kanisa mahalia(Maaskofu, Mapadre, watawa kike na Kiume na wahudumu wa Kichungaji) katika Kanisa kuu la Watakatifu Petro na Paulo huko Ulaanbaatar, Papa Francisko alikutana na mwanamke ambaye aliokota sanamu ya Mama, yaani “Mama wa Mbinguni, Maria" kwenye takataka. Kwa hiyo ni karibu na nje ya Kanisa kuu huko Ulaanbaatar, kuna Geri ambapo Papa Francisko alikutana na mwanamke huyo, Bi. Tsetsege, mama wa watoto kumi na moja, na ambaye muongo mmoja uliopita aliokota hiyo sanamu ya mbayo iliyochongwa vizuri na yenye sura za mwanamke mzuri sana, lakini ambayo ilikuwa imetupwa kwenye dampo la takataka.
Hata hivyo katika maelezo ni kwamba Mwanamke huyo hakuelewa mara moja kwamba hiyo sanamu alikuwa na maana ya Bikira Safi. Mara baada ya kurudi nyumbani, alinong'ona katika familia yake kwamba “mwanamke huyu mrembo alitaka kuja na kuishi katika hema langu". Mara tu alipoelewa yeye ni nani, mwanamke huyo alitoa zawadi ya sanamu hiyo kwa Jumuiya ya Wakatoliki, ambayo ilioneshwa katika parokia moja mahalia. Historia ya sanamu ya Bikira Maria ilifafanuliwa baadaye na Kardinali Giorgio Marengo, Msimamizi wa Kitume huko Ulaanbaatar kwamba: "Mara moja nilifikiri kuwa kupitia ugunduzi huu, Bikira alitaka kutuambia kitu."
Kardinali Marengo aidha alisema kwamba hakuweza kueleza jinsi gani sanamu hiyo iliishia kwenye jaa la takataka ikizingatiwa kwamba, hasa katika sehemu hiyo ya nchi, kuna Wakatoliki wachache sana. Kwa hiyo alifikiri kuwa Bwana, kupitia kwa Mama yake Mtakatifu, alijifanya kuwepo katika hali mbaya zaidi “ili atuambie jinsi alivyo karibu na kila mmoja wetu”, Kardinali Marengo alikumbusha hayo kwenye makala ya hivi karibuni katika Gazeti la Osservatore Romano.
Kardinali Marengo pia alisisitiza kwamba “Bikira yuko tayari kukutana nasi hata katika sehemu za kukata tamaa, upotevu, maumivu, na kutelekezwa. “Pia nilizungumzia kuhusu sanamu na Baba Mtakatifu nilipomtembelea na ujumbe mdogo wa watawa wa Kibudha kutoka Mongolia, ambapo Nilimwonesha picha na alifurahi sana". Mnamo tarehe 8 Desemba 2022, sanamu ya Bikira Maria ilitawazwa katika Kanisa kuu la Ulaanbaatar na kufunikwa kwa vazi lililoundwa na vipande vidogo vya nguo vilivyotumwa na waamini wengi wa Kimongolia na wamisionari. Katika hafla hiyo, Kardinali Marengo aliweka wakfu Mongolia yote kwa Mama Bikira Maria. Na kwa hiyo Kardinali alisema: “Na Mama wa Mbinguni amekuwa picha ya Kanisa hili changa.”