Misa ya Papa katika Uwanja wa Valodrome:Ulaya ijipyaishe kukarimu upendo
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Maisha yetu, ya Kanisa, Ufaransa na Ulaya yanahitaji neema ya mruko mpya wa imani, upendo na matumain. Yalikuwa ni kiini cha mahubiri ya Baba Mtakatifu katika Uwanja wa Mchezo Velodrome huko Marsiglia , Jumamosi tarehe 23 Septemba 2023 akiwa katika hatua ya mwisho wa ziara yake ya 44 ya kitume ya siku mbili, kusini mwa Ufaransa. Katika mahubiri mara baada ya masomo, yamejikita juu ya ushuhuda wa Maria kwenda kumtembelea Elizabeth. Kwahiyo Baba Mtakatifu akianza amesema Maandiko yanatuambia kwamba, baada ya kusimamisha ufalme wake, Mfalme Daudi aliamua kulisafirisha Sanduku la Agano hadi Yerusalemu. Baada ya kuwaita watu, alisimama na kwenda kulileta Sanduku; njiani, yeye na watu walicheza mbele yake, wakishangilia katika uwepo wa Bwana (2Sam 6:1-15). Ni kutokana na tukio hilo ambapo mwinjili Luka anasimulia kuhusu ziara ya Maria kwenda kwa binamu yake Elizabeti. Maria pia, aliinuka hupesi na kuanza kuelekea eneo la Yerusalemu, na anapoingia katika nyumba ya Elisabeti, mtoto aliyembeba, akitambua kuwasili kwa Masiha, aliruka kwa furaha na kuanza kucheza kama Daudi alivyokuwa akicheza mbele ya Sanduku (rej. Lk 1:39-45).Maria, basi, anaoneshwa kama Sanduku la kweli la Agano, akimtambulisha Bwana aliyefanyika mwili ulimwenguni. Yeye ndiye Bikira kijana aliyekwenda kukutana na mwanamke tasa, mzee na, katika kumpeleka Yesu, anakuwa ishara ya kutembelewa na Mungu ambayo inashinda utasa wote. Yeye ndiye Mama anayepanda milima ya Yuda, kutuambia kwamba Mungu anakwenda kututafuta kwa upendo wake, ili tufurahi kwa furaha.
Baba Mtakatifu akiendelea na tafakari hiyo kuhusiana na Injili ya ziara iliyosomwa amesema katika wanawake hawa wawili, Maria na Elizabeti, ziara ya Mungu kwa wanadamu inafunuliwa. Mmoja ni kijana na mwingine mzee, mmoja ni bikira na mwingine tasa, lakini wote wawili wana mimba kwa njia ‘isiyowezekana.’ Hii ni kazi ya Mungu katika maisha yetu; anawezesha hata kile kinachoonekana kuwa hakiwezekani, anazalisha maisha hata katikati ya utasa. Kwa hiyo Baba Mtakatifu amependa kusema kwamba “tujiulize kwa uaminifu, kutoka moyoni: Je, tunaamini kwamba Mungu anatenda kazi katika maisha yetu? Je, tunaamini kwamba Bwana, kwa njia zilizofichika na mara nyingi zisizotabirika, anatenda katika historia, anafanya maajabu, na anafanya kazi hata katika jamii zetu ambazo zimeainishwa na hali ya kiulimwengu na kutojali fulani kwa kidini? Kuna njia ya kutambua kama tuna imani hii katika Bwana au la. Injili inasema kwamba mara Elizabeti aliposikia salamu ya Maria, mtoto akaruka ndani ya tumbo lake". Hii ndio ishara: kuruka kwa furaha. Yeyote anayeamini, yeyote anayeomba, yeyote anayemkaribisha Bwana huruka katika Roho, na anahisi kwamba kitu kinaendelea ndani, na kucheza kwa furaha.
Kwa nja hiyo Baba Mtakatifu amependa kujikita zaidi katika suala la mruko wa imani. Uzoefu wa imani, kwanza kabisa, unaleta aina fulani ya kurukaruka katika uso wa maisha. Kuruka-ruka kunamaanisha “kuguswa ndani,” na kuwa na hisia kali la ndani, kuhisi kwamba kuna jambo linalosonga moyoni mwetu. Hii ni kinyume cha moyo wa kiju juu tu, wa baridi, ambao umezoea maisha ya kimya, ambayo yanaingizwa kutojali na huwa haupatikani. Moyo kama huo unakuwa mgumu na usio na hisia kwa kila kitu na kila mtu, hata kwa kutupwa kwa kutisha kwa maisha ya mwanadamu, ambayo inaonekana leo katika kukataliwa kwa wahamiaji wengi, watoto wengi ambao hawajazaliwa na wazee waliotelekezwa. Moyo baridi na tambarare huvuta maisha kimawazo, bila shauku, bila msukumo, bila hamu. Katika jamii yetu ya Ulaya, mtu anaweza kuwa mgonjwa kutokana na haya yote na kuteseka kwa wasiwasi, kutoridhika, kukata tamaa, kutokuwa na uhakika na huzuni kwa jumla. Mtu fulami ameita tabia hizi tamaa za kusikitisha na zinapatikana kwa wale ambao hawaruki katika uso wa maisha.
Wale waliozaliwa kwa imani, kwa upande mwingine, wanatambua kuwapo kwa Bwana, kama mtoto mchanga katika umbu la Elisabeti. Wanatambua kazi yake kila siku inapopambazuka na kupokea mitazamo mipya ya kuona ukweli. Hata katikati ya taabu, matatizo na mateso, kila siku wanatambua kutembelewa na Mungu kati yetu na kuhisi kusindikizwa na kutegemezwa naye. Wanakabiliwa na fumbo la maisha na changamoto za jamii, wale wanaoamini wana chemchemi katika hatua yao, shauku, ndoto ya kulima, maslahi ambayo yanawasukuma kujitolea binafsi. Wanajua kwamba katika kila jambo Bwana yupo, akiwaita na kuwaalika kushuhudia Injili kwa upole, ili kujenga ulimwengu mpya, kwa kutumia karama na talanta walizopokea. Baba Mtakatifu Francisko kwa njia hiyo amesema imani kutuwezesha kurukaruka katika uso wa maisha, uzoefu wa imani pia hutulazimisha kuruka kuelekea kwa jirani yetu. Hakika, katika fumbo la Kutembelewa, tunaona kwamba kutembelewa na Mungu hakufanyiki kwa njia ya matukio ya ajabu ya mbinguni, bali kwa urahisi wa kukutana. Mungu anakuja kwenye mlango wa nyumba ya familia, katika kumbatio la huruma kati ya wanawake wawili, katika ujauzito wote wawili kwa ajabu na matumaini. Hapo tunaona maombi ya Maria, ajabu ya Elizabeti, na furaha ya kushiriki.
Papa amehimiza kwamba daima tukumbuke hili katika Kanisa: Mungu ni wa uhusiano na mara nyingi hututembelea kupitia mikutano ya kibinadamu, hasa wakati tunapojua jinsi ya kuwa wazi kwa wengine, wakati kuna kichochezi ndani yetu kwa ajili ya wale wanaotupita kila siku, na wakati mioyo yetu haibaki migumu na isiyo na hisia mbele ya majeraha ya wale walio dhaifu. Miji yetu mikuu na nchi nyingi za Ulaya kama Ufaransa, ambapo tamaduni na dini tofauti huishi pamoja, ni nguvu kali dhidi ya kupindukia kwa ubinafsi, ugumu na kukataliwa ambapo husababisha upweke na mateso. “Hebu tujifunze kutoka kwa Yesu jinsi ya kujichochea ili kuwasaidia wale wanaoishi karibu. Acheni tujifunze kutoka kwake ambaye anachochewa na huruma mbele ya umati uliochoka na kuelemewa (rej. Mk 6:34) na “kuruka kwa huruma mbele ya mwili iliojeruhiwa kwa wale anaokutana nao. Kama vile mmoja wa watakatifu wao wakuu, Vincent wa Pauli, anavyohimiza, kuwa “tunapaswa, basi, kulainisha mioyo yetu na kuwafanya watambue mateso na taabu za jirani yetu. Na ndivyo hivyo tunapaswa kumwomba Mungu atupatie roho hiyo ya huruma ambayo ni Roho ya Mungu mwenyewe,” hadi kufikia hatua ya kutambua kwamba maskini ni “mabwana wetu.”
Papa Francisko aidha amefikiria juu ya “msisimko” mwingi ndani ya Ufaransa, pamoja na historia yake iliyojaa utakatifu na utamaduni; wasanii na wanafikra ambao wamehamasisha vizazi vingi. Leo, pia, maisha yetu na ya Kanisa, Ufaransa na Ulaya yanahitaji haya: neema ya kuruka mbele, hatua mpya ya imani, mapendo na matumaini. Tunahitaji kufufua shauku na utashi wetu, kuamsha tena hamu yetu ya kujitolea kwa udugu. Tunahitaji kwa mara nyingine kuhatarisha kupenda familia zetu na kuthubutu kupenda walio dhaifu zaidi, na kugundua tena katika Injili neema inayobadilisha ambayo hufanya maisha kuwa mazuri.” Papa amesisitiza Hebu tumtazame Maria, ambaye anajisumbua kuanza safari na ambaye anatufundisha kwamba hii ndiyo njia ya Mungu: Yeye hutusumbua, hutuweka katika mwendo na kutufanya turuke sawa na uzoefu wa Elizabeth. Tunataka kuwa Wakristo wanaokutana na Mungu katika maombi, na kaka na dada zetu kwa upendo; Wakristo wanaorukaruka, kusukuma na kupokea moto wa Roho Mtakatifu na kisha kujiruhusu kuchomwa moto na maswali ya siku zetu, na changamoto za Mediterania, kwa kilio cha maskini na kwa utopia mtakatifu wa udugu na amani ambayo inangoja kupatikana.
Papa Francisko amesema pamoja nao, anamuomba Mama Yetu wa Ulinzi kwamba achunge maisha yao, kwamba ailende Ufaransa na Ulaya yote, na kwamba awafanye waruke katika Roho. Alipenda kutoa maombo hayo kwa kutumia maneno ya Paul Claudel: “Naona kanisa, limefunguliwa…. Sina cha kutoa na sina cha kuomba. Ninakuja, Mama, kukutazama tu. Kukutazama, kulia kwa furaha, nikijua kuwa mimi ni mwanao, na wewe upo…. Kuwa nami Maria, mahali hapa ulipo…. Kwa sababu upo, siku zote… Kwa sababu wewe ni Maria… Kwa sababu tu upo… Mama wa Yesu Kristo, asante kuwa wako: (“The Virgin at Noon”, Poëmes de Guerre 1914-1916, Paris, 1992). Alihitimisha.