Tafuta

2023.09.04 Papa Francisko kwa wahudumu wa upendo katika Nyumba ya Huruma huko Mongolia. 2023.09.04 Papa Francisko kwa wahudumu wa upendo katika Nyumba ya Huruma huko Mongolia.  (Vatican Media)

Papa azindua Nyumba ya Huruma:kuteseka na wengine ndiyo maana ya upendo

Mwandishi alipomwona mama Teresa wa Kalkuta ameinamia vidonda vyenye harufu mbaya ya mtu mgonjwa,mara moja alimwambia,“Unachofanya ni kizuri,lakini,mimi binafsi,singefanya hivyo hata kwa dola milioni.”Mama Teresa alijibu,“Singefanya hivyo kwa dola milioni pia.Ninafanya hivyo kwa ajili ya upendo wa Mungu!”Papa amewashauri wafanye hivyo.

Na Angella Rwezaula, - Vatican.

Hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko  wakati wa Mkutano na Wanachama wa Mashirika ya kutoa Msaada na Uzinduzi wa Nyumba ya Huruma huko  Ulaanbaatar tarehe  4 Septemba 2023. Akianza hotuba yake amewashukuru kwa  ukaribisho mzuri waliompatia na kwa wimbo na dansi yao, maneno yao ya salamu na ushuhuda wao! Kwa hiyo amefikiria Papa Francisko kuwa  yanaweza kujumlishwa katika maneno ya  Yesu kuwa: “Nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula, nilikuwa na kiu nanyi mkaninywesha” (Mt 25:35). Kwa maneno hayo, Bwana anatupatia kigezo cha kumtambua yeye aliyepo katika ulimwengu wetu na hali ya kuingia katika furaha kuu ya ufalme wake kwenye Hukumu ya Mwisho. Tangu mwanzo kabisa, Kanisa lilichukua maneno hayo kwa uzito, likionesha kwa vitendo kwamba upendo ni kipengele cha msingi cha utambulisho wake. Kwa hiyo Baba Mtakatifu amesisitiza kwamba Upendo ni kipengele cha msingi cha utambulisho wa Kanisa. Vile vile kufikiria masimulizi katika Matendo ya Mitume na njia mbalimbali ambazo jumuiya ya kwanza ya Kikristo iliweka maneno ya Yesu katika matendo, ili kujenga Kanisa lililowekwa imara juu ya nguzo nne: ushirika, liturujia, huduma na ushuhuda.

Inafurahisha kuona jinsi, baada ya karne nyingi, roho hiyo hiyo inaenea  katika Kanisa la Mongolia, ingawa ni ndogo kwa ukubwa, lakini maisha yake yanatambulika kwa ushirika wa kidugu, sala, huduma ya kujitolea kwa wale wanaohitaji, na ushuhuda wa imani yake. Sawa na safu nne za wima za Geri yaani nyumba ya kijadi kubwa zinazotegemeza pete ya kati ya juu, huruhusu muundo mzima kusimama wima na kutoa nafasi ya kukaribisha ndani. Kwa hivyo Baba Mtakatifu amebainisha kuwa waliokuwa pamoja katika nyumba hiyo waliyoijenga na ambayo leo hii amekuwa na furaha ya kuibariki na kuizindua. Inasimama kama kielelezo halisi cha huduma hiyo kwa wengine ambayo ni alama maalumu ya jumuiya ya Kikristo; kwa maana pale tunapopata kukaribishwa, ukarimu na uwazi kwa wengine, tunapumua “manukato ya Kristo” (rej. 2 Kor. 2:15). Huduma ya ukarimu kwa majirani zetu, kwa  kujali afya zao bora, mahitaji yao ya kimsingi, elimu na utamaduni imetofautisha sehemu hii hai ya Watu wa Mungu na kuanzishwa kwake.” Papa Francisko amesisitiza.

Papa amekutana na watu wahudumu wa kujitolea huko chini Mongolia na kuzindua kituo cha huruma

Tangu wakati wa kuwasili kwao Ulaanbaatar katika miaka ya 1990, wamisionari wa kwanza mara moja waliona wito kwa kazi za upendo, ambao uliwaongoza kuwatunza watoto waliotelekezwa, kaka na dada zetu wasio na makao, wagonjwa, walemavu, wafungwa na wale wote, katikati ya mateso, walitafuta utunzaji wao. Leo tunaona kwamba, kutokana na mizizi hiyo, mti umeota, matawi yameenea na matunda mengi yameonekana kwa namna ya mipango mbalimbali ya upendo inayosifiwa. Hii nayo imeendelea kuwa mipango  ya muda mrefu, inayofanywa zaidi na Taasisi mbalimbali za kimisionari zilizopo huko  na kuthaminiwa sana na idadi ya watu na mamlaka za kiraia. Kwa hakika, serikali ya Mongolia yenyewe ilikuwa imeomba msaada kutoka kwa wamisionari Wakatoliki katika kukabiliana na dharura nyingi za kijamii za nchi ambayo, wakati huo, ilikuwa katika awamu nyeti ya mabadiliko ya kisiasa na yenye umaskini ulioenea. Mipango  hiyo inaendelea kutegemea kujitolea kwa wamisionari kutoka nchi nyingi wanaoweka ujuzi wao, uzoefu, rasilimali na hasa upendo wao, katika huduma ya jamii ya Wamongolia. Kwao, kwa hiyo na kwa wale wote wanaounga mkono kazi hizi nyingi nzuri, ametoa shukrani za dhati.

Nyumba hiyo ya Huruma Papa amesema inakusudiwa kuwa sehemu ya marejeo ya kazi mbalimbali za upendo yaani mikono iliyonyooshwa kuelekea kaka na dada zetu wanaojitahidi kukabiliana na matatizo ya maisha. Mahali pa usalama, kwa maneno mengine, ambapo watu wanaweza kupata sikio la kusikiliza na moyo wenye kuelewa. Ingawa sio tofauti na mipango mingine mingi inayoungwa mkono na taasisi mbali mbali za Kikatoliki, kazi hiyo mpya pia ni maalum, kwani hapo ndilo Kanisa mahalia  linalofanya kazi hiyo, likiratibu juhudi za vikundi vyote vya wamisionari, huku likihifadhi utambulisho wa mahali waziwazi kuwa usemi halisi wa Jimbo la Kitume kwa ujumla wake. Papa Francisko amependa sana jina walilochagua kuwa  “Nyumba ya Huruma”. Maneno hayo mawili yana ufafanuzi wa Kanisa, ambalo linaitwa kuwa nyumba, ambamo watu wote wanakaribishwa na wanaweza kupata upendo wa hali ya juu zaidi unaosisimua na kugusa moyo: upendo mwororo na majaliwa ya Baba, ambaye anataka sisi sote tuwe ndugu na fadhili kwa  ndugu nyumbani kwake. Ni matumaini ya Papa, basi, kwamba wote wanaweza kuchangia mpango huo na kwamba jumuiya mbalimbali za wamisionari zitashiriki kikamilifu katika mpango huo kupitia kujitolea kwa wafanyakazi na rasilimali.

Mtoto anamsalimu Papa
Mtoto anamsalimu Papa

Kwa hiyo  kutokea watu wa kujitolea mchango wao ni muhimu sana. Huduma ya ukarimu kabisa na isiyo na ubinafsi ambayo watu huchagua kwa hiari kutoa kwa wale wanaohitaji, si kwa kujali malipo ya kifedha au manufaa ya kibinafsi, bali kwa upendo safi wa jirani zao. Huu ndio “mtindo” wa utumishi ambao Yesu alitufundisha alipowaambia wanafunzi wake: “Mmepokea bure, na toeni bure” (Mt 10:8). Kutumikia wengine kwa njia hiyo kunaweza kuonekana kuwa ni jambo lisilofaa, lakini mara tu wanapojiweka kwenye mstari wa mbele, wale wanaojitolea wakati na jitihada zao hugundua kwamba chochote wanachotoa bila kutarajia malipo yoyote hakipotee kamwe, lakini badala yake kinakuwa hazina kubwa. Kwa hakika, ukarimu sio mzigo, bali huponya majeraha ya moyo, hutuleta karibu na Mungu, huwa chanzo cha shangwe, na hutuweka kuwa wadogo ndani. Katika nchi hiyo ya Mongolia  iliyojaa vijana sana,  Papa Francisko ameisisitiza kuwa kazi ya kujitolea inaweza kuwa njia madhubuti kuelekea ukuaji wa kibinafsi na wa kijamii.

Aidha Baba Mtakatifu amesema kuwa hata katika jamii zilizoendelea kiteknolojia zenye viwango vya juu vya maisha, mifumo ya ustawi wa jamii pekee haitoshi kutoa ya huduma zote zinazohitajika. Kufanya hivyo kunahitaji vikosi vya watu wa kujitolea ambao wako tayari kujitolea wakati wao, ujuzi na rasilimali kwa upendo kwa wengine. Maendeleo ya kweli ya taifa hayapimwi na utajiri wa kiuchumi, sembuse kwa uwekezaji katika uwezo wa udanganyifu wa silaha, bali kwa uwezo wake wa kutoa afya, elimu na maendeleo shirikishi watu wake. Kwa sababu hiyo Baba Mtakatifu amependa  kuwatia moyo wananchi wote wa Mongolia, ambao wanajulikana sana kwa ukarimu na uwezo wao wa kujitolea, kushiriki katika kazi ya kujitolea, kujiweka wenyewe katika huduma ya wengine. Hapo, katika Nyumba ya Huruma kuna uwanja wa mafunzo"ambao daima uko wazi, ambapo unaweza kutekeleza shauku zao  kwa mema na kufundisha mioyo yao.

Papa amekutana na watu wa kujitolea tarehe 4 Septemba 2023
Papa amekutana na watu wa kujitolea tarehe 4 Septemba 2023

Hatimaye, Papa Francisko amependa kukataa hadithi  fulani za kufikirika.  Ya  Kwanza Papa amesema ni kwamba ni wenye utajiri pekee wanaoweza kushiriki katika kazi ya kujitolea. Hiyo ni mawazo yasiyo ya kweli, ambapo ukweli unatuambia kinyume chake. Si lazima kuwa tajiri kufanya mema; badala yake, ukaribu kila mara ni watu wa hali ya chini ambao huchagua kutumia wakati wao, ujuzi na ukarimu kuwajali wengine. Hadithi nyingine inayohitaji kutupiliwa mbali ni kwamba Kanisa Katoliki, ambalo linajulikana ulimwenguni pote kwa kujitolea sana kwa kazi za kuhamasisha jamii, linafanya hayo yote ili kugeuza imani, kana kwamba kuwajali wengine ni njia ya kuwashawishi watu “wajiunge nalo.”  Baba Mtakatifu amebainisha “Hapana!” Kanisa haliendi mbele kwa kugeuza imani, bali linakwenda mbele kwa mvuto. Wakristo hufanya lolote wawezalo ili kupunguza mateso ya wahitaji, kwa sababu katika nafsi ya maskini wanamkiri Yesu, Mwana wa Mungu, na, ndani yake, kuna hadhi ya kila mtu, aliyeitwa kuwa mwana au binti wa Mungu. Papa Francisko kwa hiyo amependa kufikiria kuwa Nyumba hiyo ya Huruma iwe  kama mahali ambapo watu wa itikadi tofauti, na wasioamini pia, wanaweza kuungana na Wakatoliki wa mahali hapo ili kutoa msaada wa huruma kwa kaka na dada zetu wengi katika familia moja ya kibinadamu!

Papa amefanya mkitano na wahudumu wa Upendo kabla ya kurudi Roma
Papa amefanya mkitano na wahudumu wa Upendo kabla ya kurudi Roma

Kiukweli neno “huruma” linamaanisha uwezo wa kuteseka pamoja na wengine, na kwa kufaa Serikali itatafuta kuilinda na kuiendeleza. Ili ndoto hyio itimie, ni muhimu, hapo na kwingineko, kwamba wale walio katika mamlaka ya  umma waunge mkono mipango hiyo ya kibinadamu, wakihimiza harambee ya wema kwa ajili ya manufaa ya wote. Hatimaye, hadithi ya kufikirika tu ya  tatu  ambayo inahitaji kupuuzwa ni: dhana kwamba pesa pekee ndiyo huhesabika, kana kwamba njia pekee ya kuwajali wengine ni kuajiri wafanyakazi wanaolipwa mishahara na kuwekeza katika vituo vikubwa. Kwa hakika Papa amesema Upendo unadai taaluma, lakini kazi za upendo hazipaswi kugeuka kuwa biashara. Badala yake, wanapaswa kuhifadhi kwa upya wao kama kazi za upendo ambapo wale wanaohitaji wanaweza kupata watu tayari kuwasikiliza kwa huruma, bila kujali malipo yoyote wanayoweza kupokea. Kwa neno moja, kufanya wema kweli kweli, wema wa moyo ni muhimu kujitolea kutafuta kilicho bora kwa wengine. Kujitolea kwa ajili ya malipo si upendo wa kweli; kwani upendo pekee unaweza kushinda ubinafsi na kuendeleza ulimwengu huu.

Katika suala hilo, vile vile Baba Mtakatifu amependa kuhitimisha kwa historia kutoka katika maisha ya Mtakatifu Teresa wa Calcutta. Mwandishi mmoja wa habari, alipomwona ameinamia juu ya vidonda vyenye harufu mbaya ya mtu mgonjwa, mara moja alimwambia, “Unachofanya ni kizuri, lakini, mimi binafsi, singefanya hivyo hata kwa dola milioni.” Mama Teresa alijibu, “Singefanya hivyo kwa dola milioni pia. Ninafanya hivyo kwa ajili ya upendo wa Mungu!” Kwa hiyo Baba Mtakatifu ameongeza kusema: “Ninaomba kwamba aina hii ya upendo wa bure iwe thamani inayoongozwa na Nyumba ya Huruma. Kwa mema yote mliyofanya na mnayoendelea kufanya, ninatoa shukrani zangu nyingi za dhati na ninawapatia baraka zangu. Na ninawaomba, tafadhali, katika sala zenu mniombee." Papa Fracisko amehitimisha.

HOTUBA YA PAPA KWA WHUMU WA UPENDO
04 September 2023, 09:12