Papa Francisko:silaha zinyamaze Nagorno Karabakh,juhudi za amani zifanyike
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Ombi la kunyamazisha bunduki na kutafuta suluhisho za amani huko Nagorno Karabakh lilizinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 20 Septemba 2023 mwishoni mwa Katekesi yake katika uwanja wa Mtakatifu Petro, kwa waamini na mahujaji waliofika kutoka pande za dunia. Papa amesema “Jana nilipokea habari za kuhuzunisha kutoka Nagorno Karabakh, kusini mwa Caucasus, ambapo hali mbaya ya kibinadamu sasa inazidi kuwa mbaya kutokana na mapigano zaidi ya silaha. Kwa mara nyingine tena ninatoa wito kwa pande zote zinazohusika na jumuiya ya kimataifa ili basi silaha zinyamaze na kila juhudi ifanywe kutafuta suluhisho za amani kwa manufaa ya watu na heshima ya utu wa binadamu”.
Operesheni ya kijeshi
Azerbaijan ilianza operesheni ya kijeshi huko Caucasus Kusini mnamo 19 Septemba 2023. Wizara ya Ulinzi ya Azerbaijan ilitangaza operesheni hiyo ya kijeshi ikiitaja kuwa ni hatua ya ‘kupambana na ugaidi dhidi ya mashambulizi ya mara kwa mara ya vikosi vya Armenia na baada ya baadhi ya raia na polisi wa Azeri kufariki katika siku za hivi karibuni kutokana na mlipuko wa mgodi. Kwa mujibu wa vyombo kadhaa vya habari, jeshi la Azerbaijan tayari limeshambulia kwa mabomu Stepanakert, jiji kuu la Caucasus Kusini chini ya udhibiti wa Armenia, na maeneo mengine ya Armenia. Mamlaka ya Armenia ilizungumza kuhusu waathrika wawili wa raia, akiwemo mtoto, na watu 23 waliojeruhiwa, huku mamlaka ya Azerbaijan ikiripoti kifo cha raia mmoja huko Shusha, jiji muhimu katika eneo hilo, kufuatia shambulio la mizinga.
Ombi la Umoja wa Mataifa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa wito wa kukomeshwa mara moja kwa mapigano, kupunguza kasi na uzingatiaji mkali wa usitishaji vita wa 2020 na kanuni za sheria za kimataifa za kibinadamu. Hii iliripotiwa na msemaji wake, Stéphane Dujarric, akiongeza kuwa katibu wa Umoja wa Mataifa ana wasiwasi mkubwa kuhusu matumizi ya nguvu za kijeshi katika kanda na kuhusu ripoti za waathirika, ikiwa ni pamoja na miongoni mwa raia.
Maombi kwa ajili ya Ukraine
Hata baada ya katekesi yake Papa ameota ombi kwa ajili ya Ukraine ambapo ni karibu miezi 19 baada ya kuanza kwa vita. “Tunabaki kuwa wamoja katika ukaribu na sala kwa ajili ya Ukraine na wapendwa na wanaoteswa”, ni maneno yaliyotamkwa na Papa Francisko katika salamu zake kwa waamini wanaozungumza Kiitaliano.
Mashahidi wa Korea
Mfano unaofafanuliwa kama shujaa, unaoweza kuwa chanzo cha usaidizi kwa kila mtu katika kufanya chaguzi zenye changamoto"na uwezo wa kutoa faraja katika nyakati ngumu. Kwa maneno haya, tena mwishoni wa katekesi, Papa alizungumza juu ya Mtakatifu Andrew Kim, Paul Chông na mashahidi wenzake wa Korea ambao kumbukumbu zao Kanisa linaadhimisha kila ifikaèo tarehe 20 Septemba. Jumamosi tarehe 16 Septemba 2023, alasiri, sanamu ya Mtakatifu Andrew Kim Taegon, padre wa kwanza wa Korea na mfia dinin ilisimikwa kwenye moja ya eneo la Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, baada ya kubarikiwa na Kardinali Mauro Gambetti, kuhani mkuu wa Kanisa Kuu hilo. Ujumbe wa wamini zaidi ya 300 wa Kanisa la Korea, wakiwemo maaskofu, mapadre, watawa kike na kiume na walei, walishiriki katika uzinduzi huo, baada ya kupokelewa na Baba Mtakatifu masaa kadhaa kwa siku hiyo.