Papa asikiliza ushuhuda wa wamisionari wa Kanisa la Mongolia!
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Jumuiya ndogo ya Wakatoliki nchini Mongolia imemkumbatia Papa Francisko, Jumamosi tarehe 2 Septemba 2023. Huu ulikuwa ni Mkutano wa Papa na maaskofu, mapadre, wamisionari, watu waliowekwa wakfu na wahudumu wa kichungaji katika Kanisa kuu la Watakatifu Petro na Paulo huko Ulaanbaatar, fursa iliyopambwa kwa nyimbo na ushuhuda, katika muundo ambao unakumbusha geri ambayo ni nyumba ya jadi, makao ya kawaida ya wahamaji wa Kimongolia.
Kabla ya hotuba yake Papa, rais wa Baraza la Maaskofu wa Asia ya Kati, Askofu José Luis Mumbiela Sierra alichukua nafasi kwa niaba ya wote kutoa shukrani kwa Papa kwamba “Asante kwa kuja nyumbani kwetu, kwa geri zetu. Katika siku hizi, uwepo wa mrithi wa mtume Petro kati yetu ni ushuhuda hai na wa furaha ambao unahalalisha tumaini la karne nyingi.” Tukikumbuka basi kwamba huko Mongolia karibu wamisionari wote wametoka nchi na mabara mengine, Askofu José Luis Mumbiela Sierra alisisitiza kwamba: “Kanisa linaunda udugu na kwamba katika Kanisa Katoliki hakuna mtu mgeni.
Malezi ya watoto wenye ulemavu wa mwili na akili, msaada kwa wagonjwa na wazee waliotelekezwa na familia zao, mapokezi ya watu wasio na makazi, riziki ya wale ambao hawana chakula cha kula na msaada kwa familia masikini na watu waliotengwa, hizo ndizo huduma za Injili, inayotolewa kila siku na Wamisionari wa Upendo huko Mongolia( Wa mama Teresa wa Kalcuta. Hii ilikumbukwa na Sista Salvia Mary Vandanakara.
Katika maelezo yake Sr. Salvia Mary alisimulia kwamba alifika Mongolia mnamo mwaka wa 1998, wakati Kanisa lilikuwa limeanza kukita mizizi yake. Kwa kujitolea kuwahudumia maskini zaidi walihisi kwamba wao pia walipaswa kuishi kati yao na kupata baadhi ya matatizo waliyokumbana nayo, kama vile ukosefu wa maji na mahitaji mengine ya kimsingi.
Ushuhuda mwingine uliosikika katika wakati wa mkutano wa Papa na Kanisa la mahalia ni ule wa Rufina Chamingerel, mhudumu wa kichungaji. Kwa mujibu wake alisema: Sikukulia katika familia ya Kikatoliki lakini nilikuwa mmoja wapo nilipokuwa mwanafunzi. Mara moja nilienda kumtembelea babu yangu. Usiku kucha nilizungumza kuhusu maisha ya Yesu, tangu kuzaliwa kwake hadi kufufuka kwake.” Shauku hiyo iligeuka kuwa jukumu muhimu, la kwenda kusoma Roma na kurudi Mongolia kusaidia Kanisa la Kimongolia kukua. Tuna bahati sana kwa kuwa hatuna vitabu vingi vya katekesi katika lugha yetu lakini tuna wamisionari wengi ambao ni vitabu vilivyo hai, alikiri Rufina Chamingerel.