Papa atembelea Utume wa Upendo wa Kimisionari:udugu ni unabii
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kwa tabasamu alikuwa akizungumza na kundi alilokutana nao kuwa Kupeana mikono ni ishara ya udugu na kuishi kama ndugu ni unabii. Hii ilikuwa katika siku ya pili ya Papa akiwa Marsiglia tarehe 23 Septemba 2023 iliyofunguliwa kwa mkutano wa faragha na baadhi ya watu walio katika hali ngumu ya kiuchumi na inayofanyika kwenye Nyumba ya Wamisionari wa Upendo, watawa wa Mama Teresa wa Calcutta, huko Mtakatifu Mauront, moja ya vitongoji kati ya watu maskini zaidi nchini Ufaransa.
Papa Francisko bila hotuba iliyotarishwa alisema: "Asante kwa makaribisho yenu, kwani sisi sote ni ndugu, hii ni muhimu: udugu. Mara nyingi ustaarabu wetu unatuongoza kuishi kama maadui au wageni. Ishara ya kinabii ni kuishi kama ndugu na huu ni unabii!, ule wa udugu unaokwenda zaidi wa mawazo ya kisiasa na kidini,” alisema Papa Francisko. Kwa hiyo salamu za Papa zilikuwa ni shukrani kubwa kwa watawa hao kwamba: “Asante kwa ushuhuda wenu ambao mmeniambia, nami nimefurahi kuwa nanyi hapa.” Alisema hayo mara baada ya Msimamizi wa watawa na wageni kuzungumza.
Kwa upande wa Sr Crosvita alimmsimulia Papa kwa hisia kali kwamba kwa miaka miwili akiwa Marsiglia yeye na Masista wenzake wamekuwa wakiendesha jiko la kupika supu kwa ajili ya maskini, ambalo linakaribisha watu 50 kwa wakati mmoja, mara 3-4 kwa siku, kuanzia saa 3. 30 hadi 5.30 na katika siku moja inaweza kuwafikia watu 250.
Hawa ni maskini alieleza mtawa huyo kuwa wengine wanaishi mitaani, hivi karibuni kuna kundi la watu wamefika kutoka Sudan, hawana pa kukaa, wanalala mitaani. Halafu pia kuna watu ambao wakipata sehemu ya kulala hawana chakula kwa jiyo tunawakuta hapa kuanzia asubuhi na mapema."