Papa,huko Marsiglia:Tunahitaji makaribisho ya haki kulingana na uwezekano
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Mediterania ni kioo cha ulimwengu na hubeba ndani yake wito wa kimataifa kwa ajili ya udugu, njia pekee ya kuzuia na kushinda migogoro. Maneno haya yalikuwa miongoni mwa mambo muhimu sana katika hotuba ndefu ya Baba Mtakatifu FrancisKO Jumamosi tarehe 23 Septemba 2023 kwenye kikao cha kufunga Mikutano ya Juma zima ya Mediterania kwenye Jumba la Pharoh huko (Marsiglia), ambako kilihudhuriwa hata na Rais wa Ufaransa, Bwana Emmanuel Macron. Kwa muda wa siku saba, zaidi ya wawakilishi 120 wa Makanisa na vijana kutoka Pwani tano za Bahari ya Mediterania walishiriki changamoto za sasa za kisiasa, kiuchumi na mazingira ya eneo hilo lakini pia matumaini yao ya siku zijazo, kwa kuzingatia zaidi juu ya mgogoro wa uhamiaji wa sasa. Akikumbuka tabia ya kipekee ya ulimwengu ya Marsiglia, wimbi la watu ambalo limeufanya mji huo kuwa muundo mzuri wa matumaini na utamaduni wake mkubwa wa makabila na tamaduni nyingi, inayoakisi ustaarabu mwingi wa Mediterania, Papa Francisko alielezea tafakari yake kwa mambo matatu muhimu ambayo yanaashiria mji wa kusini mwa Ufaransa yakiwa ni bahari, bandari na mnara wa taa.
Papa alibainisha kwamba kuingiliana kwa migogoro kati ya ustaarabu, dini na maono mbalimbali katika eneo tunalosikia sana leo lazima kusahau kwamba kile ambacho Warumi walikuwa wakiita mare nostrum (bahari yetu) ambayo imekuwa kwa milenia mahali pa kukutana, miongoni mwa dini za Ibrahimu; kati ya mawazo ya Kigiriki, Kilatini na Kiarabu; kati ya sayansi, falsafa na sheria; na miongoni mwa mambo mengine mengi ya kweli. Kwa hakika, Papa Francisko alisema, huku akirejea maneno ya aliyekuwa Meya wa Mji wa Firenze Italia Giorgio La Pira, ambaye aliongoza mpango wa Mikutano ya Mediterania, kwamba Mediterania ni mwanzo na msingi wa amani kati ya mataifa yote ya dunia mkusanyiko wa watu, imani na tamaduni, sawa na Bahari ya Galilaya ambapo Yesu alitangaza Heri za Mlimani.” Njia hii ya Kaskazini na Kusini, Mashariki na Magharibi, Papa alisema,kuwa inatuhimiza kupinga mgawanyiko wa migogoro na kuwepo kwa tofauti na wakati huo huo huleta pamoja changamoto za dunia nzima leo hii, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya tabianchi. Katikati ya bahari ya leo hii ya migogoro,tuko hapa kuimarisha mchango wa Mediterania, ili iweze kurejea kuwa maabara ya amani. Kwa maana hiyo ndio wito wake, kuwa mahali ambapo nchi tofauti na hali halisi zinaweza kukutana kwa misingi ya ubinadamu tunaoshiriki sote, na sio kwa msingi wa itikadi tofauti,Papa alikazia.
Papa Francisko alisema ili Bahari ya Mediterania irudi kuwa maabara ya amani ulimwenguni, katikati ya bahari ya leo ya migogoro na utaifa wenye ugomvi unaofufuka, ni lazima isikilize kilio cha maskini, kama Yesu alivyofanya kwenye ukingo wa Bahari ya Galilaya. Tunahitaji kuanza tena kutoka hapo, kutoka katika kilio cha kimya cha mara kwa mara cha aliye mdogo kati yetu ambao sio namba bali nyuso, Papa alisisitiza. Kwa njia hiyo alibainisha kwamba bahari ya kuishi pamoja wanadamu imechafuliwa na ukosefu wa utulivu hata katika miji ya Ulaya kama Marsiglia, inayokabiliwa na mivutano ya jumuiya na uhalifu unaoongezeka, kwa hiyo Papa alisisitiza juu ya haja ya haraka ya mshikamano zaidi hata kuzuia uasi. Kiukweli uovu halisi wa kijamii sio kwa kuongezeka kwa shida tu, lakini hata kupungua kwa utunzaji kwa walio hatarini zaidi kama vile vijana ambao ni mawindo rahisi ya uhalifu, familia zinazoogopa, wazee, watoto ambao hawajazaliwa, watu wanaovumilia vurugu na ukosefu wa haki katika bara la Afrika na Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na Wakristo wanaokimbia mateso, na wahamiaji kupoteza maisha wakati wanajaribu kuvuka nostrum ya mare, yaani bahari yetu ambayo imekuwa mare mortuum, yaani bahari ya wafu yenye makaburi ya bahari bila kuzikwa kwa heshima.
Akitafakari kipengele cha pili kuhusu Marsiglia, mji mkubwa wa bandari ulio wazi kwa bahari na historia ya uhamiaji na wakimbizi, Baba Mtakatifu alipinga ukweli kwamba miji mingine kadhaa ya Mediterania imefunga bandari zao ili kuzima hofu ya uvamizi unaodhaniwa wa wahamiaji. Lakini Papa ameeleza kuwa wale wanaohatarisha maisha yao baharini hawavamii, bali wao watafuta kukaribishwa. Kwa hiyo kuhusu dharura ambayo wengi wanazungumzia, alisema kwamba jambo la uhamiaji sio dharura ya muda mfupi, na daima ni nzuri kwa kuchochea propaganda za kutisha, lakini ukweli wa nyakati zetu, mchakato unaohusisha mabara matatu karibu na Mediterania na hilo lazima litawaliwe kwa busara ya kuona mbele. Katika hilo Papa alikazia kusema Mediterania inaakisi ulimwengu, na nchi maskini zaidi za Kusini mwa dunia zinazoathirika na ukosefu wa utulivu, utawala, vita na jangwa zikigeukia Kaskazini kuwa tajiri zaidi. Tena, tatizo la kuongezeka kwa tofauti kati ya walio nacho na wasio nacho amesema sio suala geni, kama Kanisa limekuwa likisema kwa miongo kadhaa, na amebainisha hayo akinukuu Waraka wa Mtakatifu Papa Paulo VI wa ?Populorum Progressio".
Suala jingine katika hotuba hiyo, amesema matatizo yanayohusika katika kukaribisha, kulinda, kuhamasisha na kuunganisha watu wasiotazamiwa. Hata hivyo, aliongeza, kusema kigezo kikubwu hakiwezi kuwa kuhifadhi hali njema ya mtu mwenyewe, bali ni kulinda heshima ya kibinadamu. Alikariri kwamba katika kukabiliana na janga la unyonyaji wa wanadamu, suluhisho sio kukataa bali ni kuhakikisha, kulingana na uwezekano wa kila mmoja, idadi kubwa ya viingilio vya kisheria na vya kawaida vya wahamiaji, kwa kushirikiana na wao na katika nchi za asili. Papa kwa njia hiyo alisisitiza zaidi umuhimu wa ushirikiano katika nchi mwenyeji, ambayo alionya, kuwa haimaanishi kuiga, kwani mtazamo ambao hauzingatii tofauti na unabaki kuwa thabiti katika dhana zake mwenyewe hufanya mawazo tu kushinda ukweli na kuhatarisha siku zijazo, katika kuongeza umbali na kuchochea kutengwa, ambapo kwa upande wake inazua uhasama na aina nyingine za kutovumilia.
Akikumbuka kwamba bandari ya Marsiglia pia ni mlango wa imani, Baba Mtakatifu Francisko aliendelea kuashiria wajibu wa Wakristo kushuhudia upendeleo wa Bwana kwa maskini na Injili ya upendo na udugu. Tumeitwa kutoa ushuhuda, sio kupamba Injili kwa maneno, bali kuipatia mwili, alisisitiza akitoa mfano wa Mtakatifu Charles de Foucauld, ndugu wa ulimwengu wote, wa mashahidi saba wa Tibhirine huko nchini Algeria, lakini pia ya wale mawakala wote wa upendo katika siku zetu. Alikumbusha maneno yake mtakatifu huyo yasemayo: “Mwabudu Mungu na umtumikie jirani yako, hilo ndilo jambo la maana.” Na akirejea juu ya picha ya mwisho ya mnara wa taa, Papa Francisko alisisitiza haja ya Makanisa ya Mediterania kutafuta njia za ushirika mbele ili kukabiliana na changamoto za eneo hilo. Katika suala hilo alipendekeza kuzingatia pia umuhimu wa Baaraza la Maaskofu wa Mediterania ambalo linaweza kutoa uwezekano mkubwa wa mazungumzo na uwakilishi wa kikanda, na kufanyia kazi mpango maalum wa kichungaji juu ya suala la uhamiaji ili majimbo yaliyo karibu zaidi yanaweza kutoa usaidizi bora wa kiroho na wa kibinadamu kwa wahamiaji wanaohitaji.
Papa hata hivyo hakusahau jukumu la vijana kama nuru inayoonesha njia ya wakati ujao katika Mediterania, huku akisisitiza tena umuhimu wa elimu kusaidia kushinda vikwazo na kushinda mawazo potofu. Papa alisisitiza hasa kuhusu vyuo vikuu kama maabara ya ndoto na katika hilo fursa kama hiyo ya mkutano vijana hukomaa kwa kukutana wao kwa wao, kufahamiana, na kugundua tamaduni na miktadha iliyo karibu na tofauti. Kwa njia hiyo ubaguzi unasambaratishwa, majeraha yanaponywa na matamshi mabaya dhidhi ya wengine yanakataliwa, alisema, na kuongeza kwamba kwa hakika Kanisa linaweza kuchangia katika hili kwa kutoa mitandao yake ya elimu na kuhimiza ubunifu wa udugu. Na hatimaye Baba Mtakatifu Francisko katika Hotuba yake ndefu alitoa wito kuwa na Taalumungu ya Mediterania yenye uwezo wa kuendeleza njia za kufikiri zilizokita mizizi katika ukweli na katika maisha halisi. Maabara haifanyi kazi na kwa hiyo alihimiza kila mtu kuunganisha vizazi kuanzia na kumbukumbu na siku zijazo, na kuhamasisha kwa uhalisi safari ya kiekumeni ya Wakristo na mazungumzo kati ya waamini wa dini tofauti ili kuzuia vurugu na nguvu zote matumizi mabaya ya dini.
Baba Mtakatifu akitoa salamu kwa Rais Emmanuel Macron wa Jamhuri ya Ufaransa aliyekuwapo alihitimisha hotuba yake kwa kutoa wito kwa eneo bora la Mediterania kuwa: Ndugu wapendwa ninawashukuru kwa uvumilivu wenu wa kunisikiliza na kwa juhudi zenu zote. Endeleeni na kazi yenu nzuri! Iwe ni bahari ya wema, ili kukabiliana na umaskini wa leo hii katika mshikamano na ushirikiano; iwe bandari ya kukaribisha, ili kuwakumbatia wale wote wanaotafuta maisha bora ya baadaye; Iwe mnara wa amani, ili kutoboa, kupitia utamaduni wa kukutana, dimbwi la giza la vurugu na vita. Asante.”