Papa Francisko:Upendo wa Mungu hauna mipaka
Na Angella Rwezaula; - Vatican.
Katika uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican ukiwa umejaa waamini na mahujaji kutoka pande za dunia, Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 24 Septemba 2023, siku moja baada ya kurudi kutoka hija ya 44 ya kitume huko Marsiglia Kusini mwa Ufaransa hakukosa kutoa tafakari yake kutoka kifungu cha Injili ya Dominika ya 25 ya Mwaka A wa Kanisa. Baba Mtakatifu akianza alisema: “Injili ya leo inatuletea mfano wa kustaajabisha: bwana wa shamba la mizabibu alitoka alfajiri mapema, hata jioni kuwaita watenda kazi, lakini mwishowe anawalipa kila mtu sawa sawa, hata wale waliofanya kazi kwa saa moja tu (rej. Mt 20, 1-16). Inaweza kuonekana kuwa ni dhuluma, lakini mfano huo haupaswi kueleweka kupitia vigezo vya mshahara; badala yake, unakusudia kutuonesha vigezo vya Mungu, asiyehesabu sifa zetu, bali anatupenda kama watoto. Hebu tutazame kwa karibu zaidi matendo mawili ya kimungu yanayotoka kwenye simulizi hii. Kwanza, Mungu anatoka nje saa zote kutuita; pili, anamlipa kila mtu kwa sarafu sawa.”
Baba Mtakatifu Francisko akiendelea kwa hiyo kufafanua tendo la kwanza amesema: Mungu ndiye atokaye saa zote kutuita. Mfano huo unasema kwamba bwana alitoka asubuhi na mapema ili kuajiri vibarua kwa ajili ya shamba lake la mizabibu, lakini kisha anaendelea kutoka nyakati mbalimbali za mchana hadi jua linapotua, ili kuwatafuta wale ambao bado hapakuwa na mtu aliyewaajiri kuwapelekwa kazini. Kwa hivyo tunaelewa kwamba katika mfano huo watenda kazi si wanadamu tu, bali zaidi ya yote ni Mungu ambaye hutoka nje siku nzima bila kuchoka.
Baba Mtakatifu ameongeza: “Hivyo ndivyo Mungu alivyo: Hataki juhudi zetu zitufikie, Hafanyi uchunguzi wa kutathmini sifa zetu kabla ya kututafuta, hakati tamaa tukichelewa kumjibu; kinyume chake, Yeye mwenyewe alichukua hatua na katika Yesu “alitoka” ili kutuonesha upendo wake.” Naye hututafuta saa zote za mchana, ambazo, kama Mtakatifu Gregori Mkuu anavyosema, zinawakilisha hatua na majira mbalimbali ya maisha yetu hadi uzee. Kwa kusisitiza zaidi Papa amesema: “kwa moyo Wake, hujachelewa; Daima anatutafuta na kutusubiri. Hebu tusisahau hilo kwamba Bwana daima anatutafuta na anatungoja, daima!”
Kwa uhakika ni kwa sababu Yeye Mungu ni mwenye moyo mkuu. Na ndiyo hatua ya pili ambayo Mungu hulipa kila mtu kwa sarafu sawa, yaani upendo wake. Hapa kuna maana kuu ya mfano huo, Papa amekazia, kwa sababu watenda kazi wa saa ya mwisho wanalipwa kama wa kwanza kutokana na ukweli kwamba Mungu ana haki iliyo kuu. Inakwenda zaidi. Haki ya binadamu inasema: “tumpe kila mtu nafsi yake kama inavyomstahili”, wakati haki ya Mungu haipimi upendo kwa mizani ya marejesho yetu, utendaji wetu au kushindwa kwetu lakini Mungu anatupenda tu, anatupenda kwa sababu sisi ni watoto wake na anafanya hivyo kwa upendo usio na masharti, upendo unaotolewa bure.
Wakati mwingine tunahatarisha kuwa na uhusiano wa ‘kibiashara’ na Mungu, Papa amesisitiza na kwamba tukizingatia zaidi uwezo wetu kuliko ukarimu wa neema yake. Wakati mwingine hata kama Kanisa, badala ya kutoka saa zote za mchana na kunyoosha mikono yetu kwa wote, tunaweza kujisikia kama wa kwanza katika darasa letu, tukiwahukumu wengine walio mbali, bila kufikiria kwamba Mungu anawapenda pia kwa upendo sawa na Yeye kama alivyo kwa ajili yetu. Na hata katika mahusiano yetu ambayo ni msingi wa jamii, haki tunayofanya wakati mwingine inashindwa kutoka nje ya ngome ya hesabu, na tunajiwekea kikomo cha kutoa kulingana na kile tunachopokea, bila kuthubutu kwenda hatua ya ziada, bila kuhesabu juu ya ufanisi wa wema unaofanywa kwa uhuru na upendo unaotolewa kwa moyo mpana.
Kutokana na hilo, Papa ameomba: “Tujiulize: Je, mimi Mkristo ninajua jinsi ya kutoka kuelekea wengine? Je, mimi ni mkarimu kwa kila mtu, je, ninajua jinsi ya kutoa ufahamu huo wa ziada na msamaha, kama Yesu alivyofanya na anavyofanya kila siku pamoja nami? Mama Yetu na atusaidie kugeukia kipimo cha Mungu yaani cha upendo usio na kipimo.” Papa Francisko amehitimisha.