Sala ya Papa mbele ya Salus Populi Romani kushukuru kwa ziara yake
Vatican News
Mara baada ya kurejea kutoka Nchini Mongolia, kama kawaida yake ya hitimisho la Ziara yake ya kitume, tarehe 4 Septemba 2023, Baba Mtakatifu Francisko alikwenda katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Maria Mkuu, ambalo alitulia katika sala mbele ya Picha ya Bikira Salus populi romani, yaani Bikira Afya ya Watu wa Roma.
Kwa njia hiyo kama ilivyo desturi yake, hata kabla ya kuondoka katika hija yake ya 43 ya Kitume kimataifa ambayo ilimuona akienda katikati ya moyo wa Asia mnamo tarehe 31 Agosti 2023, alikuwa amekwenda kujikabidhi kwa Mama Maria. Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari Vatican, vimeeleza kuwa mwishoni mwa sala yake katika Kanisa Kuu la Kiroma, Papa alirejea mjini Vatican.
Hata hivyo kwa kujitoa kwake kwa Maria ambako kunatambulika, kumethibitishwa kwa mara nyingine tena katika fursa ya kipekee katika muktadha wa matukio ya kusisimua zaidi ya ziara yake huko Ulaanbataar ambapo tulimuona akimtembelea Bi Tsetsege, mama wa watoto kumi na mmoja, ambaye miaka kumi iliyopita aliokota sanamu ya Bikira kwenye shimo la takataka na sasa kwa waamini wa Mongolia anaitwa "Mama wa Mbinguni."