Hati ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu Awamu ya Kwanza Oktoba 2023
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yamenogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pia kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha. Huu ni utamaduni wa watu wa Mungu kusikilizana kwa makini! Ni kusikiliza Neno la Mungu, ili kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia na vipaumbele vya maisha ya waamini. Kusikiliza ni kujenga utamaduni wa kusali pamoja na Neno la Mungu, “Lectio Divina.” Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yamegawanywa katika awamu kuu mbili. Awamu ya kwanza ni kuanzia tarehe 4 hadi 29 Oktoba 2023 na Awamu ya Pili itaadhimishwa Mwezi Oktoba 2024. Lengo ni kuendelea kufanya mang’amuzi ya kina kuhusu dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa, chombo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa watu wa Mungu katika ujumla wao kutangaza na kushuhudia furaha na faraja ya Injili. Maadhimisho ya Sinodi ni wakati muafaka wa toba na wongofu wa ndani, kwa kuangalia matatizo, changamoto na fursa mbalimbali zinazojitokeza, ili hatimaye, kuhamasisha umoja na ushiriki wa watu wa Mungu kutoka katika ngazi mbalimbali za maisha, kama ilivyokuwa kwa Wafuasi wa Emau.
Hati ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu imegawanyika katika sehemu kuu tatu, hii ni dira na mwongozo wa Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu, Mwezi Oktoba 2024. Huu ni mwaliko kwa Mama Kanisa kujenga na kudumisha utamaduni wa kuwasikiliza watoto wake wote, tayari kujenga Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika msingi wa: Umoja, Ushiriki na Utume. Utume wa Mama Kanisa, Maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza na kwamba, waamini walei wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika masuala ya kisiasa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni “Xenofobia”; Makanisa ya Mashariki na hatimaye ni majadiliano ya kiekumene ili wote wawe wamoja. Sehemu ya Pili inazungumzia kuhusu Waamini walei na familia; wanawake, mfumo dume; Mashemasi wanawake; Ubaguzi na nyanyaso za kijinsia; Maisha ya wakfu, Mashemasi na Majiundo; Zawadi ya Useja, Dhamana na wajibu wa Askofu mahalia pamoja na kesi za nyanyaso za kijinsia. Sehemu ya Tatu inajikita katika Majiundo, Ujenzi wa utamaduni wa kusikiliza; Ndoa za mitara au upali pamoja na utamaduni wa kidigitali.
SEHEMU YA KWANZA: Kanisa limeadhimisha Sinodi ya XVI ya Maaskofu wakati ambapo dunia ilikuwa imechafuka kwa vita na kinzani mbalimbali zilizopolekea maafa makubwa kwa watu na mali zao na hivyo watu kulazimika kuyakimbia makazi yao. Kumekuwepo pia na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi na kwamba, kuna baadhi ya Mababa wa Sinodi wameshuhudia athari zake katika maisha ya watu wa Mungu. Matatizo pamoja na changamoto zote hizi zimefafanuliwa wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu na hatimaye, kutolewa muhtasari wake, utakaojadiliwa kwenye Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu mwezi Oktoba 2024. Mama Kanisa anaalikwa kujenga utamaduni wa kuwasikiliza watoto wake wote; kuwasindikiza waathirika wa nyanyaso za kijinsia; kuganga na kuponya madonda ya waathirika wa nyanyaso za kijinsia. Hii ni hija ndefu inayosimikwa katika haki na upatanisho pamoja na kubomoa mifumo na taasisi ambazo zimepelekea kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa, tayari kujikita katika toba na wongofu wa ndani, tayati kuambatana na kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Ujenzi wa dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa ni hatua ya kwanza na kwamba, hii ni dhana ambayo haijaeleweka vyema miongoni mwa watu wa Mungu kwa kudhani kwamba, Kanisa la Kisinodi linataka kuwapoka madaraka baadhi ya viongozi wa Kanisa. Lakini dhana ya Sinodi katika maisha na utume linapania kujenga Kanisa la Kisinodi linalosimikwa katika: Umoja, Ushiriki na Utume, kwa kuwashirikisha watu wote wa Mungu katika maisha na utume wa Kanisa. Mama Kanisa anatambua fika wasi wasi na changamoto za utekelezaji wa dhana ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi.
Utume wa Mama Kanisa unasimikwa katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika majadiliano ya kiekumene, kidini na kitamaduni; utume unaojikita katika wongofu wa kichungaji na kimisionari na kwamba, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, lugha inayotumika katika maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa iwe ni ile inayoeleweka kwa wengi. Waamini wawe kweli ni kielelezo makini cha mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili. Maskini, watu wasiokuwa na sauti pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wa Kanisa. Huu ni mwaliko wa kusikiliza kilio cha maskini wapya wanaozalishwa kutokana na vita na vitendo vya kigaidi bila kusahau rushwa inayokita mizizi yake katika mifumo ya kisiasa na kiuchumi. Siasa ni wito na si kila mwamini ana wito wa kuwa ni mwana siasa bora! Ikumbukwe kwamba, siasa si njia pekee inayoweza kuwahakikishia watu haki, kumbe, medani mbalimbali za maisha, ziwe ni mahali ambapo patawasaidia waamini kuweza kuyatakatifuza malimwengu, kwa kujikita katika mchakato wa kutafuta na kudumisha haki, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Mama Kanisa hana budi kujizatiti katika utoaji wa huduma katika sekta ya elimu, afya, maendeleo na ustawi wa jamii, bila ubaguzi wa aina yoyote ilwe. Sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Wakimbizi na wahamiaji ni fursa ya kutajirishana katika maisha na utume kwa Jumuiya zinazotoa hifadhi kwa watu kama hawa na kwamba, wao wanakuwa ni chachu ya mabadiliko ya kijamii. Jumuiya za waamini zijitahidi kujenga na kudumisha umoja na ushirika tayari kujikita katika mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili.
Chuki dhidi ya wageni “Xenofobia” ni ugonjwa hatari sana katika maisha mwanadamu na umeenea sehemu mbalimbali za dunia. Hiki ni kielelezo cha uchoyo na ubinafsi; na kiburi cha baadhi ya watu kujisikia kuwa ni watu wa maana zaidi kuliko wengine na mara nyingi chuki hizi zinachochewa na wanasiasa wanaotaka umaarufu usiokuwa na mvuto wala mashiko. Kumbe, Kanisa halina budi kusimama kidete kupambana na mifumo yote ya ubaguzi wa rangi na chuki baina ya wageni. Makanisa ya Mashariki yajenge uwezo wa kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji, huku wakiendelea kuulinda utambulisho wao. Mchakato wa majadiliano ya kiekumene yanakita mizizi yake katika: Uekumene wa: Damu, maisha ya kiroho, sala na huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ikumbukwe kwamba, uekumene wa utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha adili na matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ile ile wataweza kuhamasishana kutekeleza mchakato wa ujenzi wa umoja wa Wakristo na udugu kati yao.
SEHEMU YA PILI: Waamini walei na Familia. Kwa uhalisia wake, familia ni chimbuko la jamii na pia la Kanisa. Kutokana na ukweli huo, familia inatambulika kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani. Harakati zote zinazolihusu Kanisa na utume wake hazina budi kuanzia katika familia. Ndiyo kusema kwamba, utume na uinjilishaji wote huanzia katika Kanisa la nyumbni ambalo ni kitalu cha uhai na shule ya kwanza ya maisha. Familia ya Kikristu ni jumuia ya kwanza kabisa inayoitwa kueneza Injili, ikimsindikiza na kumlea mwanadamu katika hatua zote za kukua kwake ili afikie ukomavu wa kiutu na wa kikristo. Hatuwezi kutegemea kupata mafanikio katika nyanja nyingine zozote bila kuijali, kuilinda, kuitetea na kuisitawisha familia. Waamini walei ni kundi kubwa linalounda Kanisa. Hawa ndio walimu wa imani, wanataalimungu, walezi, wahamasishaji wa maisha ya kiroho; makatekesi na kwamba, hawa ni watu ambao wana mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, karama na mapaji yao yanapaswa kuoneshwa na kutambuliwa. Kwa wanawake kutopewa Daraja Takatifu la Upadre si kwamba, wamefungiwa mlango wa ushiriki wao katika maisha na utume wa Kanisa. Mchango wa wanawake unatambuliwa na Kanisa, kwani mahusiano msingi kati ya mwanaume na mwanamke yanawasaidia kukamilishana kadiri ya mpango wa Mungu. Kanisa linataka kuona ushuhuda makini unaotolewa na wanawake na wanaume, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, lakini kwa bahati mbaya, ushuhuda unaotolewa na wanawake ndani ya Kanisa haujathaminiwa sana, kutokana na mfumo dume kutawala kwa kiasi kikubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawake wanapaswa kushirikishwa kikamilifu ili waweze kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Bila mchango wa wanawake, Kanisa litapoteza nguvu yake ya kujipyaisha tena. Dhamana na utume wa wanawake ndani ya Kanisa unajidhihirisha wazi kwa njia ya Bikira Maria, Nyota ya Uinjilishaji mpya. Kumbe, Kanisa linapaswa kushikamana pamoja na “wanawake wa shoka” ambao wamejisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, wanarithisha: imani, tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii kwa watoto wao. Wanaume na wanawake, wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wapendane na kukamilishana; bila kuwadharau, kuwabeza na kuwanyanyasa wanawake.
Mashemasi wanawake: Sehemu hii imezua mjadala mkubwa na kwamba, Mama Kanisa anapaswa kutoa jibu muafaka kwa kusoma alama za nyakati. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kufanya tafiti za kitaalimungu na zile za shughuli za kichungaji mintarafu Kanisa kuwaruhusu wanawake kuhudumia kama Mashemasi. Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko aliunda Tume inayochunguza na kujadili uwezekano wa wanawake kuteuliwa kuwa Mashemasi na matokeo ya uchunguzi huu yanatarajiwa kuwasilishwa kwenye Maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, Mwezi Oktoba 2024. Ni muhimu ikiwa kama wanawake watashirikishwa katika vikao vya maamuzi, wapewe stahiki zao pamoja na kuthamini mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni changamoto pia ya kukuza na majadiliano ya kidugu na watawa mbalimbali ili kuondokana na tabia yam fumo dume unaopelekea na hata kuibua nyanyaso dhidi ya watawa. Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu, kumbe, majiundo awali na endelevu ni muhimu sana na kwamba, majiundo haya yanapaswa kukita mizizi yake katika uhalisia wa maisha kwa ajili ya ukuaji na ukomavu wa wito wa Daraja Takatifu. Mapadre wa Madhehebu ya Kilatini wanahimizwa kutunza zawadi ya Useja katika maisha na utume wao. Dhamana na utume wa Maaskofu mahalia ni tema iliyojadiliwa kwa mapana katika mchakato wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Askofu ni msimamizi na hakimu, hali ambayo wakati mwingine inagumisha maisha na utume wa Maaskofu mahalia na hivyo kujikuta wakiwa pweke. Kuna changamoto ya kushughulikia kesi za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa, dhamana inayopaswa kutekelezwa na Askofu mahalia na hivyo inakuwa ni vigumu kwa Maaskofu mahalia kutekeleza dhamana na wajibu wake kama Baba na Hakimu mwenye haki. Dhamana hii inapaswa kuangaliwa tena mintarafu Sheria na Kanuni za Kanisa Katoliki.
SEHEMU YA TATU: MAJIUNDO YA AWALI NA ENDELEVU. Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi unahitaji majiundo makini ya awali na endelevu kwa kuwasindikiza Majandokasisi na wanovisi ili waweze kukua na kukomaa katika hisia, ili hatimaye, waweze kuishi kikamilifu useja na usafi wa moyo. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kufanya utafiti na sayansi jamii ili kutoa mwelekeo sahihi. Mababa wa Sinodi wamegusia pia umuhimu wa kujikita katika majiundo makini mintarafu mahusiano, maisha katika hatari ya kifo; matatizo na changamoto zinazoibuliwa na matumizi ya teknolojia ya akili bandia: “Artificial Intelligency.” Kumbe, kuna umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili, utu wema na haki msingi za binadamu. Maendeleo makubwa ya sayansi yawe ni kwa ajili ya huduma, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Teknolojia isaidie kukuza na kudumisha huduma ya haki na amani duniani. Kanisa halina budi kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza ambao kimsingi ni kielelezo cha mawasiliano bora zaidi yanayosimikwa katika: ukweli na uwazi; imani na uaminifu. Kumbe, kusikiliza ni kati ya sifa kuu za majadiliano na mawasiliano bora yanayofumbatwa katika uvumilivu ili kugundua ukweli wa mambo katika ukuaji. Watu wa Mungu wanahitaji kusikilizwa kwa makini, kuheshimiwa na kuthaminiwa katika utu na heshima yao. Agano la ndoa, ambalo kwalo mume na mke huunda kati yao jumuiya ya ndani ya uzima na mapendo, limeanzishwa na kupewa sheria zake na Muumba. Kwa maumbile yake limepangiwa kwa ajili ya mema ya watu wa ndoa, pia kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Kati ya wabatizwa limeinuliwa na Kristo katika hadhi ya Sakramenti. Kumbe, Sakramenti ya Ndoa ni ishara ya umoja wa Kristo na Kanisa. Inawapatia watu wa ndoa neema ya kupendana kwa mapendo ambayo kwayo Kristo Yesu amelipenda Kanisa lake. Neema ya Sakramenti ya Ndoa hukamilisha mapendo ya kibinadamu ya mume na mke, huthbitisha umoja wao usiovunjika na huwatakasa katika safari ya uzima wa milele. Ndoa hutegemezwa juu ya ukubaliano wa wanaofunga ndoa, yaani juu ya nia ya kujitoa mmoja kwa mwingine na kamili, kwa lengo la kuishi agano la mapendo amani na ya uzazi. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM, limepewa jukumu la kufanya utafiti wa kina mintarafu ndoa za mitara au upali, ili kuwasindikiza watu wanaoishi katika ndoa za mitara pamoja na kuwashirikisha katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika.
Mabadiliko makubwa katika ulimwengu wa mawasiliano kwa njia ya utamaduni wa kidigitali yameonesha ile nguvu ya kujenga na kuimarisha mahusiano na mafungamano katika ushirika sanjari na majadiliano katika familia ya binadamu. Hizi ni juhudi za binadamu katika kupambana na hali na mazungira yake, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Hii ni kazi, ubunifu na usanii wa kisayansi unaobeba ndani mwake hekima ya Mungu inayowataka wanasayansi kujikita katika wongofu wa maisha ya kiroho ili vyombo hivi viweze kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara, yaani kuwaunganisha watu katika medani mbalimbali za maisha, ili kumkomboa mwanadamu. Ni jambo la busara kwa tasnia ya mawasiliano ya jamii kujikita katika unafishaji wa kanuni maadili, utu wema na ukweli unaofumbatwa katika huduma hii muhimu inayowawezesha watu kutambua maana ya maisha na kuonja upendo kwa njia mbalimbali za mawasiliano ya kijamii. Matumizi haramu ya mitandao ya kijamii yanaweza kusababisha madhara makubwa katika maisha ya watu. Kwa mfano ni ukatili na udhalilishaji wa mtandao (Cyber bullying) ambacho ni kitendo cha kutumia teknolojia kumdhulumu mtu. Ukatili huu unaweza kusababisha madhara makubwa katika afya ya akili kama kusababisha huzuni; upweke hasi, hali ya kutojiamini na hivyo kupelekea makuzi na maendeleo hafifu pamoja na kusababisha mawazo ya kutaka kujiua. Mitandao hii inaweza kusambaza habari za kughushi, unyanyasaji wa kijinsia pamoja na utumwa mamboleo. Ni jambo la dharura kwa Jumuiya ya waamini kufanya tafakari ya kina kuhusu matumizi bora ya mitandao ya kijamii kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika ukuaji: kiroho na kimwili.