Maadhimisho ya Siku ya 43 ya Chakula Duniani 16 Oktoba 2023: Maji ni Uhai, Maji ni Chakula!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Siku ya Chakula Duniani ilianza kuadhimishwa kunako mwaka 1981 kufuatia azimio namba A/RES/35/70 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililopitishwa tarehe 5 mwezi Desemba mwaka 1980. Na ilichaguliwa tarehe 16 Oktoba kwa kuwa ni tarehe ambayo mwaka 1945 lilianzishwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO, lenye Makao yake Makuu mjini Roma, nchini Italia. Maadhimisho ya Siku 43 ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2023 yananogeshwa na kauli mbiu “Maji ni uhai, Maji ni chakula. Usimwache mtu nyuma.” Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Dr. Qu Dongyu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa anakazia mambo makuu yafuatayo: mateso na mahangaiko ya watu kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha, maji kama rasilimali muhimu kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; Maji ni chakula; Umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa ili kushinda kinzani, migogoro na migawanyiko inayoikumba Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mateso na mahangaiko ya watu kutokana na baa la njaa na utapiamlo wa kutisha ni matokeo ya dhuluma na ukosefu usawa unaowaacha watu wengi wakisukumizwa kwenye lindi la umaskini wa hali na kipato, huku watu wachache ndani ya jamii wakiogolea kwenye utajiri na kwamba, watu wengi hawana uwezo wa kufikia na hatimaye kufaidika na rasilimali za dunia. Kumbe, Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2023 inayonogeshwa na kauli mbiu “Maji ni uhai, Maji ni Chakula, Usimwache mtu nnyuma” ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kupanga, kuratibu na kutekeleza vyema rasilimali maji ili iweze kukidhi mahitaji makubwa ya binadamu na hivyo kuchochea maendeleo endelevu ya binadamu, bila ya mtu awaye yote kutengwa na kuachwa nyuma.
Maji ni uhai kwa sababu ni sehemu muhimu sana ya maisha ya binadamu, lakini rasilimali hii kwa sasa inatishiwa na changamoto ya wingi na ubora wake, kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi; uharibifu mkubwa wa mifumo ya ikolojia na idadi ya watu; usimamizi holela wa rasilimali za maji, upotoshaji sanjari na uchafuzi mkubwa wa maji. Lakini suala la kupata maji safi na salama ya kunywa ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kwa sababu maji ni ya lazima kwa ajili ya uhai wa mwanadamu na pia ni sharti la utekelezaji wa haki nyingine za binadamu. Rej. Laudato si, 30. Kumbe, kuna haja ya kuwekeza katika miundombinu, mitandao ya maji taka, katika mifumo ya usafi wa mazingira pamoja na kusafisha maji machafu. Baba Mtakatifu anakazia pia umuhimu wa kukuza mifano ya kielimu na kitamaduni ambayo huongeza ufahamu katika jamii, jambo la msingi ambalo linapaswa kuheshimiwa na kuhifadhiwa na kamwe maji hayapaswi kugeuzwa na kuwa kama bidhaa ya kubadilishana! Majini muhimu katika mchakato wa kufikia uhakika wa usalama wa chakula na ni sehemu muhimu sana kwa kilimo. Ni vyema kukuza mipango thabiti katika kilimo cha umwagiliaji ili kuepuka kutumia dawa zinazochafua mazingira; uhaba wa maji usiwe ni sababu ya migorogoro na kinzani za kijamii na kwamba, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yasaidie kuweka uwiano endelevu kati ya matumizi na rasilimali zilizopo ili kuepuka athari mbaya kwa mifumo ya ikolojia na uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Ni katika muktadha huu, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuunganisha nguvu ili kuhakikisha kwamba, maji yanakuwa ni urithi wa kila mtu, yasambazwe na kusimamiwa vyema kwa njia inayofaa.
Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani iwe ni fursa ya kupambana, ili hatimaye, kufutilia mbali utamaduni wa kutupa, kwa kujikita katika ushirikiano na mshikamano, uwajibikaji na uaminifu wa kila mtu. Mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa ni muhimu sana, ili kutenda kwa haki kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika uhai wa binadamu. Leo hii kuna kashfa ya mahusiano ya Jumuiya ya Kimataifa kutokana na migogoro na kinzani mbalimbali. Rasilimali kubwa za kifedha na teknolojia bunifu ambazo zingeweza kutumika kufanya maji kuwa ni chanzo cha uhai, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu zinaelekezwa kwenye uzalishaji na biashara ya silaha hali inayopelekea uwepo wa kinzani na wajenzi wa amani duniani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa kwa upande wake litaendelea kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba linasaidia kujenga na kudumisha utamaduni wa upendo, heshima, umoja na mshikamano, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii, hasa wenye njaa na kiu! Mwishoni Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Dr. Qu Dongyu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2023, anapenda kuishukuru FAO kwa kujitahidi kukuza maendeleo ya kilimo, lishe bora na ya kutosha kwa kila mtu sanjari na matumizi endelevu ya maji. Baba Mtakatifu anawaombea heri na baraka wale wote wanaoendelea kupigania ulimwengu bora na wa kidugu!