Tafuta

Makardinali watano wamemwandikia Waraka Baba Mtakatifu Francisko kuelezea wasi wasi wao kuhusu masuala makuu matano huku wakiomba ufafanuzi wa kina kuhusu masuala hayo. Makardinali watano wamemwandikia Waraka Baba Mtakatifu Francisko kuelezea wasi wasi wao kuhusu masuala makuu matano huku wakiomba ufafanuzi wa kina kuhusu masuala hayo.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Majibu ya Papa Francisko Kwa "Dubia" ya Makardinali Watano: Msimamo wa Kanisa

Makardinali watano wamemwandikia Waraka Papa kuelezea wasi wasi wao kuhusu: Ufunuo wa Kimungu, juu ya baraka kwa ndoa za watu wa jinsia moja; Kuhusu Sinodi kama mwelekeo wa Kisheria wa Kanisa; Juu ya Upadrisho wa wanawake ndani ya Kanisa Katoliki na juu ya Toba kama sharti la lazima kwa ajili ya msamaha unaotolewa kwenye Sakramenti ya Upatanisho. Baba Mtakatifu amewajibu na kuonesha msimamo wa Kanisa kuhusiana na mashaka yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Walter Brandmüller, Kardinali Raymond Leo Burke, Kardinali Juan Sandoval Iñiguez, Kardinali Robert Sarah pamoja na Kardinali Joseph Zen Ze-kiun wamemwandikia Waraka Baba Mtakatifu Francisko kuelezea wasi wasi wao kuhusu masuala makuu matano huku wakiomba tafsiri kuhusiana na: Ufunuo wa Kimungu, juu ya baraka kwa ndoa za watu wa jinsia moja;  Kuhusu Sinodi kama mwelekeo wa Kisheria wa Kanisa;  Juu ya Upadrisho wa wanawake ndani ya Kanisa Katoliki na juu ya Toba kama sharti la lazima kwa ajili ya msamaha unaotolewa kwenye Sakramenti ya Upatanisho. Maswali ya Makardinali hawa, yaliandikwa tarehe 11 Julai 2023 na kutumwa kwa Baba Mtakatifu tarehe 21 Agosti 2023 na Baba Mtakatifu akajibu “Responsa Dubia” na kuchapishwa kwenye wavuti ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa tarehe 2 Oktoba 2023, siku chache tu kabla ya kufungua Maadhimisho ya Sinodi ya Kumi na Sita ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Mashaka kuhusu kutafasiri Ufunuo wa Kimungu mintarafu mabadiliko ya kitamaduni na maono ya watu.

Kufasiri Maandiko Matakatifu ni kazi ya Kanisa
Kufasiri Maandiko Matakatifu ni kazi ya Kanisa

Baba Mtakatifu anasema kuna haja ya kutambua maana inayokusudiwa kuhusu “Ufafanuzi.” Ni wajibu wa wafafanuzi kusaidia, kadiri ya mwongozo huu, kuelewa na kufasiri kwa undani zaidi maana ya Maandiko Matakatifu ili, kwa chunguzi zilizo za namna ya matayarisho, uamuzi wa Kanisa uthibitike. Kwa kweli hayo yote yanayohusu jinsi ya kufasiri Maandiko Matakatifu yapo chini ya uamuzi wa Kanisa, ambaye hutimiza amri ya Mungu na huduma yake ya kuhifadhi na kulifafanua Neno la Mungu. Rej. Dei verbum 12. Mama Kanisa lazima atoe mang’amuzi ya mambo makuu kwa ajili ya wokovu wa roho za watu. Kwa wale wanaotamani aina moja ya mkusanyiko wa mafundisho yanayofanana na yanayofuatwa na wote bila kuruhusu mwanya kwa ajili ya tofauti ndogo ndogo, hili litaonekana kama vile jambo lisilotakiwa na linalochanganya. Lakini kwa kweli tofauti ya namna hii inasaidia kuweka wazi na kuendeleza sehemu mbalimbali za utajiri wa Injili usioweza kwisha. Rej. Evangelii gaudium, 40.

Ndoa ya Kikristo inaundwa na mwanaume na mwanamke.
Ndoa ya Kikristo inaundwa na mwanaume na mwanamke.

Pili ni Mashaka Kuhusu baraka za ndoa ya watu wa jinsia moja na hapa Baba Mtakatifu anasema, Ndoa ya Kikristo kama sura inayoakisi muungano kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake, inatekelezwa kwa utimilifu katika muungano kati ya mwanaume na mwanamke wanaojitoa mmoja kwa mwenziye kwa upendo ulio huru, wenye uaminifu na wa kipekee, ambamo kila mmoja anakuwa ni mali ya mwenzake hadi kufa, na wanakuwa radhi kuendeleza uzao, tena wamewekwa wakfu kwa Sakramenti inayowaletea neema ya kuwa Kanisa la nyumbani na kuwa chachu ya maisha mapya kwa jamii. Hi indio maana ya Ndoa ya Kikristo na wala si vinginevyo! Rej Amoris laetitia 292. Pamoja na msimamo huu wa Kanisa, lakini pia upendo wa kichungaji unapaswa kuoneshwa kwa kujikita katika: uelewa, uvumilivu, huruma na ujasiri bila kuwahukumu waamini wengine kuwa ni wadhambi!

Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ni hitaji muhimu la nyakati hizi
Ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ni hitaji muhimu la nyakati hizi

Tatu ni Mashaka Kuhusu Sinodi kama mwelekeo wa kisheria wa Kanisa, Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa maana Papa kwa nguvu ya wadhifa wake kama Wakili wa Kristo na Mchungaji wa Kanisa lote, ana mamlaka katika Kanisa, iliyo kamili, ya juu kabisa na iwahusuyo wote, ambayo anaweza kuyatimiza kwa uhuru. Urika wa Maaskofu ni urithi wa Urika wa Mitume katika kufundisha na katika uongozi wa kichungaji; na ndani yake umoja wa Mitume huendelezwa katika nyakati. Huu ni mwaliko kwa Maaskofu kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi kama sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa sababu Kanisa ni Fumbo la ushirika wa kimisionari unaowataka hata waamini walei kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Kuna Ukuhani wa waamini wote na ukuhani wa daraja.
Kuna Ukuhani wa waamini wote na ukuhani wa daraja.

Nne ni Mashaka Kuhusu Upadrisho wa Wanawake ndani ya Kanisa Katoliki na Baba Mtakatifu Francisko anasema, Ukuhani wa waamini wote na ukuhani wa kidaraja au wa kihierakia, ingawa huhitilafiana kadiri ya kiini chake na siyo kadiri ya cheo tu, huelekezana kati yake kwa sababu zote mbili, na kila mmoja kwa namna yake hushiriki ukuhani mmoja wa Kristo Yesu! Tofauti kuu ni huduma na wala si utu wala utakatifu wa maisha. Kumbe, Mama Kanisa anatambua na kuthamini mchango wa wanawake katika maisha na utume wa Kanisa hata kama hawana nafasi ya kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu. Lakini kwenye Kanisa Anglikani kuna wanawake ambao wamewekwa wakfu kuwa Mapadre.

Toba ni jambo la msingi katika Sakramenti ya Upatanisho
Toba ni jambo la msingi katika Sakramenti ya Upatanisho

Tano ni Mashaka juu ya Toba kama sharti la lazima kwa ajili ya msamaha unaotolewa kwenye Sakramenti ya Upatanisho, Baba Mtakatifu anasema, toba ni jambo la msingi katika Sakramenti ya Upatanisho kwani linaonesha ile nia ya kutotenda dhambi tena na kwamba, Mapadre waungamishi ni vyombo vya huruma ya Mungu na kwa njia ya Roho Mtakatifu wanakuwa ni msaada mkubwa kwa watu wa Mungu. Kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha toba, tayari kuomba msaada wa upendo na huruma ya Mungu. Huu ni mwaliko kwa Mapadre waungamishaji kutoa kipaumbele cha ukarimu kama jibu kwa zawadi ya upendo wa Mungu unaotolewa bure bila gharama yoyote. Katika shughuli za kichungaji upendo wa Mungu usiokuwa na masharti unapaswa kutangazwa na kushuhudiwa ili kuonesha maana yake halisi. Rej. Amoris laetitia 311.

Papa Dubia
03 October 2023, 14:53