Mtakatifu Yohane Paulo II: Mfungulieni Kristo Yesu Malango ya Maisha Yenu!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume. Rej. Mt 9:9-13. Hii ni tema ya dharura na madhubuti kwa maisha ya Kikristo. Baba Mtakatifu anasema, Shauku ya Uinjilishaji: Bidii ya Kitume ya Mwamini: Wito wa Utume ni mambo muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa kwa kuwa, jumuiya ya waamini inazaliwa kwa sababu ya utume na umisionari, huku ikisukumwa na Roho Mtakatifu, waamini wanatumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Huu ndio mwelekeo na dira ya utume na maisha ya Kikristo, vinginevyo, Wakristo wanaweza kujikuta wakijitafuta wao wenyewe katika ubinafsi wao. Bila ya kuwa na shauku ya uinjilishaji, imani itadhohofu na hatimaye, kunyauka na utume ndicho kiini cha maisha ya mwamini. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano tarehe 18 Oktoba 2023 amewakumbusha waamini na watu wenye mapenzi mema kwamba, tarehe 16 Oktoba 1978 Kardinali Karol Wojtyla alichaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ujumbe wake mahususi tangu wakati ule, yaani miaka 45 iliyopita umekuwa ni Wakristo kumfungulia Kristo Yesu malango ya maisha yao. Matunda ya mwaliko huu yamesaidia kukoleza mchakato wa toba na wongofu wa ndani kwa ngazi ya mtu mmoja mmoja na jamii katika ujumla wake. Kumekuwepo na mwamko kwa baadhi ya nchi ambazo zilikuwa zimemfungia Kristo Yesu malango yake, kuanza kupokea Habari Njema ya Wokovu. Mama Kanisa anaendelea kufuata mfano wa Mtakatifu Yohane Paulo II katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Huu ni mwaliko wa kuendelea kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya unyenyekevu na upole; katika hali ya ukimya na ile ya maisha yaliyofichika na kujikita katika kutekeleza mapenzi ya Mungu. Huu ni mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kutoa kipaumbele cha pekee kwa Kristo Yesu katika hija ya maisha yao hapa duniani, kwa kujenga mahusiano na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu, tayari kumtangaza na kumshuhudia sehemu mbalimbali za dunia.
Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili alizaliwa Wadowice nchini Poland tarehe 18 Mei 1920 na kupewa jina la Karol Josef Wojtyla. Akiwa na umri wa miaka 20, alifiwa na wazazi wake pamoja na ndugu yake. Katika huzuni na upweke huu, Karol alivutwa sana na maisha na wito wa kipadre na hatimaye, akajiunga na seminari ya siri na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre, tarehe Mosi, Novemba 1946. Papa Pius XII kunako tarehe 4 Julai 1958 akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Kraków, nchini Poland. Akatekeleza dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa ari, moyo mkuu na unyenyekevu wa hali ya juu kabisa. Mtakatifu Paulo VI kunako tarehe 13 Januari 1964, akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Kraków. Tarehe 26 Juni 1967 akateuliwa na Mtakatifu Paulo VI kuwa Kardinali. Akachaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki tarehe 16 Oktoba 1978, akiwa ni Papa wa 264 kuliongoza Kanisa Katoliki. Tarehe 22 Oktoba 1978 akasimikwa na kuanza kutekeleza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ndiyo maana Kanisa linamkumbuka na kumwadhimisha kila mwaka ifikapo tarehe 22 Oktoba. Alifariki dunia tarehe 2 Aprili, 2005 na kuzikwa tarehe 8 Aprili 2005. Ilikuwa ni Mei Mosi, 2011, Baba Mtakatifu Benedikto XVI alipomtangaza kuwa Mwenyeheri mbele ya bahari ya watu waliofurika kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko akamtangaza kuwa Mtakatifu tarehe 27 Aprili 2014 sanjari na Papa Yohane XXIII, Muasisi wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua fursa hii, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II. Mwaliko wa kudumu ni kumfungulia Kristo Yesu, malango ya maisha. Mtakatifu Yohane Paulo II ameacha kumbukumbu ya kudumu katika akili na nyoyo za watu wa Mungu na kwamba, haitakuwa rahisi sana kuweza kufutika. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuiga karama na maisha ya Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, sanjari na kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kukuza ari na mwamko na huduma za kimisionari. Itakumbukwa kwamba, Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ulikuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, daima binadamu na mahitaji yake msingi, ndicho alichopenda kuona kwamba, kinavaliwa njuga na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya Tatu ya Ukristo! Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ni neema kubwa sana ambayo Mwenyezi Mungu amelijalia Kanisa lake.
Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka 45 tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipochaguliwa anasema, kwa hakika Mtakatifu Yohane Paulo II ni mtu wa Mungu aliyewasaidia wengine katika mchakato wa kuutafuta Uso wa Mungu katika maisha yao; alisimama kidete kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, akakuza na kuendeleza haki msingi za binadamu, urafiki na udugu wa kibinadamu, licha ya changamoto ya kifo iliyojitokeza tarehe 13 Mei 1981. Alikazia umuhimu wa kuheshimu dhamiri ya kiimadili, utu na heshima ya binadamu na kwamba, dhamiri ndicho kiini cha siri zaidi cha binadamu, na hekalu la Mungu. Mtakatifu Yohane Paulo II alikuwa ni mtu wa sala na mwenye Ibada kwa Bikira Maria ana daima alitamani kutenda mintarafu ukweli, haki na usawa. Naye Kardinali Grzegorz Ryś, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Łódź nchini Poland, katika mahubiri yake kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, 16 Oktoba 2023 alikazia kuhusu ushuhuda wa Injili ya huruma na upendo wa Mungu kutoka kwa Mtakatifu Yohane Paulo II na kwamba, Wakristo wote wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Mtakatifu Yohane Paulo wa II alikuwa ni chombo cha huruma na upatanisho wa Mungu, mwaliko kwa watu wa Mungu kuambata tunu hizi msingi ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, tayari kukuza misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.