Nia za Baba Mtakatifu Kwa Mwezi Novemba 2023: Sala Kwa Papa!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanabainisha kwamba, kusudi uaskofu uwe na umoja usiogawanyika, Kristo Yesu alimweka Mtakatifu Petro, juu ya mitume wengine, na katika yeye akatia chanzo na msingi unaodumu na unaoonekana wa umoja wa imani na ushirika wa Kanisa. Kwa nguvu ya Ukatoliki (Catholicitatis) huu kila sehemu huvipeleka vipaji vyake yenyewe kwa sehemu nyingine na kwa Kanisa lote, hivi kwamba sehemu zote pamoja, na kila moja pia, hukithiri kwa kushirikiana zenyewe kwa zenyewe na kufanya juhudi ili kupata ukamilifu katika umoja. Mamlaka kuu ya Kiti cha Mtakatifu Petro imepewa dhamana ya kusimamia ushirika wote wa mapendo, hulinda tofauti za haki zilizopo kwa kukazia ushirika katika mema na huduma makini kwa watu wa Mungu. Rej. Lumen gentium, 13. Urika wa Maaskofu hauwezi kuwa na mamlaka usipounganika na Baba Mtakatifu, aliye Mwandamizi wa Petro, Mtakatifu na Mtume; kwa nguvu ya wadhifa wake kama Wakili wa Kristo na Mchungaji wa Kanisa lote, ana mamlaka katika Kanisa, iliyo kamili, ya juu kabisa na iwahusuyo wote (plenam, supremama et universalem potestatem) ambayo anaweza kuyatimiza kwa uhuru. Urika wa Maaskofu ni urithi wa urika wa Mitume katika kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Rej. Lumen gentium, 22-27.
Nia za Jumla za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Novemba mwaka 2023 ni kusali kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu mwenyewe ili aweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wake barabara, huku akiendelea kuwasindikiza watu wa Mungu aliokabidhiwa, kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake unaosambazwa na Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anasema, sala za watu wa Mungu zinamtia nguvu, zinamsaidia kuwa na mang’amuzi na hivyo kulisindikiza Kanisa huku akimsikiliza Roho Mtakatifu. Kuwa Papa hakumaanishi kupoteza ubinadamu lakini badala yake, ubinadamu na utu wake, vinaendelea kukua na kukomaa na watu watakatifu wa Mungu.
Kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni mchakato unaomwezesha mtu kutambua maana ya kuwa ni mchungaji na hivyo kujifunza kuwa mpendelevu na mtu mwenye huruma zaidi, kwa kujikita katika fadhila ya uvumilivu, kama Mwenyezi Mungu alivyo mvumilivu kwa waja wake. Baba Mtakatifu anafikiri kwamba, kila Papa tangu mwanzo mwa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amehisi hofu na wasiwasi kwa kutambua kwamba, watahukumiwa vikali. Hii inatokana na ukweli kwamba, Mwenyezi Mungu atawaauliza Maaskofu kutoa hesabu ya dhati ya matendo yao. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumhukumu kwa upole. Anawaomba sala, leo hii ikiwa ni zamu yake, ili wapokee msaada wa Roho Mtakatifu na Papa anayepokea msaada huu, aweze kuwa ni mnyenyekevu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwombea ili katika utekelezaji wa utume, dhamana na wajibu wake aendelee kulisindikiza kundi alilokabidhiwa na Kristo Yesu kwa imani, daima kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwombea katika ukimya!