Tafuta

2023.09.29 Nia za Mwezi Oktoba 2023 za Papa ni kuombea Sinodi ya XVI ya Maaskofu. 2023.09.29 Nia za Mwezi Oktoba 2023 za Papa ni kuombea Sinodi ya XVI ya Maaskofu. 

Nia za Mwezi Oktoba ni kuombea Sinodi ili Roho aongoze utume wa Kanisa!

Mkutano wa XVI wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu utakaofunguliwa mjini Vatican tarehe 4 Oktoba na Siku ya 97 ya Kimisionari duniani tarehe 22 Oktoba ndiyo matukio mawili yenye uhusiano kwa sababu Sinodi ni safari ya pamoja ya watu wa Mungu, ambayo inaweza kuwa na utume tu kama upeo wake unalekezwa huko.

Na Angella Rwezaula, - Vatican

Kuombea Sinodi ambayo mada yake ni Kanisa la kisinodi, Ushirika, ushiriki na utume  ndiyo kiini cha maombi ya Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya Kanisa la Ulimwengu kwa mwezi wa Oktoba 2023. Ni mwezi ambao unajikuta ndani ya mkutano mkuu wa kawaida wa Sinodi ya Maaskofu utafanyika mjini Vatican na Siku ya 97 ya Kimisonari  Duniani itakayofanyika tarehe 22 Oktoba 2023.  Katika nia ya maombi ya sala ya kila mwezi kupitia Mtandao wa Maombi ya Papa Kimataifa  kwa njia ya video pia imeoneshwa wakati wa mkesha wa maombi ya kiekumeni katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, Jumamosi tarehe 30 Septemba 2023.

Kwa njia hiyo utume ndiyo kiini cha Kanisa kama alivyoanza Baba Mtakatifu Francisko kwa lugha ya Kihispania katika Video ikitafsiriwa kwa lugha mbali mbali za ulimwengu na kwa hiyo  na wito wa kimisionari ambao unachochea nguvu ya sinodi wakati Kanisa linapokuwa katika Sinodi. Ni jibu lake “kwa amri ya Yesu ya kutangaza Injili”. Kisha kuhusu kazi ya sinodi, Papa anabainisha: “Tuliombee Kanisa, ili likubali kusikiliza na mazungumzo kama mtindo wa maisha katika kila ngazi, likijiruhusu kuongozwa na nguvu za Roho Mtakatifu kuelekea pembezoni mwa ulimwengu.”

Tafakari ya Papa kwa Nia ya Maombi mwezi Oktoba 2023

Ujumbe kwa  njia ya video ya mwezi Oktoba, ulioundwa kwa msaada na ushirikiano wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa ya Marekani na Sekretarieti ya Sinodi, ni mwaliko wa kujiweka mbele ya Bwana katika mtazamo wa kusikiliza na mazungumzo.   Kwa hiyo wazo la Kanisa kwenye harakati na wito wake wa kimisionari, unawakilishwa katika uchaguzi wa picha, inayoelezewa, kwa namna ya sinema ya barabarani ambapo ni kupitia dirisha la gari unaweza kuona mahali na watu kutoka nchi mbalimbali kuanzia Vatican hadi Kambodia, kwenda Afrika, Mashariki ya Kati, Amerika Kaskazini ambazo zilirekodiwa katika matukio ya maisha ya kila siku.

Gari hilo linawakilisha Kanisa; mafuta yake ni nguvu ya Roho Mtakatifu, ambayo, kwa maneno ya Papa Fransisko, lazima liongoze kuelekea pembezoni mwa ulimwengu. Sinodi ina maana ya kutembea pamoja katika kusikilizana na Papa Francisko ameweka wazi kwamba usikilizaji huu hautaishia na Sinodi ya Oktoba. Katika video Papa Francisko  anawaonesha wanafunzi wa Emau kama mfano.

Ifuatayo ni tafakari nzima ya Papa Francisko iliyotafsiriwa kwa kiswahili kutoka lugha ya kihispania:

Utume ndiyo kiini cha Kanisa. Na hata zaidi wakati Kanisa liko katika Sinodi. Sinodi hii yenye nguvu pekee inaendeleza wito wake wa kimisionari, yaani, mwitikio wake kwa ajili ya Agizo la Yesu la kutangaza Injili. Ningependa kukumbusha kuwa hakuna kinachoishia hapa. Badala yake, tunaendelea na safari ya kikanisa hapa. Hii ni safari ambayo tunafanana kama wanafunzi wa Emau, wakimsikiliza Bwana ambaye daima anakuja kukutana nasi. Yeye ni Bwana wa kushangaza. Kupitia maombi na utambuzi, Roho Mtakatifu hutusaidia kutekeleza “utume wa Mungu, kuwa na sikio,” yaani, kusikiliza kwa masikio ya Mungu ili kunena kwa neno la Mungu. Na hivyo, tunakaribia moyo wa Kristo. Utume wetu na sauti inayotuvuta hutoka kwake. Sauti hii inatufunulia kwamba moyo wa utume ni kufikia kila mtu, kutafuta kila mtu, kuwakaribisha kila mtu, kuhusisha kila mtu na bila kumtenga mtu yeyote. Tuombe kwa ajili ya Kanisa, ili lipate kusikiliza na mazungumzo kama mtindo wa maisha kwa kila ngazi, likijiruhusu kuongozwa na Roho Mtakatifu kuelekea pembezoni mwa ulimwengu."

Kwa upande wa Padre Frédéric Fornos S.J., Mkurugenzi wa Kimataifa wa Mtandao wa Nia ya Maombi ya Kimataifa ya Papa anatoa maoni yake kuhusu wakati muhimu ambao Kanisa linapitia kwamba: “Katika awamu hii ya tatu ya Sinodi, Papa  Fransisko anatualika kusali ili kusikiliza na mazungumzo ni njia ya maisha katika kila ngazi ya Kanisa, kwa sababu wao ni neema. Ni kwa njia hiyo tu tunaweza kumsikiliza Roho Mtakatifu na kujiruhusu wenyewe kuongozwa naye. Roho wa Bwana ndiye anayetufungulia njia mpya. Ni yeye anayetusaidia kutambua utume wa Kristo le hii  anahitimisha Padre Fornos   na kusema kuwa na anatuongoza hadi pembezoni mwa ulimwengu. Akituhimiza, kama Baba Mtakatifu Francisko asemavyo, kumfikia kila mtu, kutafuta kila mtu, kukaribisha kila mtu, kuhusisha kila mtu, bila kumtenga mtu yeyote.

Nia za Maombi Oktoba 2023
01 October 2023, 11:38