Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana na Kanisa katika Nchi Takatifu kusali na kufunga ili kuombea amani Ukanda wa Gaza, Jumanne, tarehe 17 Oktoba 2023. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana na Kanisa katika Nchi Takatifu kusali na kufunga ili kuombea amani Ukanda wa Gaza, Jumanne, tarehe 17 Oktoba 2023.  (AFP or licensors)

Papa: Tarehe 17 Oktoba 2023 Ni Siku ya Kufunga na Kuombea Amani Ukanda wa Gaza

Baba Mtakatifu ameombea usalama na amani sehemu mbalimbali za dunia, bila kusahau Ukraine na kwamba, kusiwepo tena na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Anakiri kwamba, sala ni nguvu inayosimikwa katika: Upole, unyenyekevu na ni takatifu ya kupinga nguvu ya kishetani ya chuki, ugaidi na vita. Anawaalika waamini kuungana na Kanisa katika Nchi Takatifu kusali na kufunga ili kuombea amani Ukanda wa Gaza, Jumanne, tarehe 17 Oktoba 2023.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Uvamizi wa Kundi la Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023 umepelekea vifo vya zaidi ya watu 1,300, wakiwemo wanajeshi 247, idadi ambayo haijawahi kushuhudiwa nchini Israel kwa miongo kadhaa. Kwa upande wake, mashambulizi mfululizo ya Israel yameuwa hadi sasa zaidi ya watu 1,530 katika Ukanda wa Gaza, kwa mujibu wa takwimu ya pande zote mbili. Israel inadai kuwa wapiganaji 1,500 wa Hamas wameuawa ndani ya Israel, na kwamba mamia kati ya wale waliouawa Ukanda wa Gaza ni wananchama wa kundi hilo, ambalo linatambuliwa na mataifa kadhaa ulimwenguni kuwa kundi la kigaidi.  Pande zote mbili zina idadi kubwa zaidi ya majeruhi, huku Umoja wa Mataifa ukisema walioyakimbia makazi yao katika Ukanda wa Gaza wamefikia watu 430,000.

Tarehe 17 Oktoba 2023 ni Siku ya Kufunga na Kusali ili kuombea Amani Ukanda wa Gaza
Tarehe 17 Oktoba 2023 ni Siku ya Kufunga na Kusali ili kuombea Amani Ukanda wa Gaza

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 15 Oktoba 2023 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican amesikitishwa sana na hali ilivyo huko Ukanda wa Gaza na kwamba, waathirika wakuu ni watoto, wazee na wanawake. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kutoa mwaliko kwa pande zote mbili kuwaachilia mara moja mateka wa vita na kwamba, watoto, wagonjwa na wazee kamwe wasiwe ni chambo cha vita. Kumbe, kuna haja ya kuheshimu sheria za Jumuiya ya Kimataifa, hususan Ukanda wa Gaza ambako kuna haja ya kutoa mwanya ili shughuli za uokoaji zifanyike na msaada uendelee kutolewa kwa waathirika.

Waathirika wakuu wa vita ni watoto, wazee na wanawake
Waathirika wakuu wa vita ni watoto, wazee na wanawake

Baba Mtakatifu ameombea usalama na amani sehemu mbalimbali za dunia, bila kusahau Ukraine na kwamba, kusiwepo tena na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Anakiri kwamba, sala ni nguvu inayosimikwa katika: Upole, unyenyekevu na ni takatifu ya kupinga nguvu ya kishetani ya chuki, ugaidi na vita. Anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana na Kanisa katika Nchi Takatifu kusali na kufunga ili kuombea amani Ukanda wa Gaza, Jumanne, tarehe 17 Oktoba 2023.

Vita ina madhara makubwa kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu
Vita ina madhara makubwa kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu

Wakati huo huo, Dk. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, ametoa wito kwa Jumuiya ya Kimataifa kufungua vivuko ya Ukanda wa Ghaza na kuruhusu kuingizwa misaada mbalimbali katika eneo hilo. Ameongeza kuwa wito uliotolewa na utawala wa Israel wa kutaka kuhamishwa hospitali za Ukanda wa Ghaza kabla wanajeshi wa utawala huo kuanza mashambulizi dhidi ya eneo hilo kutasababisha vifo vya wagonjwa wengi wenye hali mahututi. Hadi sasa vituo 13 vya afya vimeshambuliwa katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza kwa mapigano na kwamba akiba ya vifaa vya matibabu imekwisha. Shirika la Afya Duniani limelitaja agizo la utawala wa Israeli kwa hospitali za kaskazini mwa Ghaza kuwa ni "hukumu ya kifo" kwa wagonjwa na majeruhi wa Palestina. Katika upande mwingine, Rais wa Mamlaka ya Ndani wa Palestina Mahmoud Abbas amesisitiza kusitishwa mashambulizi ya Israeli. Ameeleza hayo katika mazungumzo ya simu na Rais wa Marekani, Joe Biden na kusisitiza kwamba amani na usalama katika eneo la Mashariki ya Kati vinaweza tu kupatikana kupitia utekelezaji wa kile kinachojulikana kama suluhisho la serikali mbili kwa kuzingatia maazimio ya kisheria ya Kimataifa.

Amani Ukanda wa Gaza
16 October 2023, 13:57