Papa Francisko Aonesha Mshikamano na Waathirika wa Kimbunga Cha Otis Nchini Mexico
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Zaidi ya watu 43 wamepoteza maisha na wengine 36 hawajulikani mahali walipo kutokana na uharibifu mkubwa uliosababishwa na kimbunga cha Otis kilichoandamana na dhoruba kali kupiga mji wa kitalii wa Acapulco nchini Mexico, tarehe 25 Oktoba 2023. Kimbunga hiki kimesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao kiasi kwamba makazi ya watu yamebomolewa kutokana na mafuriko makubwa na hivyo kuharibu kabisa mawasiliano.
Kimbunga cha namna hii, hakijawahi kutokea nchini Mexico, isipokuwa kile kilichotokea mwaka 2015 mjini Patricia, kwenye Bahari ya Pacific. Ni katika muktadha wa maafa haya makubwa, Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 29 Oktoba 2023 ameonesha uwepo wake wa karibu kwa watu waliokumbwa na maafa haya. Amemwomba Bikira Maria wa Guadalupe kuwa karibu na kuwatia shime watoto wake wanaokabiliwa na majaribu makubwa katika historia ya maisha yao.