Tafuta

Papa Francisko tarehe 2 Oktoba 2023 amekutana na kuzungumza na wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Papa Francisko tarehe 2 Oktoba 2023 amekutana na kuzungumza na wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake.  (Vatican Media)

Papa Francisko: Moyo Mtakatifu wa Yesu ni Chemchemi ya Huruma na Upendo

Shirika la Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu mwaka 2023 wanaadhimisha Mkutano wao mkuu wa ishirini na moja unaongozwa na kauli mbiu “Yesu Anawatokea Wafuasi wa Emau.” Hii ni changamoto ya kutafakari zaidi kuhusu Moyo Mtakatifu wa Yesu, Ushirikiano wa kidugu na utangazaji wa furaha ya Injili kwa watu wote katika maisha na utume wao. Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya huruma na upendo wa kristo Yesu uliofikia kilele chake Mlimani Kalvari.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu lilianzishwa tarehe 8 Desemba 1854 na Padre Jules Chevalier, huko Issudun nchini Ufaransa. Wakati huo huo, kulianzishwa pia Shirika la Mabinti wa Moyo Mtakatifu wa Yesu pamoja na Watawa wa Moyo Mtakatifu wa Yesu bila kuwasahau Walei wa Familia ya Chevalier. Mashirika yote haya yalijikita katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu wanafahamu na hatimaye, wanaonja upendo wa Mungu. Shirika la Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu mwaka 2023 wanaadhimisha Mkutano wao mkuu wa ishirini na moja unaongozwa na kauli mbiu “Yesu Anawatokea Wafuasi wa Emau.” Rej Lk 24:13-35. Hii ni changamoto ya kuendelea kutafakari utambulisho wa karama na dhamana ya kimisionari; kwa kuhakikisha kwamba, wanazama zaidi katika: kuufahamu Moyo Mtakatifu wa Yesu; Ujumbe ushirikiano wa kidugu; mchakato wa utangazaji wa furaha ya Injili kwa watu wote katika maisha na utume wao.

Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu
Moyo Mtakatifu wa Yesu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Wamisionari hawa kuufahamu Moyo Mtakatifu wa Yesu kwa njia ya Injili, kwa kujikita katika kuitafakari, ili Kristo Yesu aendelee kuwa ni mwandani wa safari ya maisha yao ya kiroho. Injili kimsingi ni kiini cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, mwaliko kwa watu wote wa Mungu ni kuitafakari, ili hatimaye, kuwaonjesha wengine ile faraja na huruma inayobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, tayari kuwakumbatia na kuwaambata wadogo, maskini, wale wanaoteseka, wadhambi na katika mateso na mahangaiko yote ya binadamu. Ushuhuda wa Kristo Yesu kwa wafuasi wa Emau ni kielelezo cha huruma na upendo wa Kristo Yesu unaofikia kilele chake pale juu mlimani Kalvari, kwa kuchomwa moyoni kwa mkuki, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo.

Papa Francisko akutana na Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu
Papa Francisko akutana na Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kristo Yesu anaendelea kujisadaka na kujimega katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelzo cha upendo wake usiokuwa na kikomo. Bikira Maria anayeheshimika kwa kutajwa kuwa ni Bikira Maria wa Moyo Safi, aliyahifadhi yote moyoni mwake. Huu ni mwaliko wa kutafakari Injili katika ukimya! Baba Mtakatifu anawaalika Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu kuzama na kujikita katika kulifahamu Neno la Mungu na kushirikishana kidugu, kama sehemu ya ushuhuda wao wa maisha yaliyowakutanisha na Kristo Mfufuka kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau, tayari kuwa ni wadau wakuu wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, huu ni mwaliko wa kushirikishana kidugu mang’amuzi ya kukutana na Kristo Mfufuka, katika Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na maisha katika ujumla wake. Ni kwa njia hii, wataweza kukabiliana na matatizo na changamoto za maisha na utume wa kitawa. Baba Mtakatifu anawaalika na kuwahimiza Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu kutangaza furaha ya Injili kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau baada ya kukutana mubashara na Kristo Mfufuka katika medani mbalimbali za maisha.

Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu lilianzishwa mwaka 1854
Shirika la Moyo Mtakatifu wa Yesu lilianzishwa mwaka 1854

Katika maisha na utume wao kama watawa, changamoto daima zinawandama, lakini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa watu wa Mataifa, daima wakiongozwa na huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu. Malengo na mipango yao ya maisha iratibiwe na huruma kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, kama kielelezo cha ukaribu, huruma na faraja ya Mungu kwa waja wake. Yote haya yapate chimbuko lake katika sala na majadiliano na Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawataka Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha na hivyo kuondokana na huzuni moyoni, hali inayoleta karaha katika maisha ya kitawa!

Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu
02 October 2023, 14:53