Papa Francisko Tarehe 27 Oktoba 2023: Siku ya Kuombea Amani Duniani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Yohane XXIII katika Wosia wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” anasema amani inasimikwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu: utu, heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Mtakatifu Yohane wa ishirini na tatu alipoandika Waraka wake wa kichungaji, Amani Duniani, alikuwa na picha ya kinzani, migogoro na vita mara tu baada ya athari za vita kuu ya Pili ya Dunia iliyoleta maafa makubwa na mwendelezo wa vita baridi kati ya Mataifa makubwa duniani. Aliona kwamba, amani ilikuwa hatarini kutoweka na kwamba, kulikuwa kuna haja ya kujenga na kuimarisha misingi ya umoja na udugu wa kibinadamu kwa kuaminiana, sanjari na utunzaji bora wa mazingira kama sehemu ya mwendelezo wa kazi ya uumbaji. Ni katika muktadha wa ujenzi wa amani duniani, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuungana naye Ijumaa tarehe 27 Oktoba 2023 ili kufunga, kusali na kufanya toba ili kuombea amani duniani. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inasitisha vita, ili amani iweze kutawala katika akili na nyoyo za watu. Kwa hakika vita si suluhu ya matatizo na changamoto zinazomwandama mwanadamu bali ni chanzo kikuu cha maafa na umaskini. Mwaliko huu wa sala unatolewa pia kwa waamini wa Makanisa na dini mbalimbali ulimwenguni. Siku hii itahitimishwa kwa Ibada maalum ya kuombea amani duniani, majira ya Saa 12: 00 jioni kwa saa za Ulaya kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni siku maalum kwa ajili ya kuombea amani duniani, siku inayowashirikisha watu wote wa Mungu anasema Baba Mtakatifu Francisko.
Kiini cha Wosia huu wa Kitume wa Mtakatifu Yohane wa Ishirini na tatu “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” ni: maisha, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Haya ni mambo ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani na kama sehemu ya kanuni msingi katika sheria na ushirikiano wa kimataifa. Huu ndio msimamo ambao Vatican imekuwa ikiupatia msukumo wa pekee katika mikutano ya kimataifa inayojadili masuala ya haki, amani na upigaji rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za maangamizi. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kanisa Katoliki kwa upande wake, litaendelea kuhimiza umuhimu wa watu wa Mataifa kudumisha amani. Kanisa linaunga mkono Kanuni ya Sheria ya Kimataifa kuhusu Silaha za Nyuklia, ikiwa ni pamoja na Mkataba wa Kimataifa wa kupiga rufuku utengenezaji, ulimbikizaji na matumizi ya silaha za kinyuklia duniani. Amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani inatishiwa sana na mashindano ya silaha; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani!
Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani ambalo ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu! Baba Mtakatifu anasema, dunia bila kuwa na silaha za kinyuklia inawezekana kabisa na ni muhimu sana na kwamba, silaha hizi za maangamizi kamwe haziwezi kuwasaidia viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuwa na uhakika wa usalama wa raia na mali zao kitaifa na kimataifa. Kuna haja ya kufanya upembuzi yakinifu kuhusu madhara yake katika maisha ya watu sanjari na mazingira; kwa kuondoa hofu, mazingira ya kutoaminiana, chuki na uhasama vinavyozungumza “dhana ya silaha za nyuklia.” Jumuiya ya Kimataifa haina budi kujielekeza zaidi katika kubuni sera na mikakati itakayosaidia utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Mtakatifu Yohane wa Ishirini na tatu wakati anaandika Waraka huu wa kichungaji ambao unaendelea kuwa rejea katika kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na usalama wa kimataifa, aliona jinsi ambavyo dunia ilikuwa imegawanyika na kutawaliwa na vita baridi iliyokuwa inaendeshwa na Mataifa makubwa yaani: Marekani na Urusi kwa wakati huo. Kulikuwa na vitisho vya mashambulizi ya silaha za kinyuklia, jambo ambalo lilijenga hofu na mashaka makubwa miongoni mwa Jumuiya ya Kimataifa. Mtakatifu Yohane wa Ishirini na tatu akasimama kidete kuwaambia wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani duniani. Wakuu hawa wakasikia ujumbe wake, amani na utulivu vikarejea tena, ingawa vita baridi iliendelea kufuka moshi chini kwa chini! Ndiyo mchango kama huu uliotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili wakati wa uongozi wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa kukazia: ukweli, utu na heshima ya binadamu, uhuru na mshikamano wa kimataifa. Vita baridi ikafifia Mataifa yakaanza kuaminiana na kujadiliana kwa pamoja mustakabali wa Jumuiya ya Kimataifa. Lakini si nyakati zote sauti ya kinabii inayotolewa na Mama Kanisa imeweza kusikilizwa kwani, wakati mwingine wameipuuza na viongozi wakawasha moto wa vita, kiasi cha kuleta maafa makubwa.
Wosia huu wa Kitume wa Amani Duniani una utajiri mkubwa wa Maandiko Matakatifu kuhusu amani, kuwa ni zawadi kubwa ambayo Mwenyezi Mungu amempatia mwanadamu na kwamba, amani ni jina linalomwelekea Mungu mwenyewe. Amani ni neno linalowakilisha ukamilifu na lengo la maisha ya mwanadamu, kama anavyobainisha Yesu Mwenyewe kwa njia ya maisha na utume wake. Ikumbukwe kwamba, amani ni tunda la haki na mapendo. Amani ni sehemu ya mchakato wa kila siku ya maisha ya mwanadamu inayojikita katika utafutaji wa utaratibu wa muafaka kadiri ya mapenzi ya Mungu na kwamba, amani inapatikana ikiwa kila mtu atajitahidi kutekeleza wajibu wake, kwa kuzingatia: ukweli, upendo, upatanisho na sheria. Kushindwa kwa mchakato wa amani ni vita! Waraka wa Amani Duniani ni dira na mwongozo makini katika mchakato wa kujenga na kuimarisha amani duniani, hasa wakati huu wa ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hii ni changamoto ya kudumisha ushirikiano wa kimataifa unaooongozwa na kanuni ya auni kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi, kulinda na kutetea haki msingi, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Watu wana haki na wajibu wa kujenga na kuimarisha amani kwa kutoa kipaumbele cha kwanza katika haki msingi za binadamu na maendeleo endelevu yanayozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kama anavyosali Mtakatifu Francisko wa Assisi, kila mtu anapaswa kuwa kweli ni chombo cha amani. Jumuiya ya Kimataifa isimame kidete kuwalinda na kuwatetea maskini kwa kuwa kweli madaraja ya amani na wala si kinzani, migogoro na vita vinavyosababisha maafa makubwa kwa jamii. Watu wajenge na kuimarisha utamaduni wa majadiliano unaosimikwa katika ukweli, uwazi, heshima na mafao ya wengi. Viongozi wa kidini wanapaswa kuonesha utashi wa kufanya majadiliano ya kina, ili amani iweze kutawala na kudumu akili na katika nyoyo za watu.