Tafuta

Papa Francisko: Upendo kwa Mungu na Jirani Ni Sawa na Chanda na Pete

Waamini wanajifunza kuonja upendo wa Mungu, ili hatimaye, kuumwilisha katika matendo ya huruma kwani upendo wa Kristo Yesu unawabidiisha na kwamba, yote yanaanza na kupata hitimisho lake kutoka kwa Kristo Yesu anayewakutanisha na hivyo wajibu wao mkubwa ni kumfungulia Kristo Yesu mioyo kila siku ya maisha yao. Upendo kwa Mungu na jirani una maanisha kuakisi upendo wa Mungu kwa kuwapenda jirani wanaoonekana. Upendo Amri kuu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mwinjili Mathayo katika Dominika ya 30 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa anazungumzia kuhusu Amri kuu: “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.” Mt 22: 37-40. Upendo kwa Mungu na jirani ni sawa na chanda na pete, ni mambo ambayo kamwe hayapaswi kutenganishwa. Ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye anayeanza kuwapenda waja wake na kama watoto wachanga wanavyojifunza kuwapenda wazazi wao, ndivyo kwa waamini wanavyojifunza kumpenda Mungu kwa moyo wa unyenyekevu kama asemavyo Mzaburi “Hakika nimeituliza nafsi yangu, na kuinyamazisha; kama mtoto aliyeachishwa kifuani mwa mama yake; kama mtoto aliyeachishwa, ndivyo roho yangu ilivyo kwangu” Zab 131: 2.

Upendo kwa Mungu na jirani usimikwe katika uhalisia wa maisha
Upendo kwa Mungu na jirani usimikwe katika uhalisia wa maisha

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 29 Oktoba 2023. Waamini wanajifunza kuonja upendo wa Mungu, ili hatimaye, kuumwilisha katika matendo ya huruma kwani upendo wa Kristo Yesu unawabidiisha na kwamba, yote yanaanza na kupata hitimisho lake kutoka kwa Kristo Yesu anayewakutanisha na hivyo wajibu wao mkubwa ni kumfungulia Kristo Yesu mioyo kila siku ya maisha yao. Upendo kwa Mungu na jirani una maanisha kuakisi upendo wa Mungu kwa kuwapenda jirani wanaoonekana. “Mtu akisema ‘Nampenda Mungu,’ naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo. Kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona” (1 Yoh. 4:20).

Mama Theresa wa Calcutta ni mfano wa Msamaria mwema.
Mama Theresa wa Calcutta ni mfano wa Msamaria mwema.

Mama Theresa wa Calcutta anasema, kila mtu atende kadiri anavyoweza, ili upendo wa Mungu uweze kung’ara sehemu mbalimbali za dunia. Mama Theresa wa Calcutta hata katika udogo wake alijitahidi kuwa ni tone la upendo wa Mungu, mwaliko kwa waamini kutafakari ili hatimaye, waweze kuasiki upendo wa Mungu duniani. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wawe wa kwanza kuchukua hatua ya kupenda kama Mwenyezi Mungu afanyavyo bila kusubiri ulimwengu, jamii na Kanisa litende ili kuleta mabadiliko katika maisha, wala kusubiri kutambuliwa. Kumbe, upendo wa Mungu unatangulia daima. Waamini wawe na moyo wa shukrani kwa Mwenyezi mungu anayewapenda kwanza. Waamini kwa kukutana na Mwenyezi Mungu kila siku katika hija ya maisha yao wanaalikwa kumwachia nafasi ili aweze kuwaletea mageuzi ya ndani, tayari kujizatiti katika mchakato wa kumpenda Mungu na jirani, lakini zaidi maskini, wanyonge na wale wanaowatenda jeuri. Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, waamini wawe tayari kung’oa ndani mwao “ndago” za uchoyo na ubinafsi; chuki, ugumu wa moyo, kumezwa na malimwengu kwa kupenda sana vitu kiasi cha kushindwa kutafakari mng’ao wa upendo wa Mungu. Bikira Maria awasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwilisha kila siku katika uhalisia wa maisha yao, Amri kuu ya upendo.

Fadhila ya Upendo
29 October 2023, 14:57

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >