Papa akabidhi kesi ya Rupnik kwa Baraza la Kipapa husika
Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko alikabidhi Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa jukumu la kuchunguza kesi na "kuamua kuondoa sheria ya mipaka ili kuruhusu kesi kufanyika", kama ilivyoelezwa katika taarifa na Vyombo vya Habari vya Vatican
Tangazo la Wajesuit: Rupnik si sehemu tena ya Kijesuit ilikuwa ni katika Barua ya wazi kutoka kwa Mkuu wa Nyumba na shughuli za Kimataifa za Kijesuit, Roma, Padre Verschueren, juu ya Padre ambaye amri ya kujiuzulu ilitolewa kwake mnamo tarehe 14 Juni 2023.
Kuripoti kutoka kwa Ulinzi wa Watoto
Uamuzi huo, unaelezwa katika taarifa kwa vyombo vya habari, kuwa unakuja baada ya ripoti zilizotumwa mwezi Septemba na Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto Wadogo kwa Papa kuhusu “matatizo makubwa” katika usimamizi wa kesi ya Rupnik na “ukosefu wa ukaribu na waathirika.” Kwa mujibu wa taarifa za Vatican tunasoma tena kuwa: “Papa anaamini kabisa kwamba ikiwa kuna jambo moja ambalo Kanisa linapaswa kujifunza kutoka katika Sinodi ni kusikiliza kwa umakini na huruma kwa wale wanaoteseka, hasa wale wanaohisi kutengwa na Kanisa.”
Tamko la tume ya Ulinzi ya Watoto
Katika muktadha wa maamuzi ya Baba Mtakatifu kuruhusu Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kutazama kesi ya Rupnik aliyekuwa Padre Mjesuit na msanii maarufu, pia kauli kutoka Tume ya Kipapa ya Ulinzi wa Watoto inabainisha kuwa “ Tunapenda kutambua na kupongeza ujasiri na ushuhuda wa wale wote ambao wameteswa na manyanyaso ndani ya Kanisa na kuachwa mikono mitupu wanapotafuta haki.” Kwa njia hiyo “Uamuzi wa Baba Mtakatifu kuruhusu kesi ya kisheria kuendelea katika kesi ya Rupnik ni muhimu, si kwa waathirika tu bali kwa Kanisa zima. Kama Tume, tunabaki na wasiwasi kuhusu michakato ya nidhamu ya Kanisa na mapungufu yake. Tutaendelea kuwa waangalifu katika kuhakikisha utawala wa kutosha wa haki.”
Kujenga utamaduni wa ulinzi
Katika Tamko hilo aidha Tume inabainisha kuwa: “ Hakuna nafasi katika huduma kwa wale ambao wanaweza kukiuka sana wale waliokabidhiwa uangalizi wao. Tunawasihi wale wote wanaotumia aina yoyote ya uongozi kuhakikisha kwamba Kanisa letu ni mahali pa kukaribishwa, kuelewa na kujali kila mtu, kwa upendeleo kwa wale ambao wametengwa katika Kanisa letu.” “Sinodi inapofikia tamati, tunarudia jukumu muhimu ambalo utamaduni wa kulinda unapaswa kutekeleza katika taalimungu yoyote ya huduma, uongozi au ibada. Msingi wa dhamana ya Kanisa ni kumfanya kila mtu kuwa salama, kuwalinda wanyonge kutokana na chochote kinachowatishia, na kuwaongoza kwenye utimilifu wa maisha unaojulikana kwa njia ya ahadi za Mungu mwenyewe. Kujenga utamaduni wa kulinda hubeba Injili katika maisha ya watu, kuleta faraja kwa wale wanaoteseka na kuonyesha ulimwengu uliovunjika ahadi ya Mungu kwamba wote waokolewe.”