Tafuta

“Uchumi wa Francisko” ni dhana ya uchumi unaotekelezwa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu! “Uchumi wa Francisko” ni dhana ya uchumi unaotekelezwa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu!   (ANSA)

Uchumi wa Francisko: Utu, Heshima, Haki Msingi na Utunzaji Bora wa Mazingira

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake uliosomwa kwenye mkutano huu, amejikita zaidi katika Uchumi kama mchakato, uchumi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, nafasi ya wanawake katika uchumi pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anasema, uchumi ni sehemu ya mchakato unaosimikwa katika dhana ya kukubaliana na kusigana; neema na uhuru, haki na upendo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ana matumaini makubwa kwa vijana, wenye uwezo wa kuota ndoto, wanaojiandaa kwa msaada wa Mungu kujenga ulimwengu unaosimikwa katika haki na uzuri. Baba Mtakatifu anasema, “Economy of Francesco” yaani “Uchumi wa Francisko” ni dhana ya uchumi unaotekelezwa katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu! Huu ni uchumi unaohuisha na wala si ule unaowatumbukiza watu katika utamaduni wa kifo. Ni uchumi fungamani unaojikita katika tunu msingi za utu na heshima ya binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kupyaisha mchakato wa uchumi duniani, kwa kujikita katika udugu wa kibinadamu kama alivyokazia Mtakatifu Yohane Paulo II, kwa kuuchagua mji wa Assisi kuwa ni kitovu cha amani na kwa upande wake anataka mji wa Assisi uwe ni jukwaa la mchakato wa mfumo mpya wa uchumi mpya duniani. Baba Mtakatifu anasema, uchumi katika maana yake ya ndani ni utawala thabiti wa dunia kama nyumba ya wote, kwa sababu ya mwingiliano na mafungamano yake katika maisha na mahusiano ya watu. Uchumi halisi unasimikwa katika misingi inayowashirikisha watu kwa lengo la kutaka kuinua na kuboresha maisha; kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu badala ya kuabudu na kuthamini fedha. Lengo ni kuondokana na vurugu na ukosefu wa usawa. Rasilimali fedha iwe ni kwa ajili ya huduma makini kwa watu wa Mungu. Faida ya kweli iwe ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Uchumi wa Francisko: Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote
Uchumi wa Francisko: Utunzaji Bora wa Mazingira Nyumba ya Wote

Mkutano wa Nne wa Uchumi wa Francisko “Economy of Francesco”, umeadhimishwa mjini Assisi Ijumaa tarehe 6 Oktoba 2023 kwa kuwashirikisha vijana kutoka sehemu mbalimbali za dunia, walioshiriki kwa njia ya mitandao ya kijamii. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake uliosomwa kwenye mkutano huu, amejikita zaidi katika Uchumi kama mchakato, uchumi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, nafasi ya wanawake katika uchumi pamoja na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii. Baba Mtakatifu anasema, uchumi ni sehemu ya mchakato unaosimikwa katika dhana ya kukubaliana na kusigana; neema na uhuru, haki na upendo na kwamba, kuna haja ya kujitaabisha kufahamu dhamana na utume wa Kanisa katika historia ya ulimwengu mamboleo. Kumbe, kuna haja ya kujenga uchumi unaothamini utu, heshima na haki msingi za binadamu; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; ujenzi wa mshikamano na mafungamano ya kijamii, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, badala ya uchumi kuendelea kujikita katika rasilimali fedha na mishahara minono kwa watu wachache ndani ya jamii.

Uchumi wa Francisko: Utu, heshima na haki msingi za binadamu
Uchumi wa Francisko: Utu, heshima na haki msingi za binadamu

Uchumi unapaswa kuwa ni mahali shirikishi ili kukuza ushirikiano na mshikamano katika kupambana na umaskini kwa kushirikishana rasilimali, amana na utajiri wa dunia hii. Haitawezekana kujenga uchumi unaojali watu, ikiwa kama uchumi huo unahodhiwa na matajiri wachache katika jamii, wakati kuna umati wa watu wanaoogelea katika dimbwi la umaskini wa kutupwa; uchumi unaojikita katika biashara ya silaha, hautaweza kujenga na kudumisha amani duniani; uchumi unaochafua mazingira hauwezi kwenda pamoja na dhana ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kimsingi uchumi unaojikita katika biashara haramu ya silaha utaendelea kuzalisha makundi makubwa ya wakimbizi na wahamiaji, watu wanaoshambuliwa kwa magonjwa na baa la njaa. Kumbe, mchakato wa uchumi bora hauna budi kujikita katika utu, heshima, haki msingi za binadamu sanjari na mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Ni furaha ya Baba Mtakatifu Francisko kuona kwamba, kuna idadi kubwa ya wasichana na vijana wanaoshiriki kikamilifu katika ujenzi wa Uchumi wa Francisko, kwa ajili pamoja na maskini na wale wote wanaosukumizwa eambezoni mwa vipaumbele vya jamii, kwa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki zao msingi, kwa kusimama kidete kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Uchumi wa Francisko: Upendo na mshikamano dhidi ya umaskini na baa la njaa
Uchumi wa Francisko: Upendo na mshikamano dhidi ya umaskini na baa la njaa

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwakabidhi vijana mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kuwataka wawe na ujasiri wa kufanya hija inayowashirikisha katika ujenzi wa uchumi katika maeneo yao. Huu ni mwaliko kwa vijana kuhakikisha kwamba, kamwe hawajifungii katika uchoyo na ubinafsi wao, bali wawe na ujasiri wa kujenga umoja na mshikamano pamoja na wadau wengine, ili kusaidia kuleta ukombozi wa watu wa Mungu kutoka katika zama za kikoloni na ukosefu wa usawa. Huu ni mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kutoa sura kwa miradi ya kicuhumi ili kujenga udugu wa kibinadamu, kwani wao ni waasisi wa maisha mapya ya kiuchumi na maendeleo endelevu ya binadamu!

Uchumi wa Francisko OK
07 October 2023, 15:48