Waraka wa Kitume wa Papa Francisko "Laudate Deum":Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” umechapishwa tarehe 4 Oktoba 2023, Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi na mwanzo wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu inayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Waraka huu wa Kitume umechapishwa baada ya miaka minane tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochapisha Waraka wa “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Kumbe, Waraka wa Kitume wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” unakita ujumbe wake juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi duniani, upinzani na hali ya kuchanganyikiwa, shughuli za kibinadamu, Uharibifu na hatari zake; kukua kwa dhana ya kiteknolojia, tathmini mpya ya matumizi bora ya madaraka; Udhaifu wa sera za kimataifa na umuhimu wa kusanidi upya mfumo wa pande nyingi. Mikutano ya Kimataifa juu ya Mabadiliko ya Tabia nchi, ufanisi na kuanguka kwake; Matarajio ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa COP 28 huko Dubai, 2023. Motisha za maisha ya kiroho: katika mwanga wa imani sanjari na kutembea kwa pamoja katika ushirika na uwajibikaji. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi anasema na kwamba, watu wengi wanaathrika sana mintarafu afya ya binadamu, kazi, upatikanaji wa rasilimali, makazi pamoja na uhamiaji wa nguvu. Haya ni matatizo ya kijamii yanayogusa na kutikisa utu, heshima, haki msingi na maisha ya binadamu.
Athari za mabadiliko ya tabianchi duniani yamepelekea ongezeko la kiwango cha joto duniani na matokeo yake ni mvua kubwa zinazoambatana na mafuriko na sehemu nyingine ukame wa kutisha. Ongezeko la kiwango cha joto duniani kunapelekea kuyeyuka kwa barafu na matokeo yake ni ongezeko la kina cha maji baharini. Kumekuwepo na upinzani pamoja na hali ya kuchanganyikiwa kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari hali ambayo kwa siku za usoni, itawalazimisha watu kuhama kutoka kwenye fukwe za bahari. Taarifa kamili ya matokeo haya zinapaswa kutolewa na kwamba, waathirika wengi zaidi na maskini, ingawa asilimia 50% ya watu matajiri na nchi tajiri ndio wanaochafua zaidi mazingira nyumba ya wote. Kumbe, kuna haja ya kuwekeza katika teknolojia rafiki na mazingira, changamoto kwa wanasiasa na wafanyabiashara kutenda kwa haraka. Baba Mtakatifu katika Warake wake wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” anakaza kusema, shughuli za binadamu zimechangia sana katika uchafuzi wa mazingira bora nyumba ya wote: kwa kuongezeka kwa kiwango cha joto duniani na kwamba, matukio ya milipuko ya volcano ni kwa sababu ya ongezeko la shughuli za binadamu pamoja na uzalishaji mkubwa wa hewa ya ukaa! Uharibifu na hatari zake unazidi kuongezeka kiasi cha chumvi kuongezeka pia na hivyo kuathiri maisha ya viumbe vya majini pamoja na kuyeyuka kwa barafu. Ukataji wa miti ovyo ni hatari sana, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kuwajibika zaidi katika utunzaji wa mazingira nyumba ya wote. Wachunguzi wa mambo wanasema, kumekuwepo na uhusiano wa karibu sana katika kuenea kwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, maisha ya binadamu pamoja na mazingira kwani kila kitu kinamwingiliano na hakuna anayeweza kujiokoa mwenyewe.
Kukua kwa dhana ya kiteknolojia, mintarafu uchumi, fedha na teknolojia na kwamba, wachumi wamejikita katika mchakato wa kutafuta faida kubwa na kwamba, kumekuwepo na matumizi makubwa ya madaraka. Kumbe kuna haja kufanya tathmini mpya juu ya matumizi bora ya madaraka; kwa kuzingatia uwajibikaji unaokita mizizi yake katika tunu msingi za maisha ya kijamii pamoja na kuongozwa na dhamiri nyofu na utamaduni bora. Kumbe kuna haja ya kutengeneza mwingiliano wa mifumo ya asili pamoja na mifumo ya kijamii. Umakini, ukweli na uwazi ni mambo yanayomwezesha mwanadamu kutambua kwamba, kumekuwepo na matumizi mabaya ya madaraka hata dhidi ya binadamu mwenyewe. Huu ni wakati wa kuwekeza katika kanuni maadili na utu wema; kwa kuwekeza zaidi katika maisha, furaha na matumaini kwa kufanya tafakari ya kina kuhusu maana ya maisha, uwepo wa watu duniani, kazi pamoja na dhamana ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anaelezea kuhusu: Udhaifu wa sera za kimataifa na umuhimu wa kusanidi upya mfumo wa pande nyingi kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; utu, heshima na haki msingi za binadamu zinazofumbwa katika upendo, haki na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kutekeleza dhamana na nyajibu mbalimbali zinazoamriwa na Jumuiya ya Kimataifa. Hizi ni juhudi zinazopania kulinda na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; mapambano dhidi ya baa la njaa na umaskini; mambo yanayopekenya na kusigina haki msingi za binadamu. Athari za myumbo wa uchumi kimataifa kati ya mwaka 2007 hadi mwaka 2008 pamoja na kuenea kwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, ni changamoto na mwaliko wa kuondokana na mfumo wa uchoyo na ubinafsi.
Huu ni wito kwa Jumuiya ya Kimataifa anasema Baba Mtakatifu Francisko wa kuwekeza katika kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, amani sanjari na kujikita katika kanuni auni inayoweza kumwilishwa katika masuala ya kimataifa na kwa watu mahalia na kwamba, kuna haja ya kujenga na kudumisha utandawazi unaogusa maisha na utume wa watu wa kawaida. Utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kupewa uzito unaostahili. Kumbe, changamoto mamboleo zinapaswa kushughulikiwa kwa kutumia nyenzo za kimataifa mintarafu: mazingira, afya, utamaduni pamoja na masuala jamii, lakini zaidi, Jumuiya ya Kimataifa ikazie umuhimu wa kuimarisha haki msingi za binadamu, haki za kijamii pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, pamoja na kuwa na waamuzi watakaopitisha maamuzi, kwa kutoa nafasi itakayoweza kunogesha majadiliano katika ukweli na uwazi; mashauriano, usuluhishi, utatuzi wa migogoro pamoja na usimamizi. Kwa maneno mafupi ni mwaliko wa kuimarisha “demokrasia.” Baba Mtakatifu Francisko anazungumzia kuhusu Mikutano ya Kimataifa juu ya Mabadiliko ya Tabianchi, ufanisi na kuanguka kwake. Kunako Mwaka 1992, Umoja wa Mataifa uliandaa Mkutano wa Kimataifa huko Rio de Janeiro, Brazil, ambapo Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, UNFCCC ulipitishwa na Wakala wake wa kuratibu; yaani Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa ya Mabadiliko ya Tabianchi ilianzishwa. Tangu mwaka 1994, wakati mkataba huo ulipoanza kutekelezwa, kila mwaka Umoja wa Mataifa umekuwa ukizileta pamoj nchi zote duniani kwa ajili ya mikutano ya kimataifa ya tabianchi; Wakati wa mikutano hii, Mataifa yamejadili panuzi mbalimbali za Mkataba wa awali ili kuweka vikwazo vya kisheria juu ya udhibiti wa hewa chafu, kwa mfano, Itifaki ya Kyoto mwaka 1997 na Mkataba wa Paris uliopitishwa mwaka 2015, ambapo nchi zote za dunia zilikubali kuongeza juhudi katika kujaribu na kupunguza ongezeko la joto duniani hadi nyuzi joto 1.5 na kuongeza ufadhili kwenye mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano wa 2019 COP25 wa Madrid, Hispania haukupata mafanikio yoyote. Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP26) huko Glasgow nchini Scotland, kuanzia tarehe 31 Oktoba hadi tarehe 12 Novemba 2021 ni mkutano wa kwanza kufanyika baada ya maambukizi makubwa ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, na kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa Makubaliano ya Paris chini ya mkataba wa Umoja wa Mataifa Mabadiliko ya Tabianchi. Bado kumekuwepo na ugumu wa kutekelezwa kwa maazimio ya mkutano huu. Kumekuwepo na dalili za kutaka kubadili mfumo wa uchumi unaozingatia teknolojia rafiki kwa mazingira. Changamoto kubwa ilikuwa ni utekelezaji wa malengo yaliyofikiwa kadiri ya muda uliopangwa. Changamoto ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote haina budi kupewa kipaumbele cha pekee kama ilivyo pia kwa sekta ya afya na vita sehemu mbalimbali za dunia, wito kwa wote ni wongofu wa kiikolojia unaosimikwa katika wongofu wa kijumuiya ili kuleta mabadiliko endelevu na ya kudumu; mambo yanayopaswa pia kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa. Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP27) huko Sharm El-Sheikh, nchini Misri ulikuwa ni sehemu ya mchakato kwa Jumuiya ya Kimataifa kutekeleza kwa vitendo Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP27 ilikuwa fursa muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mambo makuu manne: Kudhibiti, kukabiliana, rasilimali fedha, hasara na uharibifu (Mitigation, adaptation, finance, loss and damage) lakini uliathiriwa kutokana na vita kati ya Ukraine na Urusi na utekelezaji wake ukaathirika vibaya. Baba Mtakatifu Francisko anachambua kuhusu: Matarajio ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa COP 28 huko Dubai, Falme za Kiarabu kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2023. COP28 ilete mabadiliko makubwa katika kipindi hiki cha mpito, mabadiliko ya kudumu kwa kujikita katika matumizi ya nishati ya upepo na jua ili hatimaye kuachana na matumizi ya nishati ya mafuta. Huu ni uwajibikaji wa pamoja, utakaoirejeshea tena Jumuiya ya Kimataifa kuweza kuaminika tena katika maamuzi yake; kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.
Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kuhusu: Motisha za maisha ya kiroho: katika mwanga wa imani sanjari na kutembea kwa pamoja katika ushirika na uwajibikaji kwa kutambua kwamba, imani ya kweli inawatia nguvu wanadamu na kubadilisha maisha; inageuza malengo yao na kuangaza mahusiano yao na watu wengine sanjari na kazi ya uumbaji katika ujumla wake. Imani iwasaidie waamini kutambua changamoto na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoendelea kuhatarisha maisha ya viumbe hai. Huu ni mwaliko wa kusimama na kutafakari uzuri wa kazi ya uumbaji na kuupokea kama ujumbe kutoka kwa Mwenyezi Mungu, tayari kusimama kidete kuilinda, kuitunza na kuiendeleza, kama kielelezo cha uwepo wake angavu. Huu ni wito wa kutembea kwa pamoja na uwajibikaji kwa kuwajibika kutunza kazi ya uumbaji na kuondokana na tabia ya uhabifu wa mazingira nyumba ya wote; kwa kuendelea kujikita katika mchakato wa upatanisho unaofumbatwa katika utu wa binadamu pamoja na tunu msingi za maisha tayari kuunganisha nguvu binafsi pamoja na maamuzi na sera zinazofanywa na Jumuiya ya Kimataifa. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, waendelee kujizatiti katika kupunguza ongezeko la nyuzi joto duniani, kwa kuonesha mabadiliko ya kitamaduni yanayoyopata chimbuko lake katika mabadiliko yanayofanywa na watu wenyewe. Huu ni mwaliko pia wakufanya mabadiliko na kuachana na mazoea pamoja na kufanya maamuzi bora ya kisiasa ambayo yatasaidia mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko anavyohitimisha Waraka wake wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” uliochapishwa tarehe 4 Oktoba 2023, katika Maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Francisko wa Assisi.