Hija ya Kitume ya Papa Francisko COP28 Dubai: Vita na Mazingira
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Vita na athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya mambo yanayohatarisha maisha duniani na hasa kwa vizazi vijavyo. Hii ni kinyume cha mpango wa Mungu ambaye aliumba kila kitu kwa ajili ya kuenzi Injili ya uhai. Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 26 Novemba 2023 kutoka kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha mjini Vatican amesema kwamba, kuanzia tarehe 1 Desemba hadi tarehe 3 Desemba atakuwa Dubai, Falme za Kiarabu ili kushirikishi katika Mkutano wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28 huko Dubai, kwa Mwaka 2023. Tangu wakati huu, anawashukuru waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema wanaomsindikiza kwa sala na sadaka zao sanjari na kuwajibika kwa moyo thabiti kuchukua ulinzi thabiti kwa ulinzi bora wa mazingira nyumba ya wote. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni changamoto inayokita mizizi yake katika misingi ya haki na amani kwa sababu mazingira ni sehemu muhimu sana ya maisha ya mwanadamu. Hiki ndicho kiini cha Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” uliozinduliwa tarehe 18 Juni 2015 mjini Vatican. Baba Mtakatifu anapembua kuhusu madhara ya uharibifu wa mazingira, umuhimu wa wongofu wa kiikolojia na umuhimu wa kuwekeza katika teknolojia rafiki kwa mazingira. Anazungumzia kuhusu haki ya maji safi na salama. Mazingira ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, urithi unaopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ili kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Utunzaji bora wa mazingira hauna budi kwenda sanjari na uwajibikaji na wala maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yasitumike kama nguvu ya kiuchumi kwa ajili ya kunyonya Mataifa mengine wala kuyatumbukiza katika utamaduni wa kifo. Nguvu ya fedha iwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa ijenge utamaduni wa kujadiliana, kuamua na kutenda kwa pamoja. Mapambano ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma ni muhimu, ili kujenga mtandao wa umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni mchakato unaokita mizizi yake katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kama sehemu ya kumbukizi ya Miaka Mitano tangu alipochapisha Waraka wake wa Kitume, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” sanjari na uzinduzi wa Jukwaa la Kazi “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, alipenda kukazia yafuatayo: Kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha Maskini, Utunzaji bora wa mazingira na Jukwaa la kazi ili kutekeleza sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote katika kipindi cha miaka saba kuanzia sasa! Baba Mtakatifu anasema, kunako mwaka 2015 aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema rasilimali na utajiri wa dunia. Leo hii kuna uharibifu mkubwa wa mazingira nyumba ya wote. Janga kubwa la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ni changamoto ya kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini. Kuna mwingiliano mkubwa kati ya afya bora na mazingira anamoishi binadamu. Hapa kuna haja ya kujikita katika wongofu wa kiikolojia kwa kubadili mtindo wa maisha kwa ajili ya ikolojia ya binadamu, tayari kujikita katika ujenzi wa jamii mpya!
Baba Mtakatifu anasema, Jumuiya ya Kimataifa inao wajibu mkubwa kwa vizazi vijavyo, kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Huu ni mwaliko wa kuondokana na ubinafsi unaopelekea matumizi mabaya ya rasilimali na mali ya dunia. Ni wakati wa kujenga utamaduni wa kuheshimu zawadi ya kazi ya uumbaji, kwa kuwa na mtindo mpya wa maisha, unaothamini ikolojia, ili kuwaandalia vijana leo na kesho bora zaidi, ili kuwaachia bustani inayostawi na wala si jangwa linalokatisha tamaa. Baba Mtakatifu anawashukuru wadau mbalimbali walionogesha maadhimisho ya “Mwaka wa Laudato si” uliozinduliwa tarehe 24 Mei 2020 na kuratibiwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu. Kama sehemu ya mchakato wa kufunga rasmi maadhimisho ya “Mwaka wa Laudato si”, Baba Mtakatifu akatangaza uzinduzi wa Jukwaa la Kazi la Laudato si “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, safari shirikishi ya miaka saba, kama sehemu ya mchakato wa kujizatiti kikamilifu katika maendeleo na ikolojia fungamani. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Safari ya Miaka Saba inaongozwa na: Mwono wa ikolojia fungamani, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini; kwa kujielekeza katika uchumi unaosimikwa katika ikolojia; kwa kujikita katika mtindo wa maisha ya kawaida sanjari na kuendelea kukazia elimu na tasaufi ya ikolojia pamoja na ushirikishwaji wa jumuiya! Kuna matumaini makubwa na kama wengi watashiriki na kila upande kuchangia tamaduni, uwezo, uzoefu na mang’amuzi yake, dunia inaweza kubadilika na kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi kadiri ya mpango wa Mungu. Hili ni tukio ambalo Baba Mtakatifu Francisko amelizungumzia, Dominika tarehe 12 Novemba 2023, akiwashuruku wale wote waliojiunga na Jukwaa la Kazi la Laudato si “Laudato si Plaform of Action, LSAP”, ambalo kwa sasa limeingia katika mwaka wake wa pili. Amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusali kwa ajili ya kuombea mafanikio ya Mkutano wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28 huko Dubai, kwa Mwaka 2023.
Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” anakaza kusema, shughuli za binadamu zimechangia sana katika uchafuzi wa mazingira bora nyumba ya wote: kwa kuongezeka kwa kiwango cha joto duniani na kwamba, matukio ya milipuko ya volcano ni kwa sababu ya ongezeko la shughuli za binadamu pamoja na uzalishaji mkubwa wa hewa ya ukaa! Uharibifu wa mazingira na hatari zake unazidi kuongezeka kiasi cha chumvi kuongezeka pia na hivyo kuathiri maisha ya viumbe vya majini pamoja na kuyeyuka kwa barafu. Ukataji wa miti ovyo ni hatari sana, changamoto na mwaliko kwa watu wa Mungu kuwajibika zaidi katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Wachunguzi wa mambo wanasema, kumekuwepo na uhusiano wa karibu sana katika kuenea kwa Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, maisha ya binadamu pamoja na mazingira kwani kila kitu kinamwingiliano na hakuna anayeweza kujiokoa mwenyewe. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” anachambua kuhusu: Matarajio ya Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, huko Dubai, Falme za Kiarabu kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2023. COP28 ilete mabadiliko makubwa katika kipindi hiki cha mpito, mabadiliko ya kudumu kwa kujikita katika matumizi ya nishati ya upepo na jua ili hatimaye, kuachana na matumizi ya nishati ya mafuta.
Huu ni uwajibikaji wa pamoja, utakaoirejeshea tena Jumuiya ya Kimataifa uwezo wa kuaminika tena katika maamuzi yake; kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa kwake na Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan wa Falme za Kiarabu. Kumbe, Baba Mtakatifu ametia nia ya kwenda ili hatimaye, kushiriki kwenye Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28 kuanzia tarehe Mosi Desemba hadi 3 Desemba 2023. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuwasili Dubai Ijumaa tarehe 1 Desemba 2023 majira ya Saa 2:25 za Usiku. Jumamosi tarehe 2 Desemba 2023 majira ya saa 3:15 Asubuhi atahutubia mkutano wa COP28 na jioni atatumia fursa hii kukutana na viongozi mbalimbali wa Serikali wanaohudhuria mkutano wa COP28. Dominika tarehe 3 Desemba 2023 atazindua “Banda la Imani” katika Jiji la Expo, Dubai “Faith pavilion” na baadaye majira ya saa 4:15 Asubuhi atakuwa anaagana na wenyeji wake tayari kuanza safari ya kurejea mjini Vatican, anakotarajia kuwasili majira ya saa 8:30 mchana.