Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Mama ya Makanisa yote ulimwenguni, “Caput et mater omnium ecclesiarum” liliwekwa wakfu na Papa Silvester kunako tarehe 9 Novemba mwaka 324. Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Mama ya Makanisa yote ulimwenguni, “Caput et mater omnium ecclesiarum” liliwekwa wakfu na Papa Silvester kunako tarehe 9 Novemba mwaka 324.  (Vatican Media)

Jubilei Ya Miaka 1700 ya Kutabarukiwa Kanisa Kuu la Mt. Yohane wa Laterano 2023-2024

Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kuanzia tarehe 9 Novemba 2023 hadi tarehe 9 Novemba 2024 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 1700 tangu Kanisa hili lilipotabarukiwa na Papa Silvester kunako tarehe 9 Novemba mwaka 324 maadhimisho ambayo yamezinduliwa rasmi na Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu mkuu Jimbo kuu la Roma tarehe 9 Novemba 2023 kwa Ibada ya Misa Takatifu: Mkazo: Neno la Mungu, Sakramenti na Ibada ya Kuabudu Ekaristi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 8 Novemba 2023 amewakumbusha waamini na mahujaji kwamba, tarehe 9 Novemba 2023, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Kanisa kuu la Jimbo kuu la Roma, changamoto na mwaliko kwa waamini kuamsha hamu ya kila mwamini kuwa ni mawe hai na ya thamani yanayotumiwa kwa ajili ya ujenzi wa Nyumba ya Mungu, yaani Kanisa. Hii ni changamoto na mwaliko wa kujenga Kanisa hai, yaani Jumuiya ya Kikristo katika msingi ambao ni Kristo Yesu mwenyewe. Ni katika muktadha huu, Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kuanzia tarehe 9 Novemba 2023 hadi tarehe 9 Novemba 2024 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 1700 tangu Kanisa hili lilipotabarukiwa na Papa Silvester kunako tarehe 9 Novemba mwaka 324 maadhimisho ambayo yamezinduliwa rasmi na Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu mkuu Jimbo kuu la Roma tarehe 9 Novemba 2023 kwa Ibada ya Misa Takatifu. Katika kipindi cha mwaka mzima, kutafanyika shughuli mbalimbali zenye mwelekeo wa shughuli za kidini, kichungaji, kimsionari na kiliturujia kwa kukazia umuhimu wa Neno la Mungu, ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa; Kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Mama ya Makanisa yote ulimwenguni, “Caput et mater omnium ecclesiarum” lilitabarukiwa na Papa Silvester kunako tarehe 9 Novemba mwaka 324, na kuwekwa chini ya ulinzi wa Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu. Hekalu kama Fumbo la Mwili wa Kristo na waamini wanaalikwa kujengeka juu yake na kwamba, wao ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu kwa sabababu Roho Mtakatifu anaishi na kutenda kazi ndani mwao. Uwepo wa Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni kielelezo na alama ya ulinzi na usalama kwa watu wa Mungu ndani na nje ya Jimbo kuu la Roma. “Kristo Yesu ni yeye yule, jana na leo na hata milele.” Ebr 13:8.

Uzinduzi wa Jubilei ya Miaka 1700 ya Kanisa kuu la Mt. Yohane wa Laterano
Uzinduzi wa Jubilei ya Miaka 1700 ya Kanisa kuu la Mt. Yohane wa Laterano

Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu, tayari Kanisa la Jimbo kuu la Roma kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo, ushirika na amani hata katika ulimwengu mamboleo ambao unasheheni kinzani, migogoro na vita. Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano baadaye, likawekwa pia chini ya ulinzi wa Yohane Mbatizaji, kunako karne ya kumi, wakati wa ukarabati mkubwa. Yohane Mbatizaji ndiye Nabii aliyefunga Agano la Kale, akawa daraja ya Agano Jipya, aliyemwandalia njia na hatimaye, wakati ulipowadia akamtambulisha Kristo Yesu kuwa ni Masiha, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Mtakatifu Yohane Mbatizaji alihubiri juu ya uwepo wa Masiha ambaye atajifunua kwao. Yohane Mbatizaji akawataka watu kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu na hivyo, kuanza kutembea katika mwanga wa maisha mapya kama njia makini ya kuweza kumpokea Masiha wa Bwana, atakayetambulika kwa uwepo wa Roho Mtakatifu juu yake na huyu ndiye atakayebatiza kwa Roho Mtakatifu. Wakati ulipotimia Yesu akajitokeza hadharani kando ya Mto Yordani, baada ya kukaa nyumbani kwao mjini Nazareti kwa muda wa miaka thelathini, ili aweze kubatizwa. Baada ya kubatizwa, Roho Mtakatifu akamshukia Kristo Yesu na mara sauti kutoka mbinguni ikasikika ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa wangu msikieni yeye”, alama ambayo Yohane Mbatizaji alikuwa akiisubiria na kwamba, Kristo Yesu ni Masiha wa Bwana. Kristo Yesu akajionesha kuwa ndiye Mwana kondoo wa Mungu anayeichukua na kuondoa dhambi ya ulimwengu.

Kanisa kuu la Mt. Yohane wa Laterano Makao Makuu ya Jimbo la Roma
Kanisa kuu la Mt. Yohane wa Laterano Makao Makuu ya Jimbo la Roma

Yohane Mbatizaji ndiye aliyemtambulisha kuwa Kristo Yesu ndiye Mwana kondoo wa Mungu na wale wanafunzi wa kwanza wa Yohane Mbatizaji wakawa ni wafuasi wa kwanza wa Yesu! Hawa ndio akina Simone aitwaye Petro, na Andrea nduguye, Yakobo na ndugu yake Yohane, wote hawa walikuwa ni wavuvi kutoka Galilaya kama ilivyokuwa kwa Yesu. Mtakatifu Yohane Mbatizaji ni Nabii aliyetangaza na kusimamia ukweli, aliyekatwa kichwa na wafuasi wake waliposikia wakaja na kuuchukua mwili wake kwenda kuuzika kwa heshima! Hivi ndivyo nyota angavu ya Yohane Mbatizaji, ilivyozimika baada ya kumshuhudia Kristo Yesu, Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za ulimwengu. Yohane Mbatizaji, ni kati ya watu maarufu wa Agano Jipya, anaishia kukatwa kichwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kifodini ni kielelezo cha ukatili wa binadamu dhidi ya watu waaminifu wa Mungu. Na hatimaye, ni Mwinjili Yohane, Mwanafunzi mpendwa wa Kristo Yesu na shuhuda aliyeandika Injili na kwamba, ushuhuda wake ni wa kweli. Rej. Yn 21: 20-25. Wengine ni Mtakatifu Petro na Paulo, Miamba wa imani, waliosadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano limeshuhudia maadhimisho ya Mitaguso mikuu mitano na kwa hakika limekuwa ni kitovu cha hija za kichungaji na maisha ya watu binafsi ili kurejea tena katika msingi wa imani na upendo. Ujenzi wa Kanisa hili ni matunda ya uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu uliotolewa kwa Wakristo kuabudu kadiri ya dini yao na Mfalme Costantino kunako mwaka 313. Hili lilikuwa ni Kanisa la kwanza kujengwa mjini Roma na baadaye, kuanzia mwaka 1565 Makanisa yakaanza kujengwa sehemu mbali mbali. Kanisa hili ndilo Makao makuu ya Jimbo kuu la Roma, ambalo, Baba Mtakatifu ndiye Askofu wake mkuu. Kumbe, Kanisa hili pia ni alama ya utakatifu wa Kanisa, licha ya watoto wake, wakati mwingine, kuogelea katika dimbwi la dhambi. Kanisa ni moja: lina bwana mmoja, laungama imani moja tu, lazaliwa kwa Ubatizo mmoja, lafanywa mwili mmoja, lahuishwa na Roho mmoja, kwa ajili ya tumaini moja. Rej. Efe 4: 3-5, na katika utimilifu wote migawanyiko yote itashindwa. Kanisa ni takatifu kwa sababu muasisi wake ni Mungu aliye mtakatifu sana. Kanisa ni Katoliki latangaza utimilifu wa imani. Kanisa ni la kitume kwa sababu limejengwa juu ya misingi imara ya Mitume kumi na wawili. Kanisa ni moja, takatifu, katoliki na la Kitume. Rej. KKK 866-870.

Papa ndiye Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma
Papa ndiye Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma

Baba Mtakatifu Francisko anayakumbuka Makanisa mahalia ambamo Jumuiya za waamini zinakusanyika kuadhimisha mafumbo ya Kimungu. Uhusiano wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano na Makanisa mahalia usaidie kunogesha furaha kwa kila mwamini ili kutembea pamoja katika huduma ya Injili, sala, ushirika na kama mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo. Itakumbukwa kwamba, tarehe 2 Juni 2024, Jimbo kuu la Roma litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa Daima kulikoanzishwa na Kardinali Ugo Poletti kunako mwaka 1974. Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni mahali ambapo waamini wanakusanyika kusikiliza Neno na kutafakari Neno la Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawashauri waamini: kusoma Neno la Mungu, kulisikiliza na hatimaye, kujitahidi kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao. Katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, Neno la Mungu lipewe kipaumbele cha kwanza, kwa kuandaa mahubiri kuhusiana na Maandiko Matakatifu. Wasomaji wa Neno la Mungu wanapaswa kuandaliwa vyema, ili waweze kulitangaza kwa ukamilifu, kama ilivyo kwa wahudumu wa Ekaristi Takatifu kwa wagonjwa na wazee parokiani. Kanisa ni mahali ambapo waamini wanashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ukweli na upendo kati ya watu wanaoishi nao, kwa kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu unaotengeneza sadaka safi na yenye kumpendeza Mungu. Baba Mtakatifu Benedikto XVI anawahimiza waamini kuyalinda na kuyatunza Makanisa yao, kwani huu ni urithi na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho, kitamaduni na kihistoria pamoja na kutambua kwamba, hata wao wenyewe, miili yao ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Jubilei Miaka 1700

 

11 November 2023, 15:02