Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko aliowaandikia washiriki wa kongamano la Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa Tume ya Kudumu ya Ulinzi wa Maeneo ya Kihistoria na ya Kisanaa mjini Vatican. Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko aliowaandikia washiriki wa kongamano la Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa Tume ya Kudumu ya Ulinzi wa Maeneo ya Kihistoria na ya Kisanaa mjini Vatican.   (ANSA)

Jubilei ya Miaka 100 ya Tume ya Kudumu ya Ulinzi wa Maeneo ya Kihistoria na Kisanaa Vatican

Papa Francisko anasema: Urithi huu wa kitamaduni na kisanii ni ishara ya wazi ya maisha na utume wa Kanisa katika utendaji wake wa Kiliturujia katika kutangaza na kushuhudia imani katika maadhimisho mbalimbali ya maisha ya kiroho, kama kielelezo cha mapendo. Na kwamba, kwa njia ya makumbusho ya Vatican, Kanisa limeunga mkono ulimwengu wa sanaa kwa kuzingatia lugha yake na hivyo kuwa ni chombo cha upendeleo cha maendeleo ya binadamu kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tume ya Kudumu ya Ulinzi wa Maeneo ya Kihistoria na ya Kisanaa ya Vatican ilianzishwa tarehe 27 Juni 1923 na Papa Pio XI. Kwa kupitishwa kwa Sheria ya Ulinzi wa Turathi za Utamaduni ya 2001, chini ya Mtakatifu Yohane Paulo II, Tume ya Kudumu inaitwa kutoa maoni yake juu ya:  Afua zote za ukarabati, ujenzi mpya, miradi ya maonesho na afua za ulinzi zinazofanywa mjini Vatican. Wazo la uhifadhi na ulinzi limeenea sehemu mbalimbali za dunia kwani ni sehemu ya mchakato wa ufahamu wa thamani ya kibinadamu ya urithi wa kitamaduni na kihistoria ambao unapata chimbuko lake nchini Italia, lakini zaidi kutoka Vatican na hivyo kuendelea kujiimarisha katika Sheria za Kimataifa Barani Ulaya na sehemu mbalimbali za dunia. Tangu karne ya kumi na tano, viongozi wakuu wa Kanisa walitoa matamko na amri mbalimbali kwa lengo la kukomesha ongezeko la vitendo uchimbaji wa kiikolojia uliokuwa unafanywa mjini Roma na kwenye miji mikuu Barani Ulaya, ili kujitajirisha na makusanyo ya mambo kale kutoka kwa wafalme, wakuu wa nchi na wasomi. Lakini kati ya Karne ya Kumi na nane na Kumi na tisa kulikuwepo na ukarabati mkubwa uliopelekea hata uharibifu wa mali kale. Ndiyo maana Kanisa likaanzisha mchakato wa uundaji wa kanuni maalum za kisheria, zikapitishwa na baadaye zikafanyiwa marekebisho makubwa. Miongoni mwa sheria hizi ni matumizi ya umma ya urithi wa kitamaduni, dhana inayopata chimbuko lake katika Sheria za Kirumi kwa ajili ya kulinda na kutunza mambo kale kwa ajii ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Urithi huu wa kitamaduni na kisanii ni ishara wazi ya utume wa Kanisa
Urithi huu wa kitamaduni na kisanii ni ishara wazi ya utume wa Kanisa

Hii ni sehemu ya ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko aliowaandikia washiriki wa kongamano la Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa Tume ya Kudumu ya Ulinzi wa Maeneo ya Kihistoria na ya Kisanaa mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, kunako mwaka 2001 Vatican ilipitisha sheria kuhusu ulinzi wa urithi wake wa kitamaduni na ule wa Kiti Kitakatifu ambayo sasa itasasishwa ili kuendana kikamilifu na mabadiliko ya kihistoria, kijamii na Kimataifa. Urithi huu wa kitamaduni na kisanii ni ishara ya wazi ya maisha na utume wa Kanisa katika utendaji wake wa Kiliturujia katika kutangaza na kushuhudia imani katika maadhimisho mbalimbali ya maisha ya kiroho, kama kielelezo cha mapendo. Na kwamba, kwa njia ya makumbusho ya Vatican, Kanisa limeunga mkono ulimwengu wa sanaa kwa kuzingatia lugha yake na hivyo kuwa ni chombo cha upendeleo cha maendeleo ya binadamu kiroho.

Makumbusho ya Vatican ni njia ya uinjilishaji mamboleo
Makumbusho ya Vatican ni njia ya uinjilishaji mamboleo

Kwa hakika, Majumba ya Makumbusho ya Vatican ni fursa ya ajabu katika mchakato wa uinjilishaji, kwa sababu kwa kupitia kazi mbalimbali zinazooneshwa, huwapa wageni ushuhuda makini wa mwingiliano unaoendelea kati ya Mwenyezi Mungu na mwanadamu katika maisha yake na katika historia ya watu wa Mungu. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwatakia waandaaji heri na baraka na hivyo waendelee kuwajibika kwa ari kuu na weledi wa kuonesha uzuri wa sanaa ambayo kwa hakika ni tafakafuri ya umoja, mshikamano na mafungamano kati ya binadamu na Muumba wake. Kwa upande wake, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican amebainisha kwamba, Tume ya Kudumu ya Ulinzi wa Maeneo ya Kihistoria na ya Kisanaa ya Vatican katika kipindi cha miaka mia moja cha uwepo wake, imeendelea kuimarika na kwamba, changamoto kubwa kwa sasa ni kuhakikisha kwamba kuna uratibu mkubwa kwa wafanyakazi wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika Kamati hii. Umuhimu wake umeendelea kujidhihirisha kiasi kwamba, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO limetangaza kwamba, Majumba ya Makumbusho ya Vatican ni sehemu ya urithi wa Dunia.

Jubilei Tume

 

23 November 2023, 14:26