Kumbukumbu ya Waamini Marehemu Wote: Ufufuko wa Wafu, Uzima wa Milele
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa anakiri na kufundisha juu ya “Ufufuko wa wafu na uzima wa milele.” Kumbukumbu ya Waamini Marehemu Wote kwa upande mmoja inagubikwa na huzuni na kwamba, makaburini ni mahali ambapo panaonesha huzuni ya moyo. Ni mahali ambapo waamini wanawakumbuka na kuwaombea ndugu, jamaa na marafiki zao waliotangulia mbele ya haki wakiwa na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Makaburi yanawakumbusha waamini kwamba, hapa duniani wao ni wasafiri na wala hawana makazi ya kudumu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kumbukumbu ya waamini Marehemu ni tukio la matumaini katika ufufuko wa wafu, ndiyo maana waamini wanaendelea kuyapamba makaburi kwa maua. Ni kumbukumbu ambayo imechanganyika kati ya huzuni na matumaini; mambo msingi yanayogubika nyoyo za waamini wanapowakumbuka na kuwaombea Marehemu wao. Matumaini ya ufufuko wa wafu yanawasaidia waamini kuendelea na hija kuelekea katika Fumbo la kifo, hapa kila mtu anashiriki “kivyake vyake.” Kuna baadhi watakabiliana na Fumbo la kifo kwa mateso na mahangaiko makubwa, lakini daima wakiwa na maua ya matumaini ya ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Tangu Kanisa la Mwanzo, Wakristo walijijengea utamaduni wa kuwakumbuka, kuwaenzi na kuwaombea waamini wote Marehemu. Hii ni Ibada inayopata chimbuko lake katika asili ya mwanadamu. Kumbukumbu hii inanogeshwa na Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Rej. Kol 1:18.
Waamini kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo wanajiunga na Kristo Yesu na kuanza kutembea katika mwanga wa Pasaka. Rej. Rum 6:3-4. Huu ni ushirika na Kanisa ambalo bado linasafiri huku bondeni kwenye machozi na watakatifu wa mbinguni. Rej. LG 49. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Novemba, anawakumbuka na kuwaombea waamini wote marehemu “Commemoratio Omnium Fidelium Defunctorum” waliotangulia mbele ya haki wakiwa na alama ya imani na sasa wanapumzika kwenye usingizi wa amani. Kumbukumbu inawasaidia waamini kuwatambua na kuwakumbuka wale waliowatangulia mbele za haki, wakiwa na imani na tumaini la ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele. Hii ni kumbukumbu ya umati mkubwa wa ndugu, jamaa na marafiki walioshiriki kikamilifu katika hija ya maisha ya hapa duniani, lakini leo hii hawapo tena! Kumbukumbu ya kuwaombea waamini wote marehemu ilianza kushika kasi kwenye monatseri na nyumba za kitawa kunako Karne VII na hivyo kuanza kuadhimishwa rasmi tarehe 2 Novemba ya kila mwaka, baada ya kuadhimisha Sherehe ya Watakatifu wote, hapo tarehe Mosi Novemba. Alikuwa Papa Benedikto XV kunako tarehe 10 Agosti 1915 katika Katiba ya Kitume ya “Incruentum Altaris Sacrificium” alitoa ruhusa kwa Mapadre kuweza kuadhimisha Misa tatu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Marehemu Waamini Wote Misa ya kwanza ni kwa ajili ya marehemu wote, misa ya pili ni kwa nia ya Baba Mtakatifu na misa tatu ni kwa ajili ya Padre mwenyewe!
Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, si rahisi sana kufanya kumbukumbu, ili kupitia yaliyotendeka katika maisha, familia, jamii na ulimwengu katika ujumla wake. Lakini, Mama Kanisa anafanya kumbukumbu ya Waamini Marehemu Wote, ili kuwasaidia waamini walio hai bado kutambua historia na asili ya ndugu zao waliolala katika Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, Kristo Yesu ameipitia njia ya Fumbo la kifo na kufungua lango la matumaini ya ufufuko na maisha ya uzima wa milele. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wale, Kristo Yesu amefungua lango la matumaini, linalowawezesha waamini kuingia ndani mwake, ili kulitafakari Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ayubu anakiri kwamba, Mtetezi wake yu hai na atamwona na kulitafakari kwa kina Fumbo la huruma na upendo wake. Baba Mtakatifu anawaalika waamini katika mwezi huu wa Novemba, uliotengwa maalum kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombesa Marehemu wote; kuwakumbuka marehemu wote kwani hawapo tena pamoja nao na kuanza pia kujiandaa kwa ajili ya safari inayoelekea kwenye maisha ya uzima wa milele, kwani Yesu mwenyewe anasema, atawafufua siku ya mwisho! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kumbukumbu hii inasimikwa katika imani na matumaini yanayowawezesha watu kukutana na Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo, aliyewakirimia zawadi ya maisha. Haya ni matumaini yanayobubujika kutoka Yerusalemu ya mbinguni, kielelezo cha: uzuri na upendo mkuu ambao Bwana arusi anautoa kwa bibi arusi, “asali wa moyo wake.”
Kumbe, kumbukumbu na matumaini yawawezeshe waamini kukutana na Mwenyezi Mungu, Muumbaji na Mkombozi, ambaye daima anasubiri kukutana na waja wake! Mama Kanisa anawaombea watoto wake ili watakaswe, ikiwa kama wanahitaji kutakaswa kabla ya kupokelewa mbinguni kwenye maisha na uzima wa milele wakati miili yao inapobaki ardhini ikingoja kurudi kwa Kristo Yesu na ufufuko wa wafu. “Sisi twasadiki ushirika wa waamini wote wa Kristo, wa wale walio bado safarini duniani, wa wale waliokufa ambao wanapata utakaso, wa wale wenye heri ya mbingu, wote pamoja hufanya Kanisa moja tu. Nasi twasadiki kwamba, katika umoja huu, mapendo ya huruma ya Mungu na ya watakatifu wake yasikiliza daima sala zetu.” (KKK 962). Kanisa linasali na kuwaombea waamini marehemu kusudi wapate msaada wa kiroho na waamini walio bado hai wapate matumaini ya uzima ujao mbinguni. Ni muhimu na vema kuwaombea wafu, kwani hata kama wamekufa katika neema na upendo kwa Mungu, inawezekana bado wanahitaji utakaso wa mwisho ili waweze kuingia katika furaha ya uzima wa milele. Mtakatifu Ireneo anasema utukufu wa Mungu ni mwanadamu aliye hai. Maisha ya mwanadamu, mkristo, mbatizwa huwa na aina mbili ya kifo. Kifo cha kwanza ni kwa njia ya Ubatizo na imani: Rej. Rum. 1:6 ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo, tumejiunga na Kristo Yesu aliyekufa na kufufuka kwa wafu. Rej. KKK 628. Sakramenti ya Ubatizo ambao alama yake ya asili na timilifu ni kuzamishwa kunako ashiria bayana kushuka kaburini kwa mkristo anayeifia dhambi pamoja na Kristo Yesu ili aishi maisha mapya kwa kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka. Tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka kwawafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na waamini waenende katika upya wa uzima. Rej. Rum. 6:4; Kol. 2:12.
Baba Mtakatifu Alhamis tarehe 2 Novemba 2023 anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Waamini Marehemu wote kwenye Makaburi ya vita mjini Roma: “Rome War Cemetery in Rome.” Baba Mtakatifu ameonya kuhusu tabia ya baadhi ya watu kufanya dhihaka kuhusu kifo! Kipindi hiki cha Mwezi Novemba kiwe ni fursa ya kusali na kutembelea makaburi, ili kuwasalimia na kuwaombea wale waliolala katika usingi wa amani ili hatimaye kujipatia rehema kamili kwa waamini watakaotimiza masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa! Ijumaa tarehe 3 Novemba 2023, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea: Baba Mtakatifu Benedikto XVI, Makardinali, Mapatriaki, Maaskofu wakuu na Maaskofu waliofariki dunia katika kipindi cha Mwaka 2022-2023. Hawa ni viongozi waliojisadaka kwa ajili ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Sasa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo amewaita kwenye makao ya uzima wa milele kwani yote yamekamilika, “Consummatum est” Fumbo la kifo, liwe ni changamoto kwa watu wote watakatifu wa Mungu kwa ajili ya tafakari, kukesha na kutekeleza dhamana na nyajibu mbalimbali kwa uaminifu na ukamilifu kwa kutambua kwamba, wameteuliwa ili kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Fumbo la kifo ni fursa ya kutafakari kwa kina na mapana Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.