Kutabarukiwa Kwa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano: Miaka 1700
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kila mwaka ifikapo tarehe 9 Novemba, Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano lililoko Jimbo kuu la Roma. Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Mama ya Makanisa yote ulimwenguni, “Caput et mater omnium ecclesiarum” lilitabarukiwa na Papa Silvester kunako tarehe 9 Novemba mwaka 324, na kuwekwa chini ya ulinzi wa Kristo Yesu Mkombozi wa Ulimwengu, baadaye, likawekwa pia chini ya ulinzi wa Yohane Mbatizaji na Mwinjili Yohane. Haya ni matunda ya uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu uliotolewa kwa Wakristo kuabudu kadiri ya dini yao na Mfalme Costantino kunako mwaka 313. Hili lilikuwa ni Kanisa la kwanza kujengwa mjini Roma na baadaye, kuanzia mwaka 1565 Makanisa yakaanza kujengwa sehemu mbali mbali. Kanisa hili ndilo Makao makuu ya Jimbo kuu la Roma, ambalo, Baba Mtakatifu ndiye Askofu wake mkuu. Kumbe, Kanisa hili pia ni alama ya utakatifu wa Kanisa, licha ya watoto wake, wakati mwingine, kuogelea katika dimbwi la dhambi. Kanisa ni moja: lina bwana mmoja, laungama imani moja tu, lazaliwa kwa Ubatizo mmoja, lafanywa mwili mmoja, lahuishwa na Roho mmoja, kwa ajili ya tumaini moja. Rej. Efe 4: 3-5, na katika utimilifu wote migawanyiko yote itashindwa. Kanisa ni takatifu kwa sababu muasisi wake ni Mungu aliye mtakatifu sana. Kanisa ni Katoliki latangaza utimilifu wa imani. Kanisa ni la kitume kwa sababu limejengwa juu ya misingi imara ya Mitume kumi na wawili. Kanisa ni moja, takatifu, katoliki na la Kitume. Rej. KKK 866-870.
Baba Mtakatifu Francisko anayakumbuka Makanisa mahalia ambamo Jumuiya za waamini zinakusanyika kuadhimisha mafumbo ya Kimungu. Uhusiano wa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano na Makanisa mahalia usaidie kunogesha furaha kwa kila mwamini ili kutembea pamoja katika huduma ya Injili, sala, ushirika na kama mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo. Baba Mtakatifu wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 8 Novemba 2023 amewakumbusha waamini na mahujaji kwamba, tarehe 9 Novemba 2023, Mama Kanisa anaadhimisha Kumbukumbu ya Kutabarukiwa kwa Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Kanisa kuu la Jimbo kuu la Roma, changamoto na mwaliko kwa waamini kuamsha hamu ya kila mwamini kuwa ni mawe hai na ya thamani yanayotumiwa kwa ajili ya ujenzi wa Nyumba ya Mungu, yaani Kanisa. Hii ni changamoto na mwaliko wa kujenga Kanisa hai, yaani Jumuiya ya Kikristo katika msingi ambao ni Kristo Yesu mwenyewe. Ni katika muktadha huu, Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kuanzia tarehe 9 Novemba 2023 hadi tarehe 9 Novemba 2024 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 1700 tangu Kanisa hili lilipowekwa wakfu na Papa Silvester kunako tarehe 9 Novemba mwaka 324. Katika kipindi cha mwaka mzima, kutafanyika shughuli mbalimbali zenye mwelekeo wa shughuli za kidini, kichungaji, kimsionari na kiliturujia kwa kukazia umuhimu wa Neno la Mungu, ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa; Kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.
Itakumbukwa kwamba, tarehe 2 Juni 2024, Jimbo kuu la Roma litakuwa linaadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa Daima kulikoanzishwa na Kardinali Ugo Poletti kunako mwaka 1974. Ikumbukwe kwamba, Kanisa ni mahali ambapo waamini wanakusanyika kusikiliza Neno na kutafakari Neno la Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawashauri waamini: kusoma Neno la Mungu, kulisikiliza na hatimaye, kujitahidi kulimwilisha katika uhalisia wa maisha yao. Katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, Neno la Mungu lipewe kipaumbele cha kwanza, kwa kuandaa mahubiri kuhusiana na Maandiko Matakatifu. Wasomaji wa Neno la Mungu wanapaswa kuandaliwa vyema, ili waweze kulitangaza kwa ukamilifu, kama ilivyo kwa wahudumu wa Ekaristi Takatifu kwa wagonjwa na wazee parokiani. Kanisa ni mahali ambapo waamini wanashiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ukweli na upendo kati ya watu wanaoishi nao, kwa kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu unaotengeneza sadaka safi na yenye kumpendeza Mungu. Baba Mtakatifu Benedikto XVI anawahimiza Waamini kuyalinda na kuyatunza Makanisa yao, kwani huu ni urithi na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho, kitamaduni na kihistoria pamoja na kutambua kwamba, hata wao wenyewe, miili yao ni Mahekalu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hiki ni kielelezo cha upendo na umoja wa Kanisa Katoliki.