Mahojiano Maalum Kati ya Papa Francisko na Kituo cha Televisheni cha RAIUNO: Vita, Wanawake
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Vita kati ya Israeli na Palestina; Uraibu wa vita na chuki dhidi ya Wayahudi; Vita kati ya Urusi na Ukraine; Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; Dhamana na utume wa wanawake katika maisha ya Kanisa; Sinodi ya XVI ya Maaskofu pamoja na Useja; Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa; matatizo, changamoto na fursa kwa Kanisa lijalo, Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, Imani na Afya. Kati ya wachezaji mahiri wa mpira kutoka Argentina, Baba Mtakatifu anasema anamshabikia sana Pelè. Hizi ni kati ya tema zilizojadiliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko katika mahojiano maalum kati yake na Bwana Gian Marco Chiocci, Mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Televishen cha Taifa, RAIUNO na kurushwa tarehe Mosi Novemba 2023. Baba Mtakatifu Francisko kuhusu vita kati ya Israeli na Palestina anasema, vita ni dalili za kushindwa kwa mwanadamu na kwamba, waathirika zaidi ni watu wasiokuwa na hatia, watoto, wazee na wanawake, wanaochukuliwa mateka. Kuna haja ya kuheshimu mikataba ya Kimataifa inayoruhusu Waisraeli na Wapalestina kuishi kwa pamoja na kadiri ya Mkataba wa Oslo, lazima kuwepo Serikali mbili, lakini mji wa Yerusalemu lazima uwe na hadhi yake maalum. Ni vyema ikiwa kama nchi hizi mbili zitaheshimu Mkataba wa Amani wa Oslo uliotiwa saini mwaka 1993 kati ya Yasser Arafat Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi cha Palestina, [Palestine Liberation Organization (PLO)] na Bwana Yitzhak Rabin, Waziri mkuu wa Israel. Baba Mtakatifu amegusia madhara makubwa yanayoendelea kusababishwa na vita kati ya Israeli na Palestina kwenye Ukanda wa Gaza na kwamba, haya ni matokeo ya kushamiri uwekezaji katika silaha.
Baba Mtakatifu anafuatilia kwa karibu sana vita inayoendelea kati ya Israel na Palestina huko Ukanda wa Gaza. Shirika la Masista Wamisionari wa Upendo, maarufu kama Masista wa Mama Theresa wa Calcutta ndio wanaotoa huduma kwa wagonjwa na majeruhi wa vita. Baba Mtakatifu amezungumzia kuhusu uraibu wa vita na chuki dhidi ya Wayahudi. Mwanzoni mwa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro aliitisha siku ya kusali, kufunga na kuombea amani nchini Siria. Hii ni siku iliyopata mafanikio makubwa, kwa Wakristo na Waislam kuweza kusali pamoja kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican, lakini kamwe mwanadamu asizoee vita. Kusambaa kwa vita kati ya Israeli na Palestina kunaweza kusababisha madhara makubwa kwa watu na mali zao. Kumbe, busara ya kibinadamu iwaongeze wakuu wa Mataifa haya kusitisha vita. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, anaguswa sana na vita inayoendelea Ukanda wa Gaza, Kivu nchini DRC, pamoja na Ukraine bila kusahau mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu nchini Myanmar. Vita inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia nyuma yake kuna kiwanda cha kutengeza silaha na kwamba, hiki kiwanda kinachuma fedha sana. Katika vita hii, kumezuka pia chuki dhidi ya Wayahudi, jambo ambalo si la “kupigia debe” hata kidogo. Chuki dhidi ya Wayahudi ilipamba moto wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kiasi cha Wayahudi millioni 6 waliuwawa kikatili, lakini hata leo hii bado watu wanaendekeza vita tu!
Vita kati ya Urusi na Ukraine imepelekea madhara makubwa kwa watu na mali zao; wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; Vita hii imepelekea kupanda zaidi kwa bei ya nishati ya mafuta na hivyo kuibua mnyororo wa kupanda kwa bei za uzalishaji, usafirishaji na ugavi wa bidhaa. Tatizo kubwa zaidi kiuchumi ni kwamba sasa nchi nyingi zimelazimika kutumia fedha nyingi zaidi za kigeni kuagiza nishati ya mafuta kuliko kawaida na hili limeathiri akiba ya fedha za kigeni ya nchi husika na kupunguza matumizi ya fedha ambazo zingetumika kwenye mambo mengine muhimu. Urusi na Ukraine ni wazalishaji na wasambazaji wakuu wa ngano na mazao mengine ya nafaka duniani. Vita hii imeongeza gharama ya mazao ya nafaka na hivyo kupelekea baadhi ya nchi kukosa uhakika na usalama wa chakula. Nchi zile zilizokuwa zinafanya biashara ya moja kwa moja na Urusi pamoja na Ukraine zinajikuta zikiwa na hali ngumu ya kiuchumi kutokana na vita kupamba moto. Mazungumzo kati ya Vatican na pande zinazohusika yamepelekea mateka wa vita kuachiliwa bila masharti na kwamba, Baba Mtakatifu Francisko bado ametia nia ya kutembelea pande hizi za mgogoro wa vita kati ya Ukraine na Urusi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi na usalama wa maisha! Anakiri kwamba, hata yeye amezaliwa katika familia ya wakimbizi na wahamiaji nchini Argentina. Vita kuu ya Pili ya Dunia ilizalisha wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, lakini kwa sasa dunia inaelemewa na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji. Kuna nchi kama Cyprus, Ugiriki, Malta, Italia na Hispania zinatoa hifadhi kwa wimbi kubwa la wakimbizi duniani. Kuna watu wanakabiliana na nyanyaso, ukatili na uvunjwaji wa haki msingi za wakimbizi na wahamiaji, katika changamoto hii, Sweden ni mfano bora wa kuigwa kwa sera na mikakati ya kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji.
Dhamana na utume wa wanawake katika maisha ya Kanisa: Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kuna haja kwa Mama Kanisa kuhakikisha kuwa, anatoa fursa zaidi kwa wanawake kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kutambua kwamba, wanawake wanashiriki kwa ukamilifu zaidi katika utekelezaji wa dira, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji ndani na nje ya Kanisa. Wanawake ni wadau wakuu katika kukoleza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kifamilia, ni watu wenye utajiri mkubwa, wanaoweza kusaidia upatikanaji wa amani na utulivu; wito na utume maalum kwa wanawake. Ziwepo juhudi za makusudi ili kuwahamasisha wanawake kushiriki katika maisha ya hadhara, katika medani mbalimbali za maisha: mahali panapotolewa maamuzi na utekelezaji wa mikakati na sera; kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika maisha ya kifamilia. Wanawake wasaidiwe kufanya maamuzi machungu katika maisha, kwa kuwajibika barabara katika jamii na katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu anasema hivi sasa idadi ya wanawake wenye dhamana na madaraka makubwa ndani ya Kanisa imeongezeka sana mjini Vatican. Shida kubwa ni mwono na mwelekeo wa kitaalimungu katika kuongoza Kanisa, lakini kadiri ya mwelekeo wa Kimaria, Kanisa ni Mama na Mwalimu. Sinodi ya XVI ya Maaskofu pamoja na Useja; Mtakatifu Paulo VI wakati wa hotuba yake ya ufunguzi wa maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Maaskofu alikazia umuhimu wa Mababa wa Sinodi kuimarisha: imani, mapendo na shughuli za kichungaji kwa ajili ya Makanaisa mahalia, Mashirika ya Kitawa na Kanisa la kiulimwengu. Sinodi iwe ni kielelezo cha umoja na mshikamano wa Kanisa; chombo cha ushauri unaotokana na mchango wa familia ya Mungu, ili kumsaidia Khalifa wa Mtakatifu Petro kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa ajili ya Kanisa la Kristo. Sinodi ya Maaskofu kwa kiasi kikubwa ni Baraza la ushauri linalojikita pia katika mchakato wa Kiekumene, kwa kuwapatia wajumbe fursa ya kushirikisha karama na mawazo yao kadiri Roho Mtakatifu anavyowawezesha.
Mababa wa Sinodi ni wawakilishi kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki wenye hadhi na mamlaka kamili, ambao mawazo, tafakari na mchango wao wakati wa maadhimisho ya Sinodi unapaswa kujikita katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa. Mababa wa Sinodi watambue kwamba, Kristo Yesu ndiye kiongozi mkuu wa Kanisa lake na kwamba, wao wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda amini na wachungaji makini wa Watu wa Mungu. Wasaidiwe na mabingwa na wataalam mbalimbali ili waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu na kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Baba Mtakatifu kuhusu Useja anasema ulianza kutekelezwa katika maisha na utume wa Kanisa kunako karne ya kumi na mbili. Kumbe, Sakramenti ya Daraja Takatifu inampatia Padre dhamana ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu “Munera: munus regendi, munus docendi & munus sanctificandi. Haya ni mambo ambayo wale wote wanaodai kwamba, Mapadre waruhusiwe kuoa wanapaswa kuyatafakari kwa kina na hatimaye, kusali ili kumwomba Bwana wa mavuno aweze kupeleka watenda kazi wema, watakatifu na wachapa kazi katika shamba lake. Useja ni kanuni ya maisha, anayochagua mtu wenyewe kwa hiari yake, na yeye anaipenda zaidi na kuichukulia kama ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa na kwa kuwa siyo sehemu ya imani tanzu ya Kanisa, mlango daima iko wazi katika mabadiliko. Kanisa hufundisha kwamba, Padre ni lazima akubali kwa moyo wote na kwa hiari kamili, kuitikia wito wa kujitolea bila ya kujibakiza kama mchumba wa Kanisa, kwa ajili ya utume wa Kanisa, kimsingi kuchukua Kanisa kama mke wake na kusaidia kutekeleza lengo lake. Mapadre ili kuweza kuishi kikamilifu useja wake, wanapaswa kujifungamanisha na jumuiya ya waamini.
Kashfa ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa; matatizo, changamoto na fursa kwa Kanisa lijalo: Baba Mtakatifu Francisko anasema, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ndani ya Kanisa ni kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa kiasi kwamba, haiwezi kamwe kufichwa, kuikataa wala kuibeza kwani ni ukweli usioweza kufumbiwa macho. Ukweli huu unapaswa kupokelewa na hatimaye, kumwilishwa katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, wema na utakatifu wa maisha; kwa kuganga na kutibu madonda ya kashfa ya nyanyaso za kijinsia, tayari kuambata upendo na huruma ya Mungu, ili kuanza upya kwa kuchuchumilia: kanuni maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Lengo kuu ni kuzuia kashfa ya nyanyaso za kijinsia isijitokeze tena ndani ya Kanisa. Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI alijitahidi sana kusafisha nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Mifumo mbalimbali ya nyanyaso za kijinsia inakwenda kinyume cha tunu msingi za Kiinjili, changamoto na mwaliko wa kujenga utamaduni wa kupambana na nyanyaso za kijinsia. Takwimu zinaonesha kwamba, asilimia kati ya 42% hadi 46% ya nyanyaso zinatendeka ndani ya familia na kwamba, Kanisa litaendelea kujiimarisha katika mapambano dhidi ya nyanyaso hizi. Ndani ya Kanisa kuna baadhi ya watu wasiotaka kuona mabadiliko, lakini Mapokeo ya Kanisa hayana budi kukua na kuendelea kukomaa, kama inavyojitokeza kwa adhabu ya kifo ambayo si tena sehemu ya Mafundisho ya Kanisa Katoliki. Kwa hakika, Baba Mtakatifu anasikitishwa na kuogofya na vita.
Baba Mtakatifu Francisko katika Warake wake wa “Laudate Deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” anachambua kuhusu: Matarajio ya Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, huko Dubai, Falme za Kiarabu kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2023. COP28 ilete mabadiliko makubwa katika kipindi hiki cha mpito, mabadiliko ya kudumu kwa kujikita katika matumizi ya nishati ya upepo na jua ili hatimaye, kuachana na matumizi ya nishati ya mafuta. Huu ni uwajibikaji wa pamoja, utakaoirejeshea tena Jumuiya ya Kimataifa uwezo wa kuaminika tena katika maamuzi yake; kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28, Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko uliotolewa kwake na Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan wa Falme za Kiarabu. Kumbe, Baba Mtakatifu ametia nia ya kwenda na kushiriki kwenye Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP28 kuanzia tarehe Mosi Desemba hadi 3 Desemba 2023. Baba Mtakatifu anakaza kusema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni wajibu na dhamana ya watu wote. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, katika maisha na utume wake ameendelea kuimarika katika imani, matumaini na mapendo na kwamba, kwa sasa anaendelea kukabiliana na changamoto ya afya, lakini kwa sasa hali yake ni nzuri na anaweza kula bila matatizo yoyote. Diego Armando Maradona (30 Oktoba 1960 - 25 Novemba 2020) alikuwa mchezaji maarufu wa mpira wa miguu kutoka nchini Argentina na Lionel Messi ni mchezaji wa timu ya Taifa ya Argentina. Kati ya hawa wawili, Baba Mtakatifu Francisko anasema, anamshabikia zaidi mchezaji nguli wa Brazil, Pele, kwa jina halisi Edson Arantes do Nascimento, aliyekuwa na moyo mwema na kwa hakika ni gwiji wa mpira wa miguu.