Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Desemba 2023 anawaalika waamini kusali kwa ajili ya watu wenye ulemavu. Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Desemba 2023 anawaalika waamini kusali kwa ajili ya watu wenye ulemavu.  (ANSA)

Nia za Baba Mtakatifu Francisko Kwa Mwezi Desemba 2023: Walemavu

Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Desemba 2023 anawaalika waamini kusali kwa ajili ya watu wenye ulemavu, ili waweze kupewa kipaumbele cha pekee na jamii. Hii ina maana kwa waamini kubadili mtazamo wao na hivyo kujifunua ili kujifunza uwezo na karama za walemavu. Itakumbukwa kwamba, Siku ya Kimataifa ya Watu wenye Ulemevu inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Desemba: Tumeungana katika hatua ya kuokoa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Siku ya Kimataifa ya Watu Wenye Ulemavu Duniani “International Day of Persons with Disabilities (IDPD)” inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 3 Desemba na kwa mwaka huu 2023 kauli mbiu inayonogesha maadhimisho haya ni "Tumeungana katika hatua ya kuokoa na kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu, SDGs kwa, pamoja na watu wenye ulemavu." Hii ni siku iliyoanzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 1992 na azimio la 47/3. Lengo kuu ni kukuza uelewa wa masuala ya ulemavu na kuhamasisha uungwaji mkono kwa ajili ya utu, heshima, haki, ustawi, mafao na maendeleo wa watu wenye ulemavu. Pia inalenga kuongeza ufahamu wa mafanikio yatakayopatikana kutokana na ushirikiano wa watu wenye ulemavu katika kila nyanja ya maisha: Kisiasa, kijamii, kiuchumi na kiutamaduni. Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya maadhimisho haya kwa mwaka 2022 alitoa ujumbe maalum na baadaye akakutana na kuzungumza na watu wenye ulemavu. Katika hotuba yake alikazia zaidi: Utu, heshima na mchakato wa ujenzi wa jumuiya shirikishi na kwamba, Jumuiya za Kikristo ziwe ni mahali ambapo watu wenye ulemavu watajisikia nyumbani kwa kupendwa, kukaribishwa na kuthaminiwa. Baba Mtakatifu anasema, Mama Kanisa katika maisha na utume wake, ameendelea kuwa mstari wa mbele kwa kusimama kidete kulinda, kuendeleza na kudumisha, utu na heshima ya binadamu na kwamba, huu ni wajibu fungamani wa Kanisa na hasa katika Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Walemavu katika shida na mahangaiko yao, haki zao msingi zinapaswa kulindwa. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alikuwa na Uso wa huruma kwa wale wote waliokuwa wametengwa na kusukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Siku ya Walemavu Duniani inaadhimishwa kila mwaka tarehe 3 Desemba
Siku ya Walemavu Duniani inaadhimishwa kila mwaka tarehe 3 Desemba

Jumuiya za Kikristo zinapaswa kujipambanua katika ujenzi wa ujirani mwema, kwa kuzingatia mahitaji msingi kwa watu wenye ulemavu, haki zao msingi pamoja na kuwahakikishia kwamba wanapata pia huduma za maisha ya kiroho, ili hata wao katika ulemavu wao, waweze kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani. Ni wajibu wa watu wa Mungu kujenga jumuiya shirikishi kwa kuondokana na mifumo yote ya ubaguzi, kama kielelezo cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu na ushirika unaosimikwa katika toba na wongofu wa ndani. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jumuiya za Kikristo zitajipambanua katika mchakato wa ujenzi wa jamii shirikishi, hawa ndio wale ambao Kristo Yesu anawapatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake. Walemavu waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na maridhiano kati ya watu; wawe ni ishara ya matumaini katika mchakato wa ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa katika utu na udugu wa kibinadamu. Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Desemba 2023 anawaalika waamini kusali kwa ajili ya watu wenye ulemavu, ili waweze kupewa kipaumbele cha pekee na jamii. Hii ina maana kwa waamini kubadili mtazamo wao na hivyo kujifunua ili kujifunza uwezo na karama za walemavu. Baba Mtakatifu anazialika taasisi mbalimbali kuunda programe zitakazo saidia mchakato wa ushiriki mkubwa kwa watu wenye ulemavu. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, watu wenye ulemavu wanakabiliana na tabia ya kutengwa na jamii kutokana na: Ujinga au maamuzi mbele, mwaliko wa kubadili mtazamo ndani ya Kanisa na katika jamii, ili kuwajengea uwezo wa kushiriki katika fursa mbalimbali kama vile: elimu, ajira na maeneo ambayo wanaweza kushirikisha karama na talanta zao. Kanisa liwe mstari wa mbele katika kuibua sera na mipango jumuishi na kwamba, watu wenye mioyo mizuri wangependa kuwasindikiza walemavu.

Walemavu washirikishwe kikamilifu katika sera na mipango ya jamii
Walemavu washirikishwe kikamilifu katika sera na mipango ya jamii

Naye Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, anasema, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, kila mtu ni fumbo. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alitoa kipaumbele cha pekee kwa watu waliokuwa na ulemavu wa viungo, kisaikolojia na katika maisha ya kiroho na walemavu wakatambua na kuonja kutoka kwa Kristo Yesu: Mkombozi na Ufunuo wa Uso wa Baba mwenye huruma na mapendo. Hata walemavu wanayo haki ya kushiriki katika Neno na Sakramenti za Kanisa na kwa kufuata mfano wa Kristo Yesu, utu, heshima na haki msingi za binadamu zitambulikane na kuheshimiwa kama sehemu muhimu sana za ujenzi na ukuaji wa udugu wa kibinadamu. Kwa upande wake, Padre Frédéric Fornos S.J, Mkurugenzi wa Mtandao wa Utume wa Sala Kimataifa anakaza kusema, nia za jumla za Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Desemba 2023 ni kuwahamasisha walemavu kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, walemavu wanapaswa kujisikia kwamba wanashirikishwa katika programu mbalimbali na wala asiwepo mtu awaye yote anayetengwa. Hivi ndivyo Kristo Yesu alivyotenda katika maisha na utume wake. Ili kufikia lengo hili kuna haja ya kubadilika kifikra, kuwa na maono mapya na jinsi ambavyo waamini wenyewe wanavyoiangalia dunia. Waamini wawe tayari kuwa wazi kwa karama na mapaji ya watu wenye ulemavu ndani na nje ya Kanisa.

Walemavu washirikishwe katika maisha na utume wa Kanisa
Walemavu washirikishwe katika maisha na utume wa Kanisa

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa siku hii amesema ulimwengu unakabiliwa na msururu wa majanga ambayo yanaathiri watu wenye ulemavu hivyo kunahitajika kupatikane suluhu za mageuzi ili kuwezesha kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030, SDGs na kutomwacha mtu yeyote nyuma. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema suala la mageuzi linahitaji mafungamano na ushirikiano mkubwa wa sekta ya umma na binafsi ili kuandaa sera na mikakati ya pamoja kwa kushirikiana na watu wenye ulemavu. “Msingi wa ushirikiano huu lazima uwe na ushirikishwaji kamili wa watu wenye ulemavu ili uweze kujumisha utofauti wao katika michakato yote ya kufanya maamuzi. Ubunifu na teknolojia zinaweza kuwa zana zenye nguvu za kuwajumuisha” amesema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa. Bwana Antonio Guterres ameeleza kwamba, watu wenye ulemavu wakijumuishwa wanaweza kuongeza ufikiaji wa mawasiliano, elimu, na hivyo kupata fursa ya kujifunza mambo msingi katika maisha. Na wanaweza kufungua maeneo mengine mapya kwa watu wenye ulemavu kushiriki katika nguvu kazi na jamii kwa ujumla na kwa usawa. “Lakini ili tuweze kufikia hili la kutumia vyema teknolojia, ni lazima kwanza tuondoe mgawanyiko wa kidijitali na kulinda haki za binadamu katika anga ya kidijitali. Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa kujumuisha Watu wenye Ulemavu unatoa ramani halisi ya kuendeleza ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu na kuwafikia katika kazi zote za Shirika hili. Amesema Guterres na kuongeza kwamba, “Tunafanya haya kuanzia makao makuu hadi mashinani, tunafanya kazi ya kutathmini, kushughulikia na kukuza ufikiwaji wa kidijitali na tunaongoza kuwa mfano wa ujumuishaji wa watu wenye walemavu.” Guterres amehitimisha ujumbe wake kwa kusema katika siku hii na kila siku, iwe ni fursa ya kushirikiana na kushikamana katika kutafuta suluhisho bunifu ili kujenga ulimwengu unaofikiwa na wenye usawa kwa wote bila ubaguzi.

Nia Mwezi Desemba 2023
28 November 2023, 15:48