Papa Francisko:Hakuna vita vinavyostahili machozi ya watoto
Na Angella Rwezaula, - Vatican.
Katika ujumbe mfupi wa Tweet, wa Baba Mtakatifu Francisko katika mitandao ya kijamii, umejikita juu ya kilele cha Siku ya Kimataifa ya Watoto na Vijana duniani kwa 2023 iliyopitishwa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watoto na Vijana mnamo tarehe 20 Novemba 1989. Katika ujumbe huo Baba Mtakatifu anauliza maswali: Je, ni watoto wangapi wananyimwa haki ya msingi ya kuishi na uadilifu wa kimwili na kiakili kutokana na migogoro? Je! ni watoto wangapi wanalazimishwa kushiriki au kushuhudia mapigano na kubeba makovu? Hakuna vita vinavyostahili machozi ya watoto. Papa Francisko amebainisha. Mara kadhaa Baba Mtakatifu amekuwa akizindua miito mingi juu ya watoto wanaoteseka na kunyimwa haki zao kutokana na mizozo ya kivita na vurugu katika dunia iliyochanika vipande vipande na wito wa mwisho ulizinduliwa siku kumi zilizopita mnamo tarehe 10 Novemba 2023 ambapo Baba Mtakati katika ujumbe wake aliowatumia Washiriki wa Jukwaa la VI la toleo la Paris kuhusu amani.https://www.vaticannews.va/sw/pope/news/2023-11/papa-jukwaa-la-vi-la-paris-kuhusu-amani-kusikiliza-mazungumzo-na.html.
Katika ujumbe huo Papa Francisko alisema, “Hakuna vita vinavyostahili machozi ya mama ambaye anaona mtoto wake amekatwa viungo vyake au amekufa.” Papa aliongeza kusema kuwa, “Hakuna vita vinavyostahili kupoteza hata uhai wa mwanadamu mmoja, ambaye ni kiumbe kitakatifu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Muumba; hakuna vita vinavyostahili sumu ya nyumba yetu ya kawaida pamoja; hakuna vita vinavyostahili kukata tamaa kwa wale ambao wanalazimishwa kuondoka nchi yao na kunyimwa, kutoka wakati mmoja hadi mwingine, nyumba zao na mahusiano yote ya familia, marafiki, kijamii na kitamaduni ambayo wamejenga, wakati mwingine kwa vizazi. ” Na zaidi, Papa Francisko mara baada ya sala ya Malaika wa Bwana tarehe 19 Novemba 2023 alisema, Amani inawezekana. “Tusijitoe kwenye vita! Na tusisahau kwamba vita daima, daima, daima ni kushindwa. Watengenezaji wa silaha pekee ndiyo wanaofaidika.”https://www.vaticannews.va/sw/pope/news/2023-11/papa-atoa-wito-kwa-ajili-ya-myanmar-palestina-israel-na-ukraine.html.
Hata hivyo historia ya Siku ya Watoto Duniani ilianzishwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 1954 kama Siku ya Watoto Wote na ambayo huadhimishwa na Jumuiya ya Kimataifa tkila arehe 20 Novemba ya kila mwaka ili kuhamasisha ufahamu miongoni mwa watoto duniani kote, na kuboresha ustawi, maendeleo ya watoto wote. Tarehe 20 Novemba 1959 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Tamko la Haki za Mtoto na Mwaka 1989 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Mkataba wa Haki za Mtoto. Tangu 1990, Siku ya Watoto Duniani pia inaadhimisha kumbukumbu ya tarehe ambayo Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio na Mkataba wa haki za watoto. Kwa hiyo mikataba ya Haki za Watoto ni moja za mikataba iliyotazamwa sana ulimwenguni.