Sikukuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume, Mlinzi, Mwombezi na Msimamizi wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, inayoadhimishwa na Makanisa yote kila mwaka ifikapo tarehe 30 Novemba. Sikukuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume, Mlinzi, Mwombezi na Msimamizi wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, inayoadhimishwa na Makanisa yote kila mwaka ifikapo tarehe 30 Novemba.  (ANSA)

Sikukuu ya Mtakatifu Andrea Mtume: Mchakato wa Ujenzi wa Umoja wa Wakristo

Papa Francisko katika ujumbe wake, amerejea kumbukumbu ya tarehe 6 Januari 1964 Mtakatifu Paulo VI alipokutana na kuzungumza na Patriaki Athenagoras wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli na hivyo kuvunjilia mbali kuta za utengano, hali ya kutoaminiana, chuki na uhasama katika Kanisa kunako mwaka 1054 na huo ukawa na mwanzo mpya wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika hija ya upatanisho ili kujenga mahusiano na ukaribu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo akishirikiana na Askofu mkuu Marek Solczyński, Balozi wa Vatican nchini Uturuki anaongoza ujumbe wa Vatican kwenye maadhimisho ya Sikukuu ya Mtakatifu Andrea, Mtume, Mlinzi, Mwombezi na Msimamizi wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, inayoadhimishwa na Makanisa yote kila mwaka ifikapo tarehe 30 Novemba. Ujumbe huu umeshiriki katika mkesha na hatimaye Liturujia Takatifu ambayo imeongozwa na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu George al Fanar. Baadaye wamekuwa na mazungumzo na Tume ya Sinodi yenye dhamana ya kukuza mahusiano na Kanisa Katoliki na baadaye Kardinali Kurt Koch, amewasilisha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya na hatimaye kusomwa hadharani baada ya maadhimisho ya Liturujia Takatifu.

Majadiliano ya kiekumene ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa
Majadiliano ya kiekumene ni muhimu katika maisha na utume wa Kanisa

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake, amerejea kumbukumbu ya tarehe 6 Januari 1964 Mtakatifu Paulo VI alipokutana na kuzungumza na Patriaki Athenagoras wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli na hivyo kuvunjilia mbali kuta za utengano, hali ya kutoaminiana, chuki na uhasama katika Kanisa kunako mwaka 1054 na huo ukawa ni mwanzo mpya wa majadiliano ya kiekumene yanayosimikwa katika hija ya upatanisho ili kujenga mahusiano na ukaribu, ili hatimaye, kuweza kupata suluhu ya vikwazo vinavyoendelea kukwamisha umoja kamili na unaoonekana wa Kanisa, ili kujenga udugu wa kweli wa Kikanisa. Mtakatifu Paulo VI na Patriaki Athenagoras wa kwanza wanaonesha kwamba ujenzi wa umoja wa Kanisa unasimikwa katika makutano kwa waamini kukaa pamoja; majadiliano ya kirafiki, sala za pamoja na juhudi za pamoja katika kuwahudumia watu mbalimbali wa Mungu wanaoteseka kutokana na umaskini, vita na unyonyaji, huku waamini wakiendelea kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Baba wa mbinguni, katika tumaini la ujio wa Ufalme wa Mungu ulioanzishwa na Kristo Yesu, ili kwa pamoja waamini waweze kutenda matendo ya huruma kwa maongozi ya Roho Mtakatifu.

Maadhimisho ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki
Maadhimisho ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, Makanisa haya mawili yameendelea kujikita katika njia iliyoanzishwa na watangulizi wao, kwa kuendelea kukutana mara kwa mara ili kupyaisha ile furaha ya ndugu kukutana na kukumbatiana. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kumshukuru Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopol kwa kushiriki kikamilifu katika mkesha wa Maadhimisho ya Sinodi ya 16 ya Maaskofu yaliyonogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Ushiriki wake binafsi pamoja na wajumbe kutoka Kanisa la Kiorthodox ni matukio yanayotia moyo na kwamba, haya kimsingi ni matunda ya mwendelezo wa maadhimisho ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa Katoliki. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anatoa mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwomba kwa bidii Mwenyezi Mungu, Baba mwenye rehema, ili kelele za silaha zinazokoleza utamaduni wa kifo na uharibifu zikome na kwamba, Serikali na viongozi wa kidini watafute na kudumisha daima njia ya majadiliano na upatanisho. Watakatifu Petro na Andrea Mitume wawaombee watu wote wa Mungu ili wapate karama za ushirika wa kidugu na amani.

Mtume Andrea

 

 

 

30 November 2023, 15:23